November 24, 2024

Magufuli aagiza safari za nje zipunguzwe kujikinga na virusi vya Corona

Rais John Magufuli amemuagiza Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi kupunguza kutoa vibali kwa watumishi umma kusafiri nje ya nchi huku akiwashauri wananchi wapunguze safari na kuchukua tahadhari muhimu dhidi ya virusi vya corona.

  • Amemuagiza Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi kupunguza kutoa vibali kwa watumishi wa umma kusafiri nje ya nchi isipokuwa kama kuna sababu za msingi.
  • Awataka Watanzania kupunguza safari ndani na nje ya nchi.
  • Watanzania watakiwa kuendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo kwa sababu unasambaa kwa haraka.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemuagiza Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi kupunguza kutoa vibali kwa watumishi umma kusafiri nje ya nchi huku akiwashauri wananchi wapunguze safari na kuchukua tahadhari muhimu dhidi ya virusi vya corona vinavyosambaa kwa kasi duniani.

Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Machi 13, 2020) wakati anazindua karakana kuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kambi ya Jeshi la Wananchi Lugalo Jijini Dar es salaam amesema Tanzania haijapata mgonjwa wa ugonjwa huo mpaka sasa, lakini haiwezi ikajiweka pembeni bila kuchukua hatua za kujikinga.

“Ndugu zangu Watanzania ni vizuri sana tukaendelea kuchukua tahadhari kwa nguvu zote. Ugonjwa huu unaua kwa haraka sana. Niwaombe ndugu zangu Watanzania tusipuuze ugonjwa huu hata kidogo,” amesema Magufuli.

Amewataka Watanzania wanaosafiri ndani na nje ya nchi wasafiri kama safari ni ya lazima na kuongeza kuwa Serikali itatoa vibali vya kusafiri nje ya nchi kwa watendaji kama kuna sababu za msingi.

“Ni lazima tuanze kuchukua hatua juu ya ugonjwa huu. Kwa wale wanaopenda kusafiri sana, kama safari siyo ya lazima sana usisafiri. 

“Nimeshatoa maagizo kwa Katibu Kiongozi hatutoi vibali vya watu kusafiri wanavyotaka lazima pawe na sababu ya msingi ya kusafiri,” amesema Rais Magufuli.


Soma zaidi: 


Amewakumbusha pia viongozi wa Serikali, dini na wananchi kuendelea kuelimishana juu ya tahadhari muhimu za kuchukua kujikinga na ugonjwa huo ambao amesema “ugonjwa huu unaharibu uchumi.”

“Niwaombe Waandishi wa habari, ikiwezekana kila siku Mhariri atoe tahadhari ya ugonjwa wa Corona, angalau maneno mawili matatu,”- amesisitiza Rais Magufuli.

Katika hatua nyingie amewataka Watanzania kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kushikana mikono, kukumbatiana na kupigana mabusu.

Kwa mujibu wa WHO, mpaka jana (Machi 13, 2020) watu 125, 048 walikuwa wameambukizwa ugonjwa wa virusi vya Corona ulimwenguni na vifo vilivyoripotiwa ni 4,613 huku China na Italia zikiathirika zaidi.

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania watoa tahadhari

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umewataka raia wote wa kigeni ambao si wakazi halali wa kudumu wa Marekani na ambao wanapanga kwenda katika nchi hiyo kupitia katika nchi zilizoathirika zikiwemo za Ulaya na China wasitishe safari zao kwa sababu hawataruhusiwa kuingia. 

“Kabla ya kupanga safari ya kwenda Marekani, unashauriwa kuahirisha miadi yako ya mahojiano kwa ajili ya kupata Viza hadi itakapofika siku 14 kabla ya tarehe ya kuondoka katika nchi hizo,” inaeleza taarifa ya ubalozi huo iliyotolewa leo.

Jana Machi 12, 2020, Rais wa Marekani Donald Trump alisitisha safari za raia wa nchi 26 za bara la Ulaya wanaoingia nchini Marekani kwa siku 30 ikiwa ni hatua ya kuikinga nchi hiyo dhidi ya virusi vya Corona.