November 24, 2024

Majaliwa abaini mapungufu kituo cha pamoja Tanga

Asema jengo la kituo cha pamoja cha huduma ya forodha katika mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Horohoro mkoa wa Tanga limejengwa chini ya kiwango.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoka kwenye jengo la Kituo cha Pamoja cha Huduma za Fordha cha Horohoro mkoani Tanga wakati alipokitembelea kituo hicho, Machi 2, 2020. Kulia kwa Waziri Mkuu ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Asema jengo la kituo cha pamoja cha huduma ya forodha katika mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Horohoro mkoa wa Tanga limejengwa chini ya kiwango.
  • Ujenzi wa jengo hilo umegharimu Sh7.6  bilioni lakini lina mapungufu ikiwemo kuta zake kuvimba.
  • Awataka wote waliohusika na ujenzi huo wafike ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma Machi 11, 2020.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ameagiza mkandarasi aliyejenga jengo la kituo cha pamoja cha huduma ya forodha katika mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Horohoro mkoa wa Tanga achukuliwe hatua kwa sababu jengo hilo limejengwa chini ya kiwango.

Ujenzi wa jengo hilo umegharimu Sh7.6  bilioni lakini lina mapungufu ikiwemo kuta zake kuvimba.

“Jengo hili kuta tayari zimeshaanza kuvimba, kwa nini majengo ya TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) yanajengwa kwa kiwango cha chini na kwa nini mmeruhusu majengo haya yatumike,” amehoji Majaliwa leo (Machi 2, 2020) wakati akiwa katika ziara ya kikazi wilaya ya Mkinga mkoani Tanga. 

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu amemtaka Afisa Miliki wa TRA, Haruna Sumwa, mkandarasi aliyejenga jengo hilo pamoja na wote waliohusika na ujenzi huo wafike ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma Machi 11, 2020.

“Hapa ni sura ya nchi ni lazima majengo yawe katika hali nzuri, haiwezekani mgeni anaingia na kuhudumiwa katika jengo chakavu, tutachukua hatua kwa yeyote aliyehusika, hizi ni fedha za umma lazima zitumike vizuri,” amesema Majaliwa.


Zinazohusiana:


Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Yona Maki amesema ujenzi wa jengo hilo ulianza Julai 2011 hadi Septemba 2014 na lilianza kutumika Agosti 2015 likiwa na taasisi 16 za Serikali zinazofanyakazi.

Amesema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa nyumba 62 za watumishi, maji safi na salama pamoja na upungufu wa watumishi.

Majukumu ya kituo hicho ni pamoja na kusimamia, kudhibiti uingiaji na utokaji wa raia wa Tanzania na wageni, kufanya doria na misako hasa kwenye vipenyo ambako wale wasiopenda kufuata taratibu hupenda kutumia.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameendelea kusisitiza watu wote wanaoingia nchini kupitia mipaka mbalimbali wapimwe afya zao ili kulikinga Taifa na maambuki ya magonjwa mbalimbali ikiwemo homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.

Pia amewataka wananchi kutoa ushirikiano na Serikali kwa kutoa taarifa za watu wanaoingia nchini bila ya kufuata taratibu. 

“Lazima tulinde nchi yetu katika kupambana na kuzuia magonjwa mbalimbali kwa kuhakikisha watu wote wanaingia nchini wawe salama,” amesisitiza Majaliwa.

Pia, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa Jeshi la Polisi mkoani Tanga kuimarisha doria katika maeneo ya mpakani ikiwa ni pamoja na kukagua maroli kwa kuwa yanahusika na ubebaji wa wahamiaji haramu.