Jukwaa la wakulima kupata soko la mazao yao labuniwa Tanzania
Ni jukwaa la mtandaoni linalowawezesha wakulima kupata soko la mazao yao katika mikoa mbalimbali nchini na kuwaondolea changamoto ya mazao kuharibika shambani.
- Ni jukwaa la mtandaoni linalowawezesha wakulima kupata soko la mazao yao katika mikoa mbalimbali nchini.
- Pia linawasaidia wakulima kuepuka hasara baada ya mavuno kwa mazao kuharibika kabla ya kufika sokoni.
- Linafanya kazi kama duka la mtandaoni ambapo mnunuzi anapelekewa bidhaa popote alipo.
Dar es Salaam. Huenda wakulima wa Tanzania watafaidika zaidi na kuongeza tija katika kilimo cha mazao, baada ya kubuniwa kwa jukwaa la mtandaoni linalowawezesha kupata soko la uhakika la mazao yao baada ya mavuno.
Wakulima wanaofaidika na jukwaa hilo la Kilimo Fresh ni wa mikoa ya Tanga, Arusha na Morogoro ambapo sasa wana uhakika wa kupata mahali pa kuuzia bidhaa zao kwa lengo la kuwaongezea kipato cha kujikimu na kuboresha maisha ya kila siku.
Jukwaa hilo hutumia njia za kidijitali kuratibu zoezi la ukusanyaji mazao ikiwemo nafaka, mbogamboga, matunda kutoka kwa wakulima na kuzambaza katika hoteli, migahawa, maduka makubwa, taasisi, wauzaji wa jumla na kusafirisha katika masoko ya nje kulingana na uhitaji wa soko.
Pia jukwaa hilo lililobuniwa na vijana wa Tanzania linawawezesha watu na taasisi zenye uhitaji wa mazao kuweka oda zao mtandaoni na baada ya muda hufikishiwa popote walipo.
Inasaidia kuratibu zoezi la ukusanyaji mazao ikiwemo nafaka, mbogamboga, matunda kutoka kwa wakulima. Picha | Kilimo Fresh.
Mwanzilishi wa jukwaa hilo, Baraka Chijenga ameiambia www.nukta.co.tz kuwa kampuni hiyo ilianzishwa kwa lengo kubwa la kutatua changamoto inayowakumba wakulima katika upatikanaji wa masoko ya kuuzia bidhaa zao nchini Tazania.
Amesema siyo tu linatafuta masoko kwa ajili ya mazao ya wakulima bali ni suluhisho la kupunguza hasara baada ya mavuno kutokana changamoto za teknolojia ya uhifadhi na ubora wa mazao yenyewe.
Amesema mpaka sasa wamewafikia wakulima takribani 300 kutoka mikoa ya Tanga, Arusha na Morogoro ikiwa ni hatua ya kutanua mtandao wao katika mikoa yote iliyopo nchini Tanzania.
Ili kuhakikisha lengo lao linatimia, wanafanya kazi na wauzaji bidhaa katika mikoa mingine wanaosaidia kutafuta wakulima wenye changamoto za kupata masoko kwa ajili ya kuuza bidhaa zao.
“Tunafanya kazi na watu mbalimbali kwenye mikoa ya Tanzania kuhakikisha tunawafikia wakulima wengi wanaopata changamoto ya masoko,” amesema Baraka.
- Wabuni jukwaa la mtandaoni linalotatua changamoto za kilimo kwa SMS
- Wakulima washauriwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kilimo cha umwagiliaji
Katika kipindi kifupi cha takriban mwaka mmoja tangu jukwaa hilo lianze kufanya kazi, Baraka amesema changamoto inayowakumba zaidi ni mfumo unaotumika kulipa wakulima kutokua wa kisasa kwani ni lazima wawe na pesa mkononi ndipo wakulima walipwe na siyo tofauti na hapo.
Kilimo fresh inapata faida kwa kuleta bidhaa sokoni na kuuza zaidi ya bei wanayopata kwa wakulima wanapoenda kuichukua bidhaa shambani, japo bado bei zao ni rafiki kwa wanunuaji.
Wakati Kilimo Fresh inayokusudia kuingia ubia na Chama cha Kilimo cha Mazao ya Bustani Tanzania (TAHA) mwanzoni mwa mwezi ujao ili kunufaika na taarifa za wakulima wa vitu mbalimbali bado watakuwa na kibarua cha kutatua changamoto ya usafirishaji wa mazao ya wakulima hadi kwa walengwa walionunua.
Mbali na changamoto hiyo, kampuni hiyo itatakiwa kuhakikisha wanatunza ubora wa bidhaa kutoka kwa wakulima hasa bidhaa zinapotoka mikoa ya mbali kuja Dar es salaam kwa ajili ya kupeleka sokoni.