November 24, 2024

Sakata la wanafunzi waliosimamishwa masomo Udsm latua bungeni

Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema Serikali itawachukulia hatua za kisheria wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) waliosimamishwa masomo kwa madai ya kutishia kuandamana kama changamoto zao za mikopo zisinges

  • Serikali imesema itawachukulia hatua za kisheria.
  • Ni viongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) waliotishia kuandamana kudai mikopo. 
  • Yasema changamoto nyingi za mikopo zinatokea zaidi vyuoni.

Dar es Salaam. Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema Serikali itawachukulia hatua za kisheria wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) waliosimamishwa masomo kwa madai ya kutishia kuandamana kama changamoto zao za mikopo zisingeshughulikiwa kwa wakati. 

Desemba 15, 2019 baadhi ya viongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) walitoa saa 72 kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Heslb) kutekeleza maagizo manne likiwamo kuwaingizia fedha wanafunzi ambao hawakupewa tangu chuo hicho kifunguliwe. 

Katika taarifa yao, Daruso ilieleza kuwa endapo maagizo hayo hayatatekelezwa katika muda uliotolewa wanafunzi wangekusanyika nje za ofisi za Heslb, zilizopo Mwenge jijini Dar es Salaam kupigania hatma yao. 

Ole Nasha amesema kitendo hicho ni utovu wa nidhamu na Serikali inafuatilia suala hilo na itachukua hatua stahiki kuhakikisha nidhamu inalindwa katika taasisi za elimu ya juu. 

“Hatutakaa tukubali wanafunzi ambao sisi tunawapa mikopo kama Serikali, kutishia Serikali kwamba msipotoa fedha masaa 72 tutaandamana. Tunaendelea kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria zilizopo,” amesema Naibu Waziri huyo leo (Januari 31, 2020) bungeni jijini Dodoma.

Ole Nasha alikuwa akijibu swali la Mbunge wa viti maalum, Susan Lyimo aliyetaka kujua namna tatizo la mikopo kwa wanafunzi linavyoweza kutatuliwa ili wanafunzi wapate mikopo kwa wakati.

Naibu waziri amesema ucheleweshaji wa mikopo kwa wanafunzi unasababishwa na changamoto ya michakato ya ndani ya vyuo katika kukamilisha taarifa zao.

“Mikopo siku hizi inatolewa na Serikali angalau miezi miwili kabla ya vyuo kufunguliwa. Kinachotokea na kusababisha kuchelewa, ni changamoto ya michakato ya ndani ya vyuo,” ameongeza Ole Nasha.


Zinazohusaina:


Hata hivyo, uongozi wa Udsm tayari uliwasimamisha masomo kwa muda usiojulikana viongozi hao akiwemo Rais wa  DARUSO ndugu Hamis Musa Hamis,  Mwenyekiti wa Bunge, Kasim Ititi, Waziri wa Mikopo, Joseph Malechela na Mwenyekiti Mhimili wa Mahakama, Silas Mtani, 

Wengine Milanga Husein-Mwenyekiti wa Shule Kuu ya Sayansi Asilia na Shirikishi (CONAS) na Naibu Spika wa Bunge,Hamis Thoba. 

Katika madai mengine yaliyotolewa na Daruso wakati huo ni wanafunzi wengi wa mwaka wa kwanza kukosa mikopo tangu chuo kifunguliwe huku baadhi ya wanafunzi wanaoendelea wakikatwa fedha zao. 

Daruso pia iliitaka Heslb kurejesha makato ya fedha za vitabu, mafunzo kwa vitendo na utafiti.