October 8, 2024

Ni kweli hutakiwi kuhoji maelekezo anayokupa daktari?

Siyo ukweli, una haki ya kufahamu tiba unayopatiwa na daktari na sababu zake, lakini katika kufanya hivi hauna budi kutumia kauli nzuri ili kuepusha malumbano.

Daktari hatakiwi kukuamuru bali anapaswa kukuomba na kukueleza azma ya kile anachotaka kufanya au sababu ya kile anachokuomba wewe ufanye. Picha|CDC/Unsplash.


  • Siyo ukweli, una haki ya kufahamu tiba unayopatiwa na daktari na sababu zake.
  • Una haki ya kuripoti hali ambayo siyo ya kawaida kuhusu daktari au mhudumu wa afya aliyekuhudumia.
  • Lakini katika kufanya hivi hauna budi kutumia kauli nzuri ili kuepusha malumbano.

Katika pita pita zangu mtandaoni nakutana na mada kuhusu faragha ya mgonjwa na kuhoji anachosema daktari. Wengine wanasema kuwa anachosema au kutaka kufanya daktari ni amri sharti ifuatwe bila kuhoji. 

Yaani maana yake ni kuwa kila kitu atakachokuambia ni ndiyo mzee.

Hata hivyo, wengine wametofautiana wakisema mgonjwa ana haki ya kuongea au kuhoji kuhusu huduma anayopatiwa ikiwemo kuchagua ni nani wa kumuhudumia.

Maagizo au maelekezo ya daktari siyo ndiyo mzee. Mgonjwa una haki ya kuhoji ama kuuliza kile unachotaka kufanyiwa na mhudumu wa afya. Una haki ya kujua ni kwanini anafanya au anataka kufanya kile anachotaka kufanya.

Kwa misingi hiyo, hebu tuangazie leo japo kwa uchache kile ambacho unapaswa kujua pindi uendapo hospitalini au kituo cha afya kupata matibabu.

Una haki ya kumchagua mhudumu unayemtaka. Iwapo unahisi hauko huru kuhudumiwa na mtu uliyepangiwa nae unao uwezo wa kukataa na kuchagua mtu mwingine akufanyie huduma husika.

Lakini katika kufanya hivi hauna budi kutumia kauli nzuri ili kuepusha malumbano. Iwapo hakuna mtu mwingine zaidi ya huyo aliyepo una ruksa ya kuomba mtu wa tatu baina yenu awepo wakati ukipewa huduma ambaye unaamini utakuwa huru naye.

Unaweza kuhoji huduma unayopatiwa. Una haki ya kuuliza na kuhitaji maelezo ya kina ya kile unachofanyiwa au unachotaka kufanyiwa na kujua iwapo kina madhara au la. Hii huanzia kwenye huduma unayopewa, vipimo au dawa nk.

Daktari hatakiwi kukuamuru bali anapaswa kukuomba na kukueleza azma ya kile anachotaka kufanya au sababu ya kile anachokuomba wewe ufanye.


Zinazohusiana:


Katika suala la faragha ambalo watu wengi huliongelea. Iwapo daktari atahitaji wewe kuacha wazi sehemu ya mwili wako au mwili wote, hana budi kukueleza ni  kwanini anataka ufanye hivyo.

Pia daktari anapaswa kukueleza kuacha eneo wazi lile tu analotaka kukagua ama kuangalia kwa ajili ya vipimo na iwapo kuna ulazima wa kukueleza zaidi basi atakuomba na kukwambia ni kwanini. Zingatia, hakuamuru na siyo amri.

Una haki ya kuripoti hali ambayo siyo ya kawaida kuhusu daktari au mhudumu wa afya aliyekuhudumia. Hii ni pamoja na viashiria hatarishi vya kukutaka kingono, maneno na vitendo vilivyo kinyume na maadili.

Katika haya yote, zingatia ya kuwa daktari ni rafiki yako na msiri wako. Kimaadili hapaswi kutoa siri ya mgonjwa bila ridhaa. Lakini pia mgonjwa hauna budi kutambua kuwa ni jukumu lako kuwa muwazi kumueleza daktari wako au mhudumu wa afya kinagaubaga kile kinachokusumbua bila uficho. Hii itasaidia yeye kupata mwanga wa tatizo na namna ya kukusaidia.

Mficha maradhi kifo humuumbua. Ni hayo tu kwa leo.