November 24, 2024

Madaktari kukusanya mapato vituo vya afya

Serikali imesema inaendelea kutoa mafunzo ya usimamizi wa fedha kwa Waganga Wafawidhi ili kutatua changamoto ya upungufu wa wahasibu na kuongeza mapato katika zahanati na vituo vya afya nchini Tanzania.

  • Serikali yasema  lengo  ni kukabiliana na upungufu wa wahasibu katika vituo vya afya.
  • Pia itasaidia katika utawala na usimamizi mzuri wa fedha za vituo vya afya.
  • Tamisemi yawasilisha ombi serikalini kuajiri wahasibu wasaidizi wengi zaidi.

Dar es Salaam. Serikali imesema inaendelea kutoa mafunzo ya usimamizi wa fedha kwa Waganga Wafawidhi  ili kutatua changamoto ya upungufu wa wahasibu  na kuongeza mapato katika zahanati na vituo vya afya nchini Tanzania. 

Naibu Waziri Tamisemi, Josephat Kandege ameliambia bunge leo (Februari 5, 2020) jijini Dodoma kuwa watumishi hao wa afya walipatiwa  mafunzo ya utawala na usimamizi wa fedha yaliyofanyika mwaka 2018/19 kwenye kila halmashauri.

“Vituo vya afya na zahanati wamepatiwa mafunzo ya utawala na usimamizi wa fedha yaliyofanyika kuanzia Disemba 24, 2018 hadi Januari 22, 2019 katika kila halmashauri,” amesema Kandege.

Naibu waziri huyo amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wataalam katika masuala mbalimbali ya fedha na utawala katika vituo mbalimbali wanavyovisimamia ili kuongeza mapato.

Usimamizi wa huo wa fedha hufanyika kupitia mfumo wa kielektroniki wa mapato (Facility Financing & Accounting Reporting System) unaosaidia kukabiliana na upungufu wa wataalam wa utawala na usimamizi wa fedha katika zahanati  za halmashauri mbalimbali nchini.

Kandege alikuwa akijibu swali la Mbunge wa viti maalum, Zainab Matitu Vulu ambaye alitaka kujua mikakati ya serikali katika kuwapa elimu ya utawala na usimamizi wa fedha madaktari hao ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.


Zinazohusiana:


Hata hivyo, Kandege amesema Tamisemi imewasilisha maombi ya kibali cha kuajiri zaidi ya watumishi wa kada wahasibu wasaidizi ili kuimarisha huduma za makusanyo ya mapato katika vituo mbalimbali vinavyotoa huduma za afya.

“Ofisi ya rais Tamisemi, imewasilisha maombi ya kibali cha kuajiri zaidi watumishi wa kada za wahasibu wasaidizi kwa lengo la kuimarisha utawala na usimamizi wa fedha kwenye vituo vya kutolea huduma za afya,” amesema Kandege.   

Amesema kwa mwaka 2017/18 Serikali iliajiri wahasibu wasaidizi 335 na kuwapanga katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kuimarisha usimamizi wa fedha na utoaji wa huduma katika vituo hivyo.