October 6, 2024

Watanzania wanaosoma China watahadharishwa mlipuko virusi vya Corona

Kufuatia mlipuko wa ugonjwa Corona nchini China, Serikali imewataka wazazi na walezi wenye watoto wanaosoma nchini humo ambao wapo Tanzania kwa likizo wasiwaruhusu kwenda hadi hapo Serikali itakapotangaza.

  • Wazazi na walezi wenye watoto wanaosoma nchini humo ambao wapo Tanzania kwa likizo wasiwaruhusu kwenda hadi hapo Serikali itakapotangaza.
  •  Idadi ya vifo kutokana na virusi vya Corona imefikia watu 170.

Dar es Salaam. Kufuatia mlipuko wa ugonjwa Corona nchini China, Serikali imewataka wazazi na walezi wenye watoto wanaosoma nchini humo ambao wapo Tanzania kwa likizo wasiwaruhusu kwenda hadi hapo Serikali itakapotangaza.

Vyombo vya habari vya China vimeripoti leo kuwa idadi ya vifo kutokana na virusi vya Corona imefikia watu 170 huku virusi hivyo sasa vikidaiwa kusambaa katika kila mkoa nchini humo. 

Kati ya waliofariki, 162 wanatoka mkoa wa Hubei ambao ndio kiini cha mlipuko huo. 

“Tunawasihi watoto wasirudi hadi hapo tutakapopata taarifa za kidiplomasia kuhusiana na maendeleo ya ugonjwa huo,” amesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo (Januari 30, 2020) wakati akijibu swali la Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma. 

Mbunge huyo alitaka kujua namna Serikali ilivyojipanga kukabiliana na homa hiyo pamoja na baa la nzige.

Majaliwa amesema ni kweli China kuna mlipuko wa virusi hivyo ambapo watu wengi wamepoteza maisha na tayari baadhi ya nchi jirani nazo wananchi wake wameanza kupata maambukizi.

 “Watoto wasirudi hali ikikaa vizuri warudi China kuendelea na masomo na ikiwa vinginevyo Serikali itatafuta utaratibu mwingine,” amesisitiza. 

Januari 29, 2020, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alitoa taarifa kwa umma kuhusu ugonjwa huo na aliwahakikishia Watanzania kuwa homa hiyo haijaingia nchini.


Soma zaidi: 


Waziri Mkuu amesema, “katika kukabiliana na homa hiyo, Serikali imejipanga kwa kuimarisha mawasiliano na ubalozi wetu huko China ili kujua hali inaendeleaje, na Balozi wa Tanzania nchini China, Balozi Mbelwa Kairuki anafanya kazi hiyo ya kutoa mrejesho wa kila siku wa hali ilivyo huko.”

Amesema licha ya kutuma mrejesho, pia Balozi huyo anafanya kazi nzuri ya kutoa elimu kwa Watanzania kwa kutafuta madaktari wa Kitanzania ambao wamejifunza ugonjwa huo na kuwaelimisha Watanzania waliopo nchini China namna ya kujikinga na homa hiyo.

Akizungumzia baa la nzige lililoikumba nchi jirani ya Kenya, Waziri Mkuu amesema kuwa tayari Serikali imeshachukua tahadhari ambapo Wizara ya Kilimo inashirikiana na ya Kenya kumaliza tatizo hilo. 

Pia amewataka wananchi wanaoishi kwenye mikoa, wilaya na vijiji vilivyo mipakani, watoe taarifa mara watakapowaona wadudu hao.