November 24, 2024

Mkopo wa Benki ya Dunia waibua utata ujenzi maabara za sekondari Tanzania

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Mwita Waitara amesema hatua ya Benki ya Dunia (WB) kusitisha kwa muda kutoa mkopo wa masharti nafuu wa Dola 500 milioni za Kimarekani kwa Tanzania, kumeathiri mpango wa Serikali wa kumaliza tatizo la upungufu wa maabara

  • Serikali yasema sehemu ya fedha hizo ambazo zimezuiliwa kwa muda zingemaliza tatizo la maabara katika shule za sekondari nchini. 
  • Spika Job Ndugai awa mkali kwa Wabunge wanaowashawishi kuzuiwa fedha za wahisani.
  • Naibu Waziri Tamisemi asema watatumia fedha za mfuko wa Serikali Kuu na za Halmashauri kujenga maabara hizo.

Dar es Salaam. Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Mwita Waitara amesema hatua ya Benki ya Dunia (WB) kusitisha kwa muda kutoa mkopo wa masharti nafuu wa Dola 500 milioni za Kimarekani kwa Tanzania, kumeathiri mpango wa Serikali wa kumaliza tatizo la upungufu wa maabara katika shule za sekondari nchini. 

Fedha za mkopo huo ambazo ni zaidi ya Sh1.2 trilioni zingeelekezwa katika kushughulikia programu za elimu nchini zikiwemo kujenga miundombinu ya madarasa na ununuzi wa vifaa vya kufundishia.

Waitara ameliambia Bunge leo (Februari 3, 2020) jijini Dodoma kuwa sehemu ya fedha hizo  zingetumika katika uboreshaji wa miundombinu ya vyumba na ununuzi wa vifaa vya maabara na kupunguza tatizo hilo nchini.  

“Tunakamilisha maabara zaidi ya 400 katika mpango ule, huenda hizo fedha (mkopo wa benki ya dunia) zingekuja kwa wakati na ilikuwa mpango wa Serikali. Hii kazi ya kulalamikia maabara hata kama isingeisha ingepungua sana,” amesema Waitara.

Naibu Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Ukonga amesema Serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa maendeleo imekamilisha ujenzi wa maabara 5,801 kati ya maabara 11,369 zinazohitajika hivyo upungufu uliopo ni maabara 5,568.

“Pia sisi kama wizara tunakwazwa sana na mambo haya kwa sababu tunaweka mipango, Wabunge wameleta maombi mbalimbali wizarani, fedha zimeiva halafu kuna watu wanaweka kitumbua mchanga,” amesema Waitara akionyesha kusikitishwa na Benki ya Dunia kusitisha mkopo huo.


Zinazohusiana: 


Waitara alikuwa akijibu swali la Mbunge wa kondoa Mjini, Edwin Sanda ambaye alitaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kukamilisha ujenzi wa maabara katika shule za sekondari nchini na lini vifaa vitapelekwa katika maabara zilizokamilika.  

“Hebu Serikali ione ni namna gani tunakuja na mkakati wa dharura kama ambavyo tumefanya kwenye maboma, madarasa, kama ambavyo tumefanya kwenye nyumba za walimu ili tuweze kukamilisha maabara nchi nzima,” amesema Sanda katika swali lake la nyongeza kwa Tamisemi.

Hata wakati Spika Job Ndugai akimruhusu Naibu Waziri kujibu swali hilo amesema, “wakati Serikali ikihangaika kupata fedha kwa ajili ya elimu, baadhi ya Wabunge wanaandika barua huko kwa kutumia nembo za Bunge kuzuia fedha zisije. Ndiyo maana tukiwa wakali muwe mnatuelewa tu, nia ni njema tazama matatizo yalivyo makubwa.”

Hata hivyo, Waitara amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na wananchi, itaendelea kuboresha maabara za masomo ya sayansi ili masomo yafundishwe kwa vitendo na siyo nadharia kwa kutumia mfuko wa Serikali Kuu na mapato ya halmashauri.

Imeelezwa kuwa kusitishwa kwa mkopo wa Benki ya Dunia ni shinikizo kutoka kwa wanaharakati wa Tanzania na wa kimataifa waliokuwa wakiitaka benki hiyo isitoe mkopo huo kwa Serikali kutokana na kile walichodai kuwa ni kuwepo kwa sera na sheria ya elimu ya kibaguzi kwa wanafunzi wa kike waliopata ujauzito wakiwa shuleni. 

Hatma ya wa mkopo huo imekuwa ukikabiliwa na vikwazo tangu mwaka 2018 ambapo uongozi wa Benki ya Dunia ulikataa kupitisha mkopo huo ambao awali ulikuwa dola milioni 300.