Matumizi vifungashio vya plastiki mwisho Aprili 30
sdsadsadsadsaBaada ya Serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, sasa imechukua hatua zaidi kwa kutoa muda hadi Aprili 30, 2020 kuwa mwisho wa matumizi wa vifungashio vya plastiki vinavyotumika kufungashia bidhaa ndogo ndogo yakiwemo maji, ka
- Vifungashio hivyo ni vile vinavyotumika kufungashia bidhaa ndogo ndogo yakiwemo maji, karanga na ubuyu.
- NEMC yasema imebaini uwepo wa uzalishaji wa vifungashio hivyo usiozingatia matakwa ya sheria na kanuni.
- Yasema hatua hiyo itawasaidia wawekezaji wanaotengeneza mifuko mbadala.
Dar es Salaam. Baada ya Serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, sasa imechukua hatua zaidi kwa kutoa muda hadi Aprili 30, 2020 kuwa mwisho wa matumizi wa vifungashio vya plastiki vinavyotumika kufungashia bidhaa ndogo ndogo yakiwemo maji, karanga na ubuyu.
Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mhandisi Samuel Mafwenga iliyotolewa leo (Machi 12, 2020) inaeleza kuwa wamebaini vifungashio hivyo vinazalishwa kwa wingi kwa ukubwa mbalimbali na vimekuwa vikitumika kama mifuko ya kubebea bidhaa sokoni.
Dk Mafwenga ameeleza katika taarifa hiyo kuwa katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la wazalishaji wa vifungashio vya plastiki aina ya “tubings” vinavyotumika kufungashia bidhaa kama karanga, ubuyu na barafu, vikiwa havina kibali kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na lakiri (seal) wala alama (label) kama kanuni namba 3 inavyoelekeza.
“Kwa mantiki hiyo, Katika masoko yetu hali inaonyesha kuwa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku imerudi kivingine kama ‘vifungashio’.
“Vifungashio vya plastiki (plastic wrappings) kama vinavyotumika kufungashia maji na vitu vingine havina sifa na NEMC inatoa hadi tarehe Aprili 30, 2020, visionekane sokoni,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Soma zaidi:
- Makamba awatahadharisha wafanyabiashara wanaoendelea kutumia mifuko ya plastiki
- Kanuni za kuzuia mifuko ya plastiki zakamilika
Dk Mafwenga amesema marufuku hiyo itasaidia kuondokana na kero ya kuzagaa kwa mifuko ya plastiki na kupungua kwa vifo vya mifugo.
Pia itasaidia kupungua kwa matumizi yasiyo rasmi ya mifuko ya plastiki katika kufunikia vyakula na kuwashia moto ambayo yanasemekana kuwa kisababishi cha saratani, ugumba na athari nyingine za kimazingira.
“Aidha, faida nyingine ni kujitokeza kwa fursa ya kutumia rasilimali zilizopo nchini zitokanazo na miti, katani, pamba na mazao mengineyo kutengeneza mifuko ya kubebea bidhaa isiyo na athari kiafya na ambayo ikiingia ardhini huoza. Hali kadhalika kuongeza mauzo kwa viwanda vyetu vya ndani vinavyozalisha malighafi ya karatasi,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Tathmini iliyofanyika Disemba 2019, kwa mujibu wa Mhandisi huyo jumla ya vikundi 2,761 vya utengenezaji mifuko ya karatasi vimeanzishwa nchini, ambapo 1028 viko mkoa wa Iringa na 1,733 sawa na asilimia 62 viko jijini Dar es Salaam.
Juni 1, 2019 Serikali alianza kutekeleza marufuku ya matumizi ya plastiki ikihusisha utengenezaji, ununuzi na kuuza ili kunusuru uharibifu wa mazingira, vifo kwa wanyama na kuziba kwa mitaro.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira wa wakati huo, Januari Makamba alisema zoezi la kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki litaenda hatua kwa hatua kabla ya kuondoa kabisa mifuko hiyo nchini.
Huenda hatua iliyochukuliwa leo na NEMC ni muendeleo wa jitihada za kuondoa mifuko yote yenye malighafi ya plastiki ili kulinda mazingira.