Serikali ya Tanzania yaunda kamati tatu kupambana na Corona
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeunda kamati tatu kwa ajili ya kukabiliana na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi ya corona (COVID-19).
- Kamati hizo ni pmaoja na ya Kitaifa ambayo itaongozwa na Waziri Mkuu na itahusisha baadhi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu na Msemaji Mkuu wa Serikali.
- Zitakuwa na wajumbe mbalimbali wataalam wa afya.
- Waziri Mkuu amesema kuwa kinga dhidi ya virusi vya corona iwe ni jambo la kimkakati zaidi kuliko kusubiri kutibu
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeunda kamati tatu kwa ajili ya kukabiliana na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi ya corona (COVID-19).
Majaliwa amezitaja kamati hizo leo (Machi 23, 2020) wakati akizungumza na Mawaziri na Makati Wakuu katika Kikao Kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma.
Kamati hizo ni ya Kitaifa ambayo itaongozwa na Waziri Mkuu na itahusisha baadhi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu na Msemaji Mkuu wa Serikali.
Amesema kamati ya pili ni ya Makatibu Wakuu kutoka sekta husika na itaongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi na kamati ya tatu ni ya Kikosi Kazi cha Taifa ambacho kitaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
“Wajumbe wake wakiwa ni wataalamu akiwemo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,” amesema Majaliwa wakati akitaja wajumbe wa kamati ya tatu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali inaendelea kufanya tathmini ili kuhakikisha inazuia ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona isiweze kusambaa kwa kiasi kikubwa nchini.
Pia, Waziri Mkuu amevishukuru vyombo vya habari nchini kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Serikali katika kuelimisha umma namna ya kujikinga na virusi vya corona.
Zinazohusiana
Amesema kuwa kinga dhidi ya virusi vya corona iwe ni jambo la kimkakati zaidi kuliko kusubiri kutibu, hivyo kwa sasa Serikali imeweka mkazo kwenye kuwahamasisha wananchi kujikinga na virusi hivyo.
“…Mawaziri hakikisheni katika kipindi hiki ziara za kwenda kukagua miradi zielekezwe kwa Wakurugenzi ikibidi kwa Makatibu Wakuu, Mawaziri mnatakiwa mjikite katika kukinga Taifa na corona,” amesema Majaliwa.
Awali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema katika kipindi cha saa 24 jumla ya watu 292,142 duniani walibainika kuwa na virusi vya corona kati yao 12,784 wamefariki.
Pia, katika Bara la Afrika watu 736 wamebainika kuwa na virusi vya corona na kati yake watu 20 wamefariki katika kipindi cha saa 24.
Akizungumzia kwa upande wa Tanzania, Waziri Ummy amesema jumla ya watu 12 walibainika kuwa na virusi vya corona tangu mgonjwa wa kwanza alivyogundulika nchini na kwamba wagonjwa wote hali zao ni nzuri na mmoja amepimwa zaidi ya mara mbili na kubainika kuwa hana virusi.