Thamani ya mauzo soko la hisa Dar yapaa zaidi ya mara 40
Thamani ya mauzo ya wiki nzima katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imepanda zaidi ya mara 40 hadi Sh19.3 bilioni kutoka Sh472.5 milioni iliyorekodiwa juma lililopita
- Thamani ya mauzo ya wiki nzima katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imepanda zaidi ya mara 40 hadi Sh19.3 bilioni kutoka Sh472.5 milioni iliyorekodiwa juma lililopita
- Wachambuzi waeleza soko hilo huenda likafanya vizuri zaidi siku zijazo kutokana na kuongezeka kwa kiwango na thamani ya mauzo ya hisa.
Dar es Salaam. Thamani ya mauzo ya wiki nzima katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imepanda zaidi ya mara 40 hadi Sh19.3 bilioni kutoka Sh472.5 milioni iliyorekodiwa juma lililopita huku wachambuzi wakitabiri mwenendo chanya siku zijazo.
Uchambuzi wa soko kwa wiki iliyoanzia Februari 17 hadi 21, 2020 uliofanywa na kampuni ya udalali ya masoko ya mitaji na dhamana, Zan Securities, unabainisha kuwa thamani ya mauzo katika soko hilo iliongezeka kwa asilimia 3,982 kutoka yale ya wiki iliyopita.
Wiki za DSE hujumuisha siku za kazi pekee yaani Jumatatu hadi Ijumaa.
“TBL (Kampuni ya bia Tanzania) ndiyo kampuni iliyochagiza zaidi ongezeko la mauzo hayo baada ya kurekodi asilimia 94.81 ya thamani ya mauzo yote ikifuatiwa na benki ya CRDB yenye asilimia 4.35,” imesema taarifa iliyotolewa jana (Februari 21, 2020) na Mtendaji Mkuu wa Zan Securities, Raphael Masumbuko.
Zinazohusiana:
- M-pesa, intaneti vyachangia Vodacom Tanzania kupata faida ya Sh90 bilioni
- Wawekezaji wa Acacia soko la hisa Dar tabasamu tupu
- Maumivu kwa wawekezaji wa kampuni ya bia soko la hisa Dar
Masumbuko amesema soko la mitaji lilionyesha matumaini makubwa baada ya thamani ya mauzo kuvuka kikomo cha bilioni licha ya benki ya CRDB haikufanya vizuri katika uuzaji wa hisa zake.
“Licha ya kupungua kwa thamani ya mauzo (ya CRDB), bado soko limetoa sababu zinazotia matumaini ikizingatiwa kuwa kiwango na thamani ya mauzo ya hisa yameongezeka,” amesema Masumbuko katika utabiri wa hali ya soko wiki ijayo.
Wakati thamani ya mauzo yakiongezeka, mtaji wa jumla wa soko hilo umepungua kwa asilimia 1.64 hadi Sh17.3 trilioni kutoka Sh17.6 trilioni iliyorekodiwa wiki iliyopita.