October 6, 2024

Waziri Mkuu awasimamisha kazi watumishi watatu Korogwe

Ni Mweka Hazina wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Subilaga Kapange pamoja na maafisa wengine wawili kwa sababu wameshindwa kuwasilisha mapato serikalini ya kituo cha mabasi cha Korogwe.

  • Ni Mweka Hazina wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Subilaga Kapange pamoja na maafisa wengine wawili.
  • Wameshindwa kuwasilisha mapato serikalini ya kituo cha mabasi cha Korogwe.
  • Asema Serikali haitawavumilia watumishi wezi, wabadhilifu, wavivu na haitosita kuwachukulia hatua.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mweka Hazina wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Subilaga Kapange pamoja na maafisa wengine wawili wanaosimamia ukusanyaji wa mapato katika kituo cha mabasi cha Korogwe baada ya kushindwa kuwasilisha mapato Serikalini.

Maofisa wengine waliosimamishwa kazi ni Meneja wa kituo cha mabasi Majid Salehe na msaidizi wake Ismail.

“Mnakusanya fedha na kuziweka mfukoni hazipelekwi benki mnazitumia kwa matumizi yenu binafsi na kuna siku inaonesha hamjakusanya chochote, hatuwezi kuvumilia hali hii, hawa wote wakamatwe na wawekwe ndani na hii iwe funzo kwa waweka hazina wote nchini,” ameagiza Majaliwa.

Majaliwa alitoa maagizo hayo jana (Machi 5, 2020) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe na wananchi kwenye mkutano wa hadhara akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Tanga. 

Amesema Halmashauri hiyo ya Mji Korogwe imejenga kituo cha mabasi lakini makusanyo yake hayafikishwi Serikalini huku baadhi ya wazabuni waliopewa kazi hiyo wakiwa hawana hata mikataba jambo linalochangia Halmashauri hiyo kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji. 

Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotolewa jana inaeleza kuwa hadi sasa Halmashauri hiyo imekusanya asilimia 36 tu.

“Kuna siku kituo kinakusanya Sh51,000 tu licha ya mabasi mengi kupita, hata hivyo Februari 27, 2020 hawakukusanya kiasi chochote ina maana hakuna basi lililopita. 

“Februari 28, 2020 walikusanya Sh785,000 na Februari 29, 2020 walikusanya mara mbili Sh500,000 na Sh990,000 lakini fedha zote hizo hazikupelekwa benki,” amesema Majaliwa.


Zinazohusiana: 


Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kulea watumishi wa aina hiyo, hivyo amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe, Nicodemus Bei ahakikishe anakuwa makini katika kufuatilia zinakopelekwa fedha za mapato yanazokusanywa kwenye eneo lake.

Amesema Serikali inataka kila mtumishi wa umma nchini awajibike kwa kufanya kazi kwa bidii na kwamba Serikali ya awamu ya tano haitowavumilia watumishi ambao ni wezi, wabadhilifu, wavivu na haitosita kuwachukulia hatua.

Pia, Waziri Mkuu amewataka Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe wahakikishe wanakuwa wakali katika usimamizi wa makusanyo ya mapato pamoja na matumizi yake.

Kwa uapande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela amesema kufuatia ubadhilifu wa fedha za makusanyo katika kituo cha mabasi Korogwe, tayari ameagiza kukamatwa na kuwekwa ndani kwa Mweka Hazina.

Awali, Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda amemuomba Waziri Mkuu awasaidie kutatua tatizo la ubadhilifu wa fedha za mapato kwani wamejenga kituo kizuri cha mabasi lakini hakiwanufaishi. 

Amesema licha ya mabasi mengi kupita katika kituo hicho mapato wanayoyapa ni kidogo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Chuo cha Ualimu cha Korogwe, Machi 5, 2020. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.