November 24, 2024

Jifunze kuwa mkweli kwa afya yako 2020

Ukweli ni huo ni kuhakikisha unazingatia kanuni za afya ikiwemo kuchunguza afya na kutafuta bima ya afya

  • Ukweli ni huo ni kuhakikisha unazingatia kanuni za afya ikiwemo kuchunguza afya na kutafuta bima ya afya.
  • Epuka kutumia dawa kabla hujapata maelekezo ya daktari
  • Ifanye 2020 kuwa ya afya bora ili utumize kikamilifu majukumu yako.

Nikiwa katika mizunguko  yangu ndani ya wodi maarufu kwa madaktari kama “ward rounds” nakutana na mgonjwa akiwa amelala kitandani amechoka, ananishika mkono na kuniangalia kwa macho yaliyolegea. Midomo yake ikipepesuka kwa ugumu wa maneno ya kutamkika. 

Anajaribu kuongea, anajikaza kwa sauti ya ukakasi yenye udhaifu tena kavu isiyoelezeka na kusema “Dokta nimechoka, laiti ningejua na kuzingatia, natamani nipumzike.” 

Natakiwa kumfanyia mazoezi mgonjwa huyu lakini moyo wangu unayeyuka. Nahisi baridi kali kifuani mwangu, lakini najikaza na kumsogelea kwa tabasamu lililojaa maumivu ya ndani nyuma yake likificha uchungu ninaosikia moyoni mwangu na kumueleza “utaimarika rafiki yangu, piga moyo konde.”

Hapa ndipo ninatambua umuhimu wa kuzingatia kanuni za kuwa na afya bora na natamani kila mtu aelewe hivyo lakini bado ni changamoto kwa watu wengi. 

Afya bora haina mbadala. Wengi wetu tumewekeza nguvu zetu kufanya mambo mengi na kusahau afya zetu zinahitajika kukamilisha mipango yetu ya maisha tunayoipanga kila siku.

Tumejiwekea fikra na dhana kuwa ni masuala ya Wazungu au watu wa Magharibi na kutokujiwekea utaratibu wa kupima afya mara kwa mara. 

Tunasahau ya kuwa miili yetu inachakaa na inaweza kuzidiwa kinga. Daktari mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Dk Christopher Peterson aliwahi kusema katika moja ya makala yake kuwa “kinga ya mwili ni rafiki mzuri ambaye anaweza kukusaliti pia.”  


Zinazohusiana:


Katika chaguzi zako na mipango yako mwaka huu weka uchaguzi wa kua na afya njema. Na haya ni baadhi ya maeneo utayopaswa kuzingatia ukifanya chaguzi za kuwa na afya:

Chunguza afya yako walau mara mbili kwa mwaka

Kuwa na utaratibu wa kufanya uchunguzi wa kiafya walau mara mbili kwa mwaka yaani kila baada ya miezi sita. Kama una nafasi walau mara tatu kwa mwaka hata kama hauhisi kuumwa kabisa. 

Kuna baadhi ya magonjwa ikiwemo saratani hayaoneshi dalili za awali hivyo hugundulika  katika hatua ambazo matibabu yake ni magumu na uwezekano wa kupona ni mdogo. 

Ongea na daktari wako kuhusu mpango sahihi wa kufanya uchunguzi (chek up). Pia kama una familia ni vyema kuwajengea utaratibu huu hasa watoto na ndugu zako.

Dhamana ya afya yako iko mikononi mwako. Picha| Hush Naidoo/Unsplash

Hakikisha una bima ya afya

Asilimia kubwa ya Watanzania hawana bima ya afya. Yamkini hata wewe unayesoma ujumbe huu huna bima kwa sasa. Ukweli mchungu ni kwamba gharama za matibabu huwa kubwa maana ugonjwa hauna taarifa. 

Rafiki yangu niliemuelezea awali hakuchoka kwa sababu hakuna tiba ya ugonjwa wake, hasha! Bali ni kwa sababu ametumia pesa nyingi. Kwanza kuutibu ugonjwa ambao yumkini angefanya uchunguzi asingepata shida hiyo. 

Pili, kwa sababu analipia gharama kubwa kwa ajili ya matibabu. Huu ni sawa na msumari wa moto kwenye kidonda kibichi.

Usipuuzie dalili za awali za ugonjwa 

Unapohisi mwili wako hauko katika hali ya usawa pata ushauri wa daktari kwa kwenda hospitali. Watu wengi hubwia madawa ya kuondoa maumivu kisha kuendelea na shughuli hadi pale wanapozidiwa. 

Fungua mfuko wa takataka wa akili yako na ridhia kuitupa hii tabia humo mwaka huu.

Usitumie dawa bila kuandikiwa na daktari

Watu wengi huko mtaani wana tabia ya kutumia dawa za kutuliza maumivu (antibiotic) bila kuandikiwa na daktari. Inafedhehesha mtu anapoenda nunua “Amoxylin” kwa ajili ya mafua. 

Hii itakutengenezea usugu wa dawa na kufanya dawa nyingi zisifanye kazi kwako. Matokeo yake ni machungu.

Hudhuria kampeni za upimaji afya na utoaji chanjo

Hii itakupa kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali. Nakushauri iwapo hujapata chanjo ya homa ya ini, nenda ukapate chanjo hii. Hudhuria matamasha ya kiafya ili ujijengee afya yako kwa ushauri adhimu. Ngoma ya sindimba huchezwa ukiwa na afya bwana wewe!.

Usitumie dawa bila kupata maelekezo ya daktari. Kendal /Unsplash

Zingatia ulaji sahihi wa chakula 

Tumia mlo kamili. Chagua kula kwa usahihi na mpangilio mzuri. Muone mtaalamu wa lishe, fanya vipimo vya BMI (Body Mass Index) kujua uwiano wa uzito wako, fanya mazoezi ujijenge.

Usikubali 2020 ikupite bila kuzingatia kanuni za kujenga afya bora. Ufanye mwaka huu kuwa mwaka bora kwako. Weka kipaumbele kwa afya yako.

Dk Joshua Lameck Sultan ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba katika Chuo cha Tiba na Sayansi Shirikishi Moshi (KCMC) pamoja na hospitali ya KCMC. Pia ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) ambapo hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza