November 24, 2024

Baraza la biashara EAC lataka mipaka isifungwe vita ya corona

Baraza la Biashara la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EABC) limetoa mapendekezo 15 yatakayosaidia kukabiliana na ugonjwa virusi vya Corona katika jumuiya hiyo ikiwemo kuhakikisha mipaka haifungwi ili kufanikisha usafirishaji wa bidhaa na huduma unaendelea kam

  • Baraza la Biashara la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EABC) limesema mipaka ya nchi hizo isifungwe kuruhusu usafirishaji wa bidhaa.
  • Nchi wanachama zibadilishane taarifa na uzoefu wa kupambana na Corona.

Dar es Salaam. Baraza la Biashara la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EABC) limetoa mapendekezo 15 yatakayosaidia kukabiliana na ugonjwa virusi vya Corona katika jumuiya hiyo ikiwemo kuhakikisha mipaka haifungwi ili kufanikisha usafirishaji wa bidhaa na huduma unaendelea kama kawaida katika ukanda huo.

Mpaka jana Machi 26, 2020 nchi nne za jumuiya hiyo za Tanzania, Uganda, Kenya na Rwanda zimethibitisha kuwa na wagonjwa wa virusi hivyo.

Katika tamko la pamoja la wanachama wa EABC linalojumuisha Wakurugenzi Watendaji wa taasisi za sekta binafsi wa kila nchi katika jumuiya hiyo, wameeleza kuwa ugonjwa huo una athari kubwa katika ukuaji wa uchumi.

“Janga la COVID-19 ni changamoto kubwa kwa uchumi wa EAC, umevuruga mnyororo wa thamani wa kimataifa na kanda na hivyo kuathiri biashara, uwezo wa uzalishaji, mifumo ya usambazaji bidhaa na matumizi ya rasilimali,” linaeleza tamko hilo la EABC lililotolewa jana usiku.

Wajumbe wa baraza hilo kutoka nchi sita za EAC za Kenya, Rwanda, Uganda, Sudan Kusini, Burundi na Tanzania wamesema mshikamano unahitajika kutokomeza ugonjwa huo bila kuathiri shughuli za uchumi na uzalishaji.

Wamependekeza kuwa shughuli za mpakani katika jumuiya hiyo ziendelee kama kawaida ikiwemo usafirishaji wa bidhaa na huduma.

Wamesema hilo litawezekana kama nchi wanachama wa EAC zitatengeneza mkakati wa pamoja wa kukabiliana na ugonjwa huo kwa kuweka msisitizo katika biashara na uwekezaji.

Nchi za EAC pia zimeshauriwa kufundishana njia sahihi za kukabiliana na ugonjwa huo unaozidi kuenea duniani ili kuushinda kwa pamoja.

“Baraza la Mawaziri la EAC liendelee kufanya vikao vya mara kwa mara ili kubadilishana taarifa na kushirikiana katika mapambano hayo,” inasomeka sehemu ya tamko hilo.


Zinazohusiana


Baraza hilo pia limezitaka nchi wanachama katika bajeti zao za mwaka huo kuongeza fedha katika sekta za afya, usalama wa chakula, huduma za jamii na kuajiri watumishi wengi wa afya watakaosaidia kupambana na Corona.

Aidha, nchi hizo zimeshauriwa kulegeza Sera za kodi hasa kwenye biashara sambamba na mfumo mzuri wa mnyororo wa thamani wa bidhaa za ndani ili kupunguza utegemezi wa uagizaji wa bidhaa za nje ya jumuiya hiyo.

“Vyama vya sekta binafsi vishirikiane na kubadilishana taarifa kuhusu athari za muda mfupi na mrefu za COVID-19 kwenye biashara,” linaeleza tamko hilo.

Mapendekezo mengine ni kutengeneza mfumo wa haraka na rahisi wa biashara ya mtandaoni utakaosaidia upatikanaji wa bidhaa kwa walaji na malighafi kwa ajili ya viwanda vya ndani.

EABC imesema ikiwa mapendekezo hayo yatatekelezwa yatasaidia ukuaji wa uchumi na uzalishaji, jambo litakalosaidia jumuiya hiyo kuimarika.

Mpaka jana EAC hiyo ilikuwa imeripoti visa 96 vya wagonjwa wa Corona ambapo wanne wamepona na huku Kenya ikitangaza mgonjwa mmoja mwenye umri wa miaka 66 kuwa amefariki kwa maradhi hayo yanayodhidi kuutesa ulimwengu. Mtu huyo aliyefariki Kenya alikuwa pia akisumbuliwa na kisukari, kwa mujibu wa Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Mutahi Kagwe.  

Nchi za Burundi na Sudan Kusini Mpaka sasa hazijathibitisha mgonjwa hata mmoja wa Corona, hata hivyo zimetakiwa kuchukua tahadhari za kuwakinga raia wake.