October 8, 2024

Upanuzi wa uwanja wa ndege wa Musoma kuongeza kasi ya utalii kanda ya Ziwa

Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa aliyekuwa akizungumza leo (Februari 4, 2020) bungeni jijini Dodoma, amesema kabla ya kuanza upanuzi wa uwanja huo, watawalipa wananchi fidia ili waondoke katika maeneo yanayozunguka uwanja huo.

  • Upanuzi wa uwanja huo utasaidia kuongeza kasi ya shughuli za utalii.
  • Pia utafungua fursa mbalimbali kibiashara kwa wakazi wa mkaoa huo.
  • Serikali yasema imetenga Sh4.319 bilioni za fidia kwa wananchi wanaokapisha upanuzi wa uwanja huo. 

Dodoma. Serikali imesema inakusudia kuufanyia maboresho na kuupanua uwanja wa ndege wa Musoma mkoani Mara ili kuchochea shughuli za utalii katika mikoa ya kanda ya Ziwa Victoria na kuiongezea Serikali mapato.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa aliyekuwa akizungumza leo (Februari 4, 2020) bungeni jijini Dodoma, amesema kabla ya kuanza upanuzi wa uwanja huo, watawalipa wananchi fidia ili waondoke katika maeneo yanayozunguka uwanja huo. 

“Lazima kwanza wananchi tuwalipe ndipo tuweze kupeleka huduma hii,” amesema Kwandikwa.

“Wananchi 135 watalipwa fidia kwa sababu tumeshawatambua baada ya kufanya mapitio. Niwahakikishie wananchi wa kata ya Nyasho, wananchi 97 watalipwa, wananchi wa kata ya Kamunyonge, wananchi 38 watalipwa,” amesema Kwandikwa.

Naibu Waziri huyo alikuwa akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu, Joyce Sokombi aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuboresha uwanja huo ambao unaweza kutumika kuvutia watalii wanaotembelea vivutio vilivyomo mkoani humo. 

“Ndiyo maana Serikali imefanya juhudi kubwa kuhakikisha uwanja huu tunaupanua, tunauweka ukae vizuri ili huduma iwe kubwa zaidi katika eneo hilo,” amesema Kwandikwa.

Amesema Serikali imetenga kiasi cha Sh4.319 bilioni kulipa fidia kwaa wananchi watakaoathirika na upanuzi wa uwanja huo ambao kwa asilimia 95 utatumika kwa shughuli za kitalii.

Mbali na hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mkoa wa Mara unaibeba hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Julius Nyerere na Rumanyika. ambazo zimeanzishwa.


Zinazohusiana


Hifadhi ya Serengeti ambayo ina ukubwa wa kilometa za mraba 30000, kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018, watalii 899,677 wameitembelea hifadhi hiyo tangu mwaka 2014 hadi mwaka juzi. 

Idadi hiyo ni sawa na asilimia 17.5 ya watalii milioni 5.12 walioingia nchini tangu mwaka huo.

Uwanja huo, utawarahisishia watalii wanaolazimika kutumia viwanja vya ndege vya Mwanza, Kagera na Arusha kwa ajili ya kwenda katika maeneo ya vivutio. 

Pia utasaidia kuinua uchumi wa mkoa huo ambao unategemea shughuli za kilimo na uvuvi katika Ziwa Victoria.