November 24, 2024

Mikopo kutangaza biashara mtandaoni yazinduliwa Tanzania

Wamiliki wa biashara ndogo ndogo wenye ndoto za kujitanua na kuwafikia watu wengi hasa mtandaoni, sasa wana kila sababu ya kutabasamu kwa sababu mitaji ya kijitangaza inaweza kuwafikia popote walipo Tanzania.

  • Ni kampuni ya GrowthBond ambayo imeingia Tanzania kutoa mikopo na mitaji kwa ajili kuzitangaza biashara ndogo ndogo.
  • Inatoa mikopo kuanzia Sh200,000 hadi Sh115 milioni.
  • Pia inatoa ushauri wa masoko na matangazo kwa biashara zinazochipukia.

Dar es Salaam. Wamiliki wa biashara ndogo ndogo wenye ndoto za kujitanua na kuwafikia watu wengi hasa mtandaoni, sasa wana kila sababu ya kutabasamu kwa sababu mitaji ya kijitangaza inaweza kuwafikia popote walipo Tanzania. 

Kampuni ya GrowthBond  inayotoa mitaji na mikopo kwa biashara ndogo ndogo za nchi za Afrika kuendesha shughuli za masoko mtandaoni imeingia nchini Tanzania ikiwa ni hatua ya kujitanua zaidi kwa wafanyabiashara wenye nia ya kuyafikia masoko wasiyoweza kuyafikia kirahisi.

Meneja Mawasaliano wa kampuni hiyo Arina Zhukova ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa wamezifikia nchi nne za za Afrika za Nigeria, Kenya, Tanzania na Gambia mwaka mmoja uliopita na wamezisaidia kampuni takriban 1,000.

Kwa sasa wanaangazia kufanya kazi na kampuni zinazochipukia za Tanzania ambazo zinazokabiliwa na changomoto ya mitaji ya kutekeleza mipango ya masoko na kujitangaza. 

“Tumezindua huduma zetu Tanzania miezi miwili iliyopita na kuvutia watu binafsi na kampuni kadhaa. Tunatazamia kuungana na wabia nchini Tanzania kuwafikia watu wengi zaidi,” amesema Zhukova.

Licha ya kutoa mitaji na mikopo, kampuni hiyo inatoa elimu na ushauri wa masoko kwa watu binafsi na  biashara ambazo ziko chini yake ili zikue katika viwango vinavyotarajiwa.

Zhukova amesema kampuni hiyo inatoa mikopo kwa njia ya mtandao kuanzia dola za Marekani 100 (Sh230,616) hadi dola 50,000 (Sh115.3 milioni)  kwa ajili ya matangazo ya mtandaoni. 


Zinazohusiana:


Hata hivyo, utoaji wa mikipo na ufadhili wa mitaji hutegemea ukubwa na mikakati ya masoko na kujitangaza kwa kampuni husika.

Mfumo wa GrowthBond unaofanya kazi mtandaoni unaweza kuchambua mahitaji ya mkopo uliowasilisha na kampuni husika kabla ya kushauri kiwango cha mkopo kinachotakiwa kutolewa.

“Tunakagua uuzaji na data ya mapato ya kampuni, mapato ya kila mwezi, faida ya matumizi ya matangazo, na kitengo cha uchumi  kuharakisha mchakato na kufanya uamuzi wa ufadhili kwa dakika, ikilinganishwa na miezi katika mfumo wa benki za kawaida,” amesema.

Kuhakikisha kazi ya utoaji mitaji na mikopo inaenda vizuri, kampuni hiyo inatoa kozi za muda mfupi kuwaandaa mataalam wake wa masoko kufanya kazi na kampuni zilizopata mikopo au mitaji.

Matarajio ya kampuni hiyo inayokua kwa kasi ni kuzifikia kampuni 60,000 mwaka 2022 duniani na kujiimarisha zaidi nchini Tanzania.