November 24, 2024

Mfumuko wa bei Tanzania wakwama kiwango cha Januari 2020

Ripoti ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Februari 2020 inaeleza kuwa kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma ilibaki asilimia 3.7 kama ilivyokuwa Januari.

  • Ripoti ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Februari 2020 inaeleza kuwa kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma ilibaki asilimia 3.7 kama ilivyokuwa Januari.
  • Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Februari umeongezeka kidogo hadi kufikia asilimia 5.9 kutoka asilimia 5.7 ilivyokuwa Februari  2019.
  • baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizopungua bei kwa mwezi Februari 2020, zikilinganishwa na bei za mwezi Februari 2019 ni pamoja na jiko la gesi la kupikia kwa asilimia 2.5 na gharama za huduma za burudani na starehe kwa asilimia moja.

Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Februari 2020 imeendelea kubaki kama ilivyokuwa Junuari mwaka huu jambo linaloonyesha mwenendo imara wa mabadiliko ya bei katika kipindi hicho.

Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na zinazotumiwa na kaya binafsi nchini. 

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Februari 2020 ulikuwa asilimia 3.7 ikiwa ni sawa kabisa na kiwango kilichorekodiwa katika mwaka ulioishia Januari 2020.

Taarifa ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali iliyotolewa  leo (Agosti 9, 2019) imeeleza kuwa hali hiyo imechangiwa na kuongezeka na kupungua kwa bei za baadhi za vyakula na bidhaa zisizo za chakula kwa kipindi kilichoishia Februari 2020.

Licha ya mfumuko wa jumla kubaki tambalale, taarifa hiyo inaeleza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Februari 2020 umeongezeka kidogo hadi kufikia asilimia 5.9 kutoka asilimia 5.7 ilivyokuwa Februari 2019.

“Baadhi ya bidhaa zilizoongezeka bei kwa mwezi Februari zikilinganishwa na Februari 2019 ni pamoja na nyama kwa asilimia 1.6, samaki (asilimia 6.1), mafuta ya kupikia (asilimia 2.8), na machungwa kwa asilimia 9.3.

“Kwa upande mwingine, baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizopungua bei kwa mwezi Februari 2020, zikilinganishwa na bei za mwezi Februari 2019 ni pamoja na jiko la gesi la kupikia kwa asilimia 2.5 na gharama za huduma za burudani na starehe kwa asilimia 1.0,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo. 


Zinazohusiana: 


Mfumuko wa bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki, taarifa inaonyesha kuwa Kenya ilikuwa na kiwango cha juu cha mfumuko wa bei Februari 2020, ambapo kiwango chake kilifikia asilimia 6.4 ikilinganishwa na asilimia 5.8 kwa mwaka ulioishia Februari 2020.

Taarifa ya mfumuko wa bei katika nchi ya Uganda katika mwaka ulioishia Februari 2020, zinaonyesha kuwa mfumuko wa bei umebaki katika kiwango kilekile cha Januari 2020 cha asilimia 3.4.