October 6, 2024

Sababu za Rais Magufuli kumteua Dk Abbas kuwa bosi wizara ya habari

Rais Magufuli amesema Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbas amefanya kazi nzuri sana kuisemea Serikali na ataendelea kuwa msemaji mkuu wa Serikali kwa muda licha ya cheo chake kupanda zaidi.

  • Amesema Dk Abbas hakuchoka kuisemea Serikali na alistahili kupandishwa cheo.

Dar es Salaam. Rais Magufuli amesema Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbas amefanya kazi nzuri sana kuisemea Serikali na ataendelea kuwa msemaji mkuu wa Serikali kwa muda licha ya cheo chake kupanda zaidi.

Dk Magufuli ameeleza leo Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua Januari 31, kuwa kwa kazi aliyoifanya Dk Abbas alistahili kupandishwa cheo.

Kabla ya cheo hicho kipya, Dk Abbas alikuwa ni Mkurugenzi Mkuu na Msemaji mkuu wa Serikali tangu alipoteuliwa na Rais Magufuli Agosti 11, 2017 kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016.


Soma zaidi: 


Dk Abbas amedumu katika wadhifa huo kwa muda sasa tangu alipoteuliwa na aliyekuwa Waziri wa habari wa wakati huo Nape Nnauye Agosti 9 mwaka 2016.

“Hakuchoka. Aliisemea vizuri sana Serikali. Alifuata vizuri miongozo ya Dk (Harrison) Mwakyembe na viongozi wengine katika wizara hiyo. Tungependa aendelee tu kuwa msemaji wa Serikali. Lakini mahali mtu anapohitaji promotion (kupandishwa cheo), usimnyime kwa sababu ni motivating agent (motishaa) ndiyo maana tumemteua awe Katibu Mkuu wa wizara,” amesema Dk Magufuli.

 “Kwa sasa ataendelea kuwa msemaji wa Serikali mpaka tutakapopata mwingine na sasa atakuwa anasema akiwa mkubwa zaidi.”

Licha ya kuwa msemaji wa Serikali, Dk Abbas amekuwa kinara wa kuchochea mageuzi ya kidijitali katika mawasiliano serikalini ambapo kwa sasa taasisi nyingi za umeme zimejikita kutoa habari kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.