October 6, 2024

Wasira amjibu Zitto kuzuiwa mkopo wa Benki ya Dunia

Mwanasiasa mkongwe, Stephen Wasira amesema hoja ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuishawishi Benki ya Dunia kuzuia mkopo wa dola za Marekani milioni 500 kwa Tanzania, siyo jibu pekee la kutatua tatizo la wasichana wanaopata mimba wakiwa shuleni.

  • Asema kuzuia mkopo wa Benki ya Dunia siyo suluhisho pekee la mimba kwa wasichana waliopo shuleni.
  • Asema mkopo huo ungesaidia kuwajengea hosteli wasichana na kuwaepusha na mimba.
  • Awataka watu wamjibu Zitto kwa hoja na siyo kumshambulia yeye binafsi.

Dar es Salaam. Mwanasiasa mkongwe, Stephen Wasira amesema hoja ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuishawishi Benki ya Dunia kuzuia mkopo wa dola za Marekani milioni 500 kwa Tanzania, siyo jibu pekee la kutatua tatizo la wasichana wanaopata mimba wakiwa shuleni. 

Fedha za mkopo huo ambazo ni zaidi ya Sh1.2 trilioni zingeelekezwa katika kushughulikia programu za elimu nchini zikiwemo kujenga miundombinu ya madarasa na ununuzi wa vifaa vya kufundishia.

Hata hivyo, Zitto na wanaharakati wa Tanzania na wa kimataifa waliishinikiza benki hiyo isitoe mkopo huo kwa Serikali kutokana na kile walichokiita kuwa ni sera na sheria ya elimu ya kibaguzi kwa wasichana wanaotapata mimba wakiwa shuleni. 

Wasira aliyekuwa akizungumza leo (Februari 10, 2020) katika kipindi cha Clouds 360 cha televisheni ya Clouds, amesema kupata mimba ni changamoto ya jinsia na msingi wa nchi ni kusomesha watoto wote bila kuwabagua na lazima nchi iangalie namna ya kumaliza tatizo la mimba kwa wasichana waliopo shuleni.  

“Kuzuia Benki ya Dunia isitoe mkopo siyo jibu, mimi ningefikiri vijana wote wangekaa chini pamoja na Zitto tuseme benki lazima itupe pesa. Lakini ili tusaidie wasichana wanaopata mimba tunawasaidiaje? Kuambia kwamba mtarudi shule siyo jibu peke yake, jibu ni kuwazuia wasipate mimba na kuwasaidia,” amesema Wasira.

Wasira ambaye pia ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema Benki ya Dunia itoe mkopo ili isaidie kuboresha elimu ya sekondari na wasichana wapendelewe kwa kujengewa hosteli ili wapate mazingira mazuri ya kusomea.


Zinazohusiana: 


​Amesema katika maeneo ambayo hosteli zimejengwa, mimba zimepungua kwa sababu wasichana wanakaa shuleni na kuepuka vishawishi vya barabarani. 

“Siyo kwamba ilani ilisema zaeni tu mtarudi, Aah wewe! sasa sisi chama kikubwa cha siasa (CCM) tuwaambie wasichana wetu zaeni tu. Kujenga nchi ni kujenga tabia, tunawaambia wasichana someni, vumilieni, fanyeni kazi ya kusoma halafu baadaye mengine yatafuata, tunawajengea mazingira,” amesisitiza Wasira.

Baadhi ya vijana na wanasiasa walishauri Zitto achukuliwe hatua za kisheria na wengine wakishauri auwawe kwa sababu hatua yake kuishawishi Benki ya Dunia isitoe mkopo ni kukosa uzalendo kwa nchi yake. 

Katika hatua nyingine, Mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa Mbunge wa Bunda Mjini mkoani Mara amesema Zitto alikuwa na hoja zake na zimekubaliwa na Benki ya Dunia na hapaswi kushambuliwa binafsi lakini anatakiwa ajibiwe hoja zake.

Amewataka vijana kujenga utamaduni wa kujibu hoja na kuepuka mashindano yasiyo na tija hasa yale yanayohusu uchama kila linapokuja suala lenye maslahi ya kitaifa. 

“Tusikilize hoja na tujibu hoja. Yule mwenye hoja tuachane naye tusikilize unachosema halafu tumjibu. Kama wewe una hoja na sikubaliani na wewe, nitaachana na wewe lakini nitasema hoja yako si sawa. 

“Tusijibu tumekasirika, unajua hasira ni wazimu fulani hivi na ukipata wazimu wa hasira unapoteza mwelekeo wa kutoa sababu,” amesema Wasira. 

Amebainisha kuwa uongozi wa kisiasa unajengwa kwa hoja na kuwasikiliza wengine na kuwataka viongozi wa ngazi za juu kuwasikiliza wanaowaongoza kwa sababu wana hoja ambazo zikifanyiwa kazi zinatachagiza maendeleo ya nchi.