October 6, 2024

Jukwaa la Wahariri laiomba Serikali kutoa mwongozo kujikinga na Corona nyumba za ibada

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limesema licha ya kuwa Serikali haijasema lolote juu ya mikusanyiko katika nyumba za ibada, wameiomba itoe maelekezo mahususi kwa viongozi wa dini ili wachukue tahadhari za kuwakinga waumini wao dhidi maambukizi ya virusi

  • Limesema maeneo ya ibada yanakuwa na msongamano mkubwa wa watu na ni rahisi waumini kuambikizana virusi hivyo.
  • Pia laiomba Serikali kuweka vifaa vya kunawia mikono vituo vya daladala, mabasi ya mwendokasi, pantoni na kwenye masoko. 
  • Waandishi watakiwa kuwaelemisha zaidi wananchi kuhusu ugonjwa huo. 

Dar es Salaam. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limesema licha ya kuwa Serikali haijasema lolote juu ya mikusanyiko katika nyumba za ibada, wameiomba itoe maelekezo mahususi kwa viongozi wa dini ili wachukue tahadhari za kuwakinga waumini wao dhidi maambukizi ya virusi vya Corona. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Tanzania ina wagonjwa sita wa virusi vya Corona. 

 Ugonjwa huo ambao unasambaa kwa kasi duniani  kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) umepoteza maisha ya watu 7,807 na 191,127 wameambukizwa duniani hadi jana.

 Taarifa ya TEF iliyotolewa leo (Machi 19, 2020) imeeleza kuwa jukwaa hilo limeshtushwa na habari za kuwapo kwa ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) nchini kwa sababu unaua watu na  kuharibu uchumi kwa kiwango kikubwa.

 Hata hivyo, limesema hatua za viongozi na wananchi kujikinga na ugonjwa huo zinatakiwa ziimarishwe ikiwemo kuepuka mikusanyiko. 

 Hata hivyo, limesema hadi sasa Serikali haijazungumzia suala la mikusanyiko ya ibada kama misikiti na makanisani ambako kunakuwa na msongamano mkubwa wa watu na kuitaka itoe mwongozo kuwakinga waumini.  

 “Pamoja na viongozi wa kidini kutoa miongozo ya ibada, tunaiomba serikali itoe maelekezo mahususi kwa viongozi hao ili wachukue hatua madhubuti za kukinga waumini dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona,” amesema Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile katika taarifa hiyo. 


Zinazohusiana


Amesema kwa sasa hatua za haraka zinatakiwa kuchukuliwa hasa katika vituo vya daladala, mwendokasi, pantoni na kwenye masoko kwa sababu katika maeneo hayo hakuna maji ya kunawa mikono kama ambavyo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilivyoagiza. 

“Tunaomba serikali ihakikishe maeneo haya yenye msongamano mkubwa yanawekewa vifaa vya kusafisha mikono kuepusha maambukizi ya Corona,” amesema Balile.

Aidha, Balile amevitaka vyombo vya habari kuufanya ugonjwa wa virusi vya Corona kuwa ajenda ya kudumu hadi utakapotokomezwa kwa kuwekeza nguvu kuandika habari za jinsi ya kuzuia maambukizi na kukabiliana na ugonjwa huo.

“Tunatoa rai kwa waandishi wa habari wote nchini na watu wanaomiliki mitandao ya kijamii zikiwamo blogs, twitter accounts, WhatsApp, Instagram na mitandao mingine ya kijamii kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi bila kuziongezea chumvi,” inasomeka sehemu ya Taarifa ya TEF.