November 24, 2024

Ugonjwa wa Corona unavyopukutisha mifuko ya wanunuzi Kariakoo

Ugonjwa huo uliolipuka nchini China mwishoni mwa Desemba 2019 unaendelea kuwatesa wafanyabiashara ambao wanategemea nchi hiyo kwaajili ya manunuzi ya bidhaa zao.

  • Ndani ya muda mfupi, bidhaa za kutoka China zimezidi kuadimika huku bei zake zikipanda.
  • Wanaoagizia bidhaa nchini China ndiyo waliothirika zaidi huku wanaoagiza mataifa mengine wakizidi kunawiri.
  • Serikali yasema ni wakati wa wazalishaji wa Tanzania kuzalisha kwa wingi na kwa ubora kukidhi mahitaji ya soko.

Dar es Salaam. “Nimechoka! Tangu saa mbili natembea kila duka la vyombo ninachokitafuta sikioni,” amesema Martha Malima aliyekuwa akitafuta karatasi maalumu za kubebea vikombe vya kahawa katika maduka mbalimbali ya Kariakoo jijini Dar es Salaam. 

Licha ya jua kali la saa sita mchana, mfanyabiashara huyo anayemiliki  mgahawa maeneo ya Sinza, yupo sokoni Kariakoo kwa mara ya pili sasa akitafuta bidhaa hiyo ambayo wauzaji wanasema imezidi kuwa adimu. 

Siyo karatasi hizo tu. Martha amesema mbali na kukosa bidhaa hizo ambazo huwa lukuki sokoni, pia katumia zaidi ya saa nne kuzunguka katika maduka hayo katikati ya jiji kusaka mirija ya karatasi ambayo kwa kawaida huipata haraka na kwa bei nafuu. 

“Vinatengenezwa na Wachina sasa kila duka hamna nawaza wateja wangu nitawahudumia vipi,” ameongezea Martha. 

Martha licha ya kuwa hayupo nchini China, bado ni miongoni mwa mamilioni ya watu wanaothirika na madhara ya ugonjwa wa virusi vya Corona (Covid19) kutokana na kuyumba kwa uzalishaji na kuporomoka kwa biashara ya kimataifa baina ya China na mataifa mengine duniani.

Ugonjwa huo uliolipuka nchini China mwishoni mwa Desemba 2019 umeshaua watu zaidi ya 2,600 hadi jana (25 Februari, 2020) huku watu zaidi 80,000 wakiambukizwa ulimwenguni. China ina zaidi ya asilimia ya 97 ya vifo na kesi ya wagonjwa wa ugonjwa huo hatari kwa sasa duniani. 

Hata wakati martha akilalamika na hayo, Muuzaji wa duka la vifaa vya vyombo Shabani Saleh amesema muda siyo mrefu, Watanzania wengi wataungana na Martha kulalamikaa kuadimika na kupanda kwa bei za bidhaa zinazotokea China. 

“Unadhani ni mirija tu? Vikombe? Kila mtu ambaye anaagizia mzigo China analalamika. Siyo wenye mikoba, vitu vya umeme wote wanalalamika biashara hamna,” Saleh amesema huku mkono wake ukionyesha hali ya maduka ya jirani zake.

“Acha tu braza,” amesema Shabani akionyesha kukata tamaa na hali ya biashara yake.

Wapo wafanyabiashara ambao wameuona ugonjwa huo kama fursa na hivyo kununua bidhaa kwa wingi na kuzihifadhi wakisubiri ukame. Picha| Mtandao.

Muuza mikoba Dismas Mushi, ambaye duka lake halina shehena kama ilivyo kawaida, amesema hali iliyopo kwa sasa inakatisha tamaa.

Hali hiyo inatokana na wafanyabiashara wengi kukosa bidhaa kwa kuwa wengi wao wameagiza kutoka China na “oda” zao zimesitishwa kutokana na ugonjwaa huo. 

“Hapa mimi nashukuru hiyo Corona imekuja mzigo wangu ulikuwa tayari kwenye meli. Japo umekawia lakini hali yangu siyo mbaya kama wengine,” amesema Mushi.

Mushi ameeleza kuwa bei ya bidhaa kwa sasa inazidi kupaa huku vitu vikiadimika na baadhi ya wafanyabiashara kufunga maduka.

“Mkoba nilikuwa nauza Sh30,000 hadi Sh35,000  lakini kwa sasa ninauza Sh38,000 hadi Sh40,000  na hizi ni siku chache tangu ugonjwa uanze… sasa mwezi ujao unadhani hali itakuwaje?” amesema. 

Kule mizigo haitoki hata kama ulikuwa umetoa oda, oda hiyo imestishwa na pesa haijarudi,” amesema Mushi ambaye hajui lini janga hilo litaisha.

Mfanyabiashara wa mavazi ambaye ameomba jina lake lisitajwe amesema kwenda nchini China ni mtihani kwani kuna hatua nyingi hadi kufika nchini humo.

Amesema mbali na kuchukua siku 14 kwenye vyumba vya uchunguzi, bado inakuwa ni tishio kwa afya ya mfanyabiashara yeyote kwenda nchini China.

Hata hivyo, mfanyabiashara huyo amesema wakati biashara ikizidi kusuasua kwa baadhi ya wauzaji, wapo wafanyabiashara ambao wameuona ugonjwa huo kama fursa na hivyo kununua bidhaa kwa wingi na kuzihifadhi wakisubiri ukame.

Wakati Saleh na Mushi wakilalamika, hali ni tofauti kwake Ayda Ramathan ambaye anauza duka la vifaa vya umeme vikiwemo taa na frem zake.

Ayda amesema yeye na mumewe hawanunui bidhaa zao China hivyo hawaelewi uchungu wa virusi vya Corona kwenye biashara yao.

“Sisi tunachukulia mzigo wetu Dubai. Alhamdulillah hatujaathirika,” amesema Ayda mwenye duka lake Mtaa wa Swahili.


Zinazohusiana


Wadau wa biashara wanasema ugonjwa huo unaweza kuathiri zaidi ya bishara ya bidhaa kutoka China lakini ni fursa kwa wajasiriamali wa Tanzania kuzalisha zaidi na kwa ubora unaotakiwa sokoni. 

Mwakilishi wa Tanzania kwenye Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC), Raphael Maganga amesema kupanda bei kwa bidhaa kunatokana na mahitaji kuwa mengi zaidi ya bidhaa iliyopo sokoni.

“Wapo wafanyabiashara ambao wanahitaji kununua vitu lakini hawawezi kuenda, hili linaleta madhara kwenye kupanda bei na tunatarajia suala hilo kuendelea kwa miezi sita kwani mahitaji yatakuwa mengi na bidhaa hamna na hivyo bei zitapaa,” amesema Maganga.

Zaidi, mdau huyo wa biasara anasema wafanyabiashara wanapaswa kuelimishwa juu ya umuhimu wa kuwa na sehemu mbalimbali za kununulia bidhaa ikiwemo India na siyo kutegemea sehemu moja ili kuzuia hasara zisizo la lazima. 

“Ukiangalia bidhaa za nchi hiyo (India) unaweza kukuta zina bei ndogo zaidi. Ni masaa matano tu kutoka Dar es Salaam hadi India na inaonekana masoko ya Tanzania na India yanashamiri,” amesema Maganga na kubainisha kuwa tatizo hilo ni fursa kwa wajasiriamali wa Tanzania kuonyesha ubora wa bidhaa zao ambazo zilikuwa na ushindani na bidhaa za China.

Maganga amesema kwa kipindi hiki, Tanzania haitopata shida ya kibiashara tu bali hadi sekta ya utalii kwa kuwa China na Tanzania zilianza kuwa mahusiano mazuri ya kitalii. 

“Tutegemee kushuka kwa watalii kutoka nchi hiyo,” amesema Maganga.

Hata wakati bidhaa za Kichina zikianza kuadimika sokoni, kuna hatua ambazo Wafanyabiashara wanaweza kuzichukua ili kuepuka kufunga maduka yao na kuingia hasara wakati wakisubiri hali kuwa sawa nchini China. 

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa wakati China ikiendelea kutafuta suluhu ya ugonjwa wa Corona wazalishaji wa ndani wanatakiwa kuzalisha kwa wingi bidhaa wanazozishindana na Wachina ili kuwaepusha Watanzania na uhaba huo na kuongeza uzalishaji viwandani.

“Wazalishaji wazalishe zaidi kwa sababu soko lipo kutokana na uhaba wa bidhaa,” amesema Manyanya.

Manyanya amewashauri Watanzania kuwa licha ya ugonjwa huo kuwepo na kuwa tishio kwa nchi nyingi zinazotumia bahari ya Hindi, wapende bidhaa za nyumbani zikiwemo batiki na maisha hayana budi kuendelea.