Hii ndiyo sababu inayoweza kuua biashara yako kwa haraka
Sababu kubwa i ni kukosa kutoa huduma na kuwapa bidhaa bora wateja wako.
- Sababu kubwa iliyopo ni kukosa kutoa huduma bora kwa wateja wako.
- Ipe thamani biashara yako kwa kuwathamini na kuwajali wateja wako.
Dar es Salaam. Wafanyabiashara wenye ndoto ya kuendeleza biashara zao na kuhimili ushindani wa soko la bidhaa wametakiwa kuimarisha mifumo ya kuwahudumia wateja wao kwa kuwathamini na kuwapa bidhaa bora.
Siku zote tabia ya ununuzi ya wateja hubadilika, ni wajibu wa mfanyabiashara kujifunza mbinu za kufikia matarajio ya wateja wake na kutoa huduma zilizo bora kila wakati.
Mchambuzi huru wa masuala ya biashara, Nazareth Eliguard aliyekuwa akizungumza na Nukta (www.nukta.co.tz) amesema mfanyabiashara mzuri ni yule anayetambua umuhimu wa wateja wake kwani ndiyo wanaoipa biashara jina na wana uwezo wa kuinua biashara hiyo katika viwango anavyotaka.
“Ukitoa huduma mbaya kwa mteja mmoja, kumbuka unaweza ukawa umeua soko la watu wengine 10 kwani wateja wana tabia ya kuambizana na mara baada ya kuambizana wanahama wote kwa pamoja,” amesema Eliguard.
- Mbinu zitakazowasaidia wahudumu kuvuta wateja wengi mgahawani
- Biashara ya mtandaoni ni tishio kwa maduka makubwa Tanzania?
Wapo baadhi ya wafanyabiashara waliofanikiwa sana, huridhika na mafanikio waliyoyapa hata kufikia hatua ya kujisahau kuwajali wateja wao, pasipo kujua huo ndiyo mwanzo wa anguko lao.
Eliguard amesema hatua muhimu za kuchukuliwa na wafanyabiashara ni kujenga biashara kwa uangalifu kwa sababu siyo kazi rahisi kujua kila kitu anachopenda mteja wako, lakini mfanyabiashara anaweza kuweka jitihada za kuleta wateja kutokana na huduma bora anazotoa.
Amesema pamoja na matamanio ya kufanikiwa katika biashara, mfanyabiashara ana jukumu la kuongeza thamani ya bidhaa anayouza ili huduma ya mteja anayotoa iwe na maana zaidi.
Naye mwanafunzi anayesomea masuala ya biashara kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam (Tudarco), Emmanuel Asenga amesema kuwa kuna hatari ya biashara kufa mapema ni inatokea pale mfanyabiashara anaposhindwa kutambua kwamba wateja ulionao ni mali na kuwahudumia vile wanavyopaswa kuhudumiwa.
“Ukifanya biashara kwa mazoea lazima ife. Ukijua kuchukulia wateja wako kama “Asset” (mali) kamwe biashara haitoyumba ila ukifanya vinginevyo ni hatari kwani utafunga biashara mapema sana,” amesema Asenga.