UN yazidi kukipaisha Kiswahili kimataifa
Umoja wa Mataifa (UN) umeipigia chepuo lugha ya Kiswahili kuwa ni miongoni mwa lugha inayozidi kupanuka kimatumizi duniani na kusaidia kueneza utamaduni wake.
- Yasema ni miongoni mwa lugha inayozidi kupanuka kimatumizi duniani.
Dar es Salaam. Umoja wa Mataifa (UN) umeipigia chepuo lugha ya Kiswahili kuwa ni miongoni mwa lugha inayozidi kupanuka kimatumizi duniani na kusaidia kueneza utamaduni wake.
Katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya lugha mama inayoadhimishwa jana (Februari 21, 2020), Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Audrey Azoulay amesema lugha hiyo imevuka mipaka ya kimataifa na kuwafikia watu wengi ulimwenguni.
“ikiwa na wazungumzaji kati ya milioni 120 hadi 150, lugha ya Kiswahili ni moja ya lugha zinazoshamiri kuvuka mipaka ya kule inamozungumzwa. Lugha ya Kiswahili ina maneno kutoka Kusini mwa Afrika, uarabuni, Ulaya na India,” amesema Azoulay katika taarifa iliyotolewa na UN.
Azoulay amesema ikiwa ni lugha ya Taifa na rasmi kwa Tanzania na pia lugha ya taifa Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kiswahili pia kinazungumzwa Burundi, kaskazini mwa Msumbiji, Uganda, Rwanda, kusini mwa Somalia na kwa kiasi fulani Malawi, Sudan Kusini na Zambia.
Soma zaidi:
- Kiswahili ndiyo mpango mzima wa kusaka wateja Tanzania: Ripoti
- Wageni kufunzwa Kiswahili katika Chuo cha Diplomasia
- Kiswahili chapendekezwa kuwa lugha rasmi ya SADC
Mkurugenzi Mkuu huyo wa UNESCO amesema ni kwa kuzingatia athari chanya za lugha ndiyo maana katika maadhimisho ya 22 ya lugha ya mama duniani hii leo maudhui ni lugha bila mipaka ikimulika lugha zote pamoja na lugha mama na mchango wake katika kuleta umoja.
“Kwa kuleta wazungumza pamoja, na kuwawezesha kuchanua na kuchangamka katika muktadha mmoja, lugha mama zinachochoea utangamano wa kijamii, ubunifu na kukuza fikra,” amesema Azoulay.
Aidha, amesema lugha hizo pia zinaimarisha utofauti wa kitamaduni na kuwa chombo cha kujenga amani na zaidi “lugha mama ni muhimu katika jitihada zetu za kufanikisha elimu kwa wote.”