Thamani ya hisa benki ya CRDB zashuka soko la hisa Dar
Huenda leo isiwe siku njema kwa wawekezaji wa kampuni nne katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ikiwemo benki ya CRDB baada ya thamani ya hisa za kampuni hizo kushuka kwa viwango tofauti ikilinganishwa na ilivyokuwa jana.
- Hadi soko linafungwa thamani ya hisa moja ya CRDB ilikuwa ni Sh185 kutoka Sh205 iliyorekodiwa jana.
- Kampuni nyingine ambazo hisa zake zimeshuka ni pamoja na TBL, EABL na kampuni ya habari ya NMG.
Dar es Salaam. Huenda leo isiwe siku njema kwa wawekezaji wa kampuni nne katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ikiwemo benki ya CRDB baada ya thamani ya hisa za kampuni hizo kushuka kwa viwango tofauti ikilinganishwa na ilivyokuwa jana.
Ripoti ya soko ya siku ya DSE ya Februari 19, 2019 inaonyesha kuwa hadi soko linafungwa jioni ya leo CRDB ndiyo iliyofanya vibaya zaidi baada ya thamani ya hisa zake kushuka kwa asilimia 9.76 ambapo imepoteza Sh20 kwa kila hisa moja.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa hadi soko linafungwa thamani ya hisa moja ya CRDB ilikuwa ni Sh185 kutoka Sh205 iliyorekodiwa jana.
Kampuni nyingine ambayo thamani ya hisa zake zimeshuka ni pamoja na kampuni ya habari ya NMG ambayo imeshuka kwa asilimia 2.6 ambapo hadi soko linafungwa hisa moja ya kampuni hiyo ilikuwa inauzwa Sh750 ukilinganisha na Sh770 ya jana.
Zinazohusiana:
- M-pesa, intaneti vyachangia Vodacom Tanzania kupata faida ya Sh90 bilioni
- Wawekezaji wa Acacia soko la hisa Dar tabasamu tupu
- Maumivu kwa wawekezaji wa kampuni ya bia soko la hisa Dar
Pia thamani za hisa za kampuni ya bia ya Afrika Mashariki (EABL) zimeshuka kwa asilimia 1.64 na Jubilee Holdings Limited (JHL) kwa asilimia 0.74.
Wakati thamani ya hisa za kampuni hizo zikishuka, hakuna hata kampuni moja ambayo thamani ya hisa zake imepanda katika soko hilo huku nyingi zikibaki katika viwango vilivyokuwepo jana za zikiwemo Vodacom na benki ya DCB.
Hata hivyo, kampuni ya uwekezaji ya NICO ndiyo iliyofanya vizuri zaidi leo baada ya kuongoza kwa kuuza kiwango kikubwa cha hisa.
NICO imeuza hisa 388,390 sawa na asilimia 63.9 ya hisa zote zilizouzwa sokoni leo ikifuatiwa kwa mbali na benki CRDB ambayo imeuza hisa 181,718 na kampuni ya bia ya TBL (33,680).