October 8, 2024

Sababu za kwanini waajiri hawakujibu ukikosa kazi uliyoomba

Zipo sababu mbalimbali ambazo zinawasukuma waajiri wengi kutokutoa mrejesho kwa kila mwombaji wa kazi ambaye hajafanikiwa kuitwa kazini ikiwemo kuwapunguzia waombaji msongo wa mawazo.

  • Sababu kubwa ni kukwepa gharama za kuwajibu watu kwani maombi huwa mengi.
  • Pamoja na hayo, waajiri hufanya hivyo kuwapunguzia waombaji msongo wa mawazo.
  • Baadhi wa wadau washauri walau kutoa mrejesho kwa wale ambao wana makosa madogo ili wajirekebishe wanapoomba sehemu zingine.

Dar es Salaam. Hapana! Siyo kwamba una bahati mbaya ya unasahaulika mara zote unaposhindwa kupata majibu baada ya kutuma maombi ya kazi kama hujafanikiwa kuchaguliwa katika kazi husika.

Huenda hali hiyo imekuacha na maswali mengi yasiyokuwa na majibu na wakati mwingine umefikia hatua ya kuona ni jambo la kawaida kutokupewa sababu za kutochaguliwa katika kazi husika uliyoomba kutoka waajiri.  

Zipo sababu mbalimbali ambazo zinawasukuma waajiri wengi kutokutoa mrejesho kwa kila mwombaji wa kazi ambaye hajafanikiwa kuitwa katika interview ili kuwasaidia kujirekebisha katika maeneo waliyofanya makosa. 

Nukta (www.nukta.co.tz) imefanikiwa kuzungumza na wadau mbalimbali wa ajira nchini ambao wameeleza sababu zinazosababisha waajiri wasitoe mrejesho, licha ya kutoa majina ya waombaji waliofanikiwa kuingia katika mahojiano au kupata kazi. 

Kupunguza gharama

Katika maombi mengi ya kazi yanayotumwa kwa waajiri, siyo mtu mmoja au  wawili  wanatuma maombi hayo. Kwa mujibu wa waajiri  walioongea na Nukta, tangazo moja la ajira huvutia vijana wengi kutuma bahasha au barua pepe za maombi na wakati mwingine waajiri huelemewa na maombi mengi.

Baada ya kufanya uchambuzi wa maombi, waliofanikiwa kupenya kuingia katika mchujo wa pili (interview) ndiyo hujulishwa lakini wengine hawapati taarifa yoyote, kwa sababu ni gharama kumjibu kila mtu. 

Hata hivyo, ziko baada ya kampuni ambazo zinatumia mifumo ya kidijitali kuwajibu wale ambao hawajafanikiwa kupata kazi husika lakini hawawapi sababu kila mmoja zaidi ya kuwaambia maombi yalikuwa mengi na nafasi zilikuwa chache. 

Waajiri waliohojiwa na Nukta wamesema ni vigumu kumjibu kila mwombaji wa kazi aliyetuma maombi ya kazi kwa sababu ni gharama kubwa. Picha| Helloquence/Unsplash.

Kuokoa muda

Fikiria, ni muda gani anaohitaji mtu kujibu maelfu ya watu waliotuma maombi ya kazi moja au hata mbili? Ni takribani siku nzima na zaidi.

Mwanzilishi wa App ya Toolboksi, Julius Mbungo anasema kwa kampuni ambazo hazina wafanyakazi wengi au zenye mzunguko mkubwa wa majukumu, ni vigumu kupoteza muda kwa shughuli zisizo na manufaa.

“Kwa muda ambao utakaa kujibu kila mtu alietuma maombi, unafikiri ungeweza kuomba tenda ngapi au kuhudumia wateja wangapi?,” amehoji Mbungo.


Zinazohusiana


Huchukuliwa kama jambo la kawaida

Afisa Utawala wa kampuni ya Seedspace Dar es Salaam, Lilian Mgeni amesema waajiri wengi wameshazoea kuwa endapo mtu hatojibiwa, ni dhahiri kuwa atajiongeza kuwa hajapata kazi hiyo.

“Imeshazoeleka hivyo lakini mimi kwa upande wangu nashauri waajiri kama wanaweza, wawapatie walau feedback “mrejesho” wa makosa waliyofanya ili wajirekebishe,” amesema Mgeni.

Kuwapunguzia waombaji msongo wa mawazo

Lilian ameenda mbali zaidi na kusema, “huwezi kujua huyo mtu ametuma maombi mangapi na siku hiyo amepokea majibu mangapi ya kukatisha tamaa” hivyo muda mwingine ni bora umpunguzie mateso kwa kumwacha ajijibu mwenyewe.

“Wewe upokee email (barua pepe) tano kwa siku zote zina sema umekosa kazi, haujafanikiwa kupata kazi hii au pole jaribu tena unafikiri utakuwa kwenye hali gani? Muda mwingine “it is for the best” (ni kwa heri),” amesema Mgeni.

Wapo vijana ambao hupokeataarifa zakuvunja moyokila kukicha. waajiri hufanya hivyo kuwaondolea adha hiyo. Picha| Young men’s health.

“Inachosha kujibu”

Meneja wa kampuni ya kusaga unga na vyakula vya mifugo, Lina Mills, Christian Kulwa, amesema“baaadhi ya waombaji wanakera hata kujibu.”

Kulwa amesema ni heri basi maombi yao yangekuwa yanavutia kiasi cha kukufurahisha hata uwajibu lakini unawezaje kumjibu mtu ambaye hayuko makini kiasi cha kutuma barua pepe isiyo na ujumbe wowote?

Kulwa amesema wapo ambao wanatuma barua pepe haina hata utambulisho au kichwa cha barua hiyo “Subject”

“Unafungua email vuum! (barua pepe) Unaona CV (wasifu) sasa hata salamu kweli hamna? Unakuta umetangaza kazi zenye taaluma tofauti tofauti nazo mtu haandiki ata anaomba kazi gani sasa mimi ndiyo nianze kusoma Cv yake nijue huyu ni wa kazi hii na huyu ni wa kazi ile? Siwezi,” amesema Kulwa.

Sababu hizi zisikukatisha tamaa ya kuendelea kupambana kuifikia hatma ya maisha yako. Muhimu, ongeza umakini wakati wa kutuma maombi. Hakikisha taarifa unazotuma ziko sahihi na zinakidhi vigezo vyote anavyovitaka mwajiri.

Katika makala ya kesho tutaangazia, ni mambo gani ambayo vijana walioajiriwa wanatakiwa kuzingatia ili kuwawezesha kudumu katika kazi muda mrefu hata kuwawezesha kukua kitaaluma.