Mafunzo ya aina yake kwa asasi za kiraia yaja Tanzania
Ni mafunzo maalum yaliyoandaliwa na kampuni ya Nukta Africa kuziwezesha asasi za kiraia kutumia zana na njia za kidijitali kukabiliana na habari za uzushi.
- Ni mafunzo maalum kuziwezesha asasi za kiraia kutumia zana na njia za kidijitali kukabiliana na habari za uzushi.
- Yatasaidia wafanyakazi wa asasi hizo kufanya maamuzi sahihi kutokana na habari wanazopata.
- Yatafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Machi 23 hadi 27, 2020.
Dar es Salaam. Kama kujifunza na kupata maarifa mapya kwa ajili ya kuboresha utendaji wako wa kazi ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli za kijamii, basi mlango umefunguliwa mbele yako kufaidika na mafunzo yatakayobadilisha fikra zako mwaka 2020.
Kampuni ya teknolojia na habari ya Nukta Africa imeandaa mafunzo maalum kuhusu uthibitishaji habari (Fact Checking) kwa wafanyakazi wa asasi za kiraia yatakayowawezesha kutumia zana za kidijitali kukabiliana na habari za uzushi katika shughuli zao.
Mafunzo hayo ya siku tano, yatakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Machi 23 hadi 27, 2020, yanawahusu zaidi wasimamizi na waendeshaji wa mitandao ya kijamii (social media managers), wasimamizi wa uchaguzi, watafiti na maafisa usimamizi na ufuatiliaji katika mashirika hayo.
Washiriki katika mafunzo hayo watapata nafasi ya kujifunza kwa vitendo zana za kidijitali na njia za kuthibitisha habari zikiwemo picha, video na tovuti za habari ili kuwa katika nafasi nzuri ya kukwepa kuangukia katika mtego wa habari za upotoshaji na uzushi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Baada ya mafunzo hayo maalum ambayo yatakuwa kwa vitendo zaidi, kila mshiriki atapata cheti, nyaraka za mafunzo na usimamizi na mwongozo wa wataalam waliobobea kwa muda wa siku 30.
Soma zaidi:
- Nukta Africa yateuliwa katika mpango wa Google
- Internews, Nukta Africa wafungua fursa ya mafunzo kwa wanahabari Tanzania
- Fursa nyingine ya mafunzo ya nishati jadidifu kwa wanahabari Tanzania
Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen amesema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la kasi la habari za uzushi ulimwenguni ikiwemo Tanzania ambazo baadhi zinaathiri utendaji na taswira za watu na mashirika.
Kwa kuwa teknolojia ya habari inakua kwa kasi, kuna uwezekano mkubwa wa habari hizo kuongezeka siku zijazo na kuathiri zaidi taswira na shughuli za asasi za kiraia.
“Hivyo, tunaamini kuanza kwa mafunzo haya nchini hasa kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, kutasaidia maofisa wengi wa asasi za kiraia kukusanya taarifa sahihi na kuepuka habari za uzushi zinazoweza kuharibu taswira za mashirika yao na wakati mwingine kuwafanya wachukue maamuzi yasiyo sahihi,” amesema Dausen.
Amebainisha kuwa japo nafasi za mafunzo hayo ni chache, anawasihi maofisa na hata wengine ambao hujihusisha na asasi hizo za kiraia wajitokeze kwa wingi kupata mafunzo hayo ya kwanza ya aina yake Tanzania.
Mafunzo hayo yatafanyika kuanzia Saa 10 hadi saa moja jioni ili kutoa fursa kwa maofisa hao kutekeleza baadhi ya majukumu yao ya kiofisi.
Ili uwe miongoni mwa washiriki watakaofaidika na fursa hiyo azimu kwa mwaka 2020, utachangia kiasi cha Sh250,000 ikiwa ni gharama ya ada na baadhi ya vifaa vya kujifunzia.
Naye Mkuu wa Uendelezaji Biashara na Mafunzo wa Nukta Africa, Daniel Mwingira amesema watu watakaofanikiwa kushiriki mafunzo hayo watakuwa na uwezo kutambua kikamilifu habari za uongo na kujiweka katika nafasi ya kuwa salama zaidi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa miaka takriban miwili Nukta Africa imekuwa ikishirikiana na wadau wengine kama Internews, Hivos na Code for Africa kutoa mafunzo ya aina hiyo kwa wanahabari na wahariri nchini.
Ili kupata fomu na maelezo ya jinsi kushiriki mafunzo hayo ingia katika tovuti za www.nuktaafrica.co.tz, au tumia kiunganishi hiki >>> https://bit.ly/38ZoWje.