October 6, 2024

Fursa zinazoweza kuwapa ahueni vijana wasio na ajira Tanzania

Baada ya kukuletea makala mbalimbali za mambo yanayohusu ajira Tanzania, leo tena tunaendelea kuliangalia suala hilo kwa mapana hasa fursa wanazoweza kuzitumia vijana ambao bado hawajapata kazi.

  • Hauna haja ya kukaa nyumbani bila kazi wakati zipo kazi unazoweza kufanya bila kuhitaji mtaji mkubwa au mtaji kabisa.
  • Kati ya shughuli hizo ni kutumia kipaji chako au kutumia mitandao yako ya kijamii kwa shghuli zinazokuongezea thamani.

Dar es Salaam. Baada ya kukuletea makala mbalimbali za mambo yanayohusu ajira Tanzania, leo tena tunaendelea kuliangalia suala hilo kwa mapana hasa fursa wanazoweza kuzitumia vijana ambao bado hawajapata kazi.

Kukosa kazi ya ndoto yako siyo mwisho wa maisha. Mbali na kujiajiri bado una fursa nyingi zinazokuzunguka ambazo ukizitumia zinaweza kupunguza ukali wa maisha yako na kukuingizia kipato.

Wakati huu ndiyo unaoshauriwa kujaribu kila kitu halali ili kubaini jambo moja ambalo hapo baadaye litakuja kuwa nguzo muhimu ya kuendesha maisha yako binafsi na familia yako. 

Ni kweli umesoma na ungetamani ungekuwa katika ofisi yenye kiyoyozi ukitekeleza majukumu yanayoendana na fani yako, lakini fahamu kuwa njia siyo rahisi hivyo unahitaji kujiandaa na kuangalia fursa mbalimbali.

Huenda unayofikiria kufanya sasa yasikutoe kimaisha kutokana na uhalisia wa maisha. Bado una nafasi ya kufanikiwa ikiwa utajaribu kuzitendea kazi dondoo hizi wakati ukisaka ajira:

Kifanye kipaji kuwa biashara

Kama wewe ni mwanamuziki, mcheza mpira, muigizaji, mchoraji au hata mpiga vyombo vya muziki na mengineyo, unaweza kutumia kipaji chako kujiajiri na kujiongezea kipato.

Charles Burton ni mchoraji wa picha ambaye huenda umewahi kumuona katika majengo ya Mlimani City jijini Dar es Salaam kama ni eneo lako la kutembelea.

Burton ameiambia www.nukta.co.tz kuwa, hakutaka kuendelea kutafuta kazi lakini anatumia kipaji chake kupata kipato cha kukidhi maisha.

Siyo tu anachora picha, bali anatumia kipaji cha kuimba alichonacho kuimba katika korido za maduka ya Aura Mall kati ya jiji la Dar es Salaam nyakati za jioni ili kuwaburudisha watu wanaoingia na kutoka. 

“Siyo rahisi kuamini lakini kupitia kazi ninazozifanya bila malipo nikiwa nachora Mlimani City au nikiwa ninaimba Aura Mall nimepata kazi ambazo zimenikwamua kwa namna tofauti tofauti,” amesema Burton.

Ukitumia kipaji chako kinaweza kukupa ajira itakayoboresha maisha yako. Picha|Mtandao.

Tumia mitandao yako ya kijamii

Hapa ndipo udalali unapoanza. Hauna haja ya kuwa na idadi kubwa ya watu kwenye kitabu chako cha mawasiliano (Phone book) na usiwatumie kama mtaji. Ndiyo, watu wanaposema “binadamu ni mtaji” hapa ndipo maana yake inaanza.

Mjasiriamali wa mavazi wa jijini Dar es Salaam, Sia Lazaro ni kati ya wasakatonge waliotuma maombi ya kazi kwa muda mrefu bila mafanikio. Changamoto ya kukosa kazi imemuibuliwa fursa nyingine ya kuingiza kipato. 

Tofauti ya Sia na wasakatonge wengine, ameamua kuwatumia marafiki zake kama mtaji kwa kuwaondolea kero ya kwenda Kariakoo kufanya manunuzi ya nguo na viatu badala yake anawafanya kwa niaba yao.

Sia hutembea kwenye maduka mbalimbali ya nguo, viatu na vipodozi na kupiga picha bidhaa hizo na kuziweka kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii. Huko watu humpatia tabasamu kwa kuuliza “Shilingi hii” na kukamilisha tabasamu lake kwa kusema “niletee na ninakutumiaje hela?” 

Sia amesema hupata faida ya Sh20,000 akiuza bidhaa hizo mtandaoni lakini siyo kila siku. Hutumia zaidi mtandao wa Instagram ambao hutumiwa zaidi na wanawake.  

Mbali na kile anachokifanya Sia, endapo mtandao wako wa kijamii una wafuasi wengi, anza kuutumia kama ukurasa wa matangazo ya biashara. Itakupatia pesa usiyoitarajia.


Zinazohusiana


Omba kujitolea kwenye makampuni na sehemu mbalimbali

Huenda ikawaacha wengi na mshangao wa ni kwa namna gani hii inakuwa suluhu kwenye shida yako.

Kupitia kujitolea, siyo kazi zote zinaweza kukunufaisha kiuchumi kwa muda huo lakini kwa mujibu wa Gerald Kanza ambaye ni Meneja Rasilimali Watu wa kampuni ya Cas Medics, mtu ambaye amejitolea na kuonyesha uwezo mzuri wa kufanya kazi, endapo kutatokea nafasi inayoweza kumfaa kwenye kampuni hiyo, anaweza kupewa.

“Watu wengi hawaoni umuhimu wa hili lakini kama umejitolea na tukaona uwezo wako ni mkubwa, kama nafasi ikitokea ofisini ni lazima watu watakufikiria,” amesema Kanza.

Kujitolea kufanya kazi kwa muda fulani katika kampuni zinazofanya uliyosomea kunaweza kukuongezea ujuzi zaidi. Picha|Mtandao.

Tazamia kuwa msaidizi binafsi

Japo hii inategemea na uwezo wako wa uvumilivu lakini wapo mabosi wengi wanaotafuta watu wa kuwa wasaidizi binafsi kwa gharama ndogo.

Kulingana na fani uliyosomea, unaweza kutafuta kazi kwa mtu mkubwa ambaye unaweza kumsaidia baadhi ya majukumu ambayo unayaweza.

Mkurugenzi wa kampuni ya J Sisters, Jessica Mshama amesema aliwahi kutingwa na majukumu na mmoja wa wafuasi wake alimtafuta DM (meseji za moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii) na kumuomba kuwa msaidizi wake binafsi.

Alichokifanya Mshama ni kupitia wasifu wa mfuasi huyo mtandaoni na baada ya kuona kuwa anafanya shughuli zinazoendana na zake, alimpatia nafasi hiyo.

“Amekuwa msaada kwangu na ni ajabu kuwa sikuwahi kufikiri kama kuna mtu anaweza kujitoa kufanya kazi hii,” amesema Mshama.