November 24, 2024

Jinsi unavyoweza kutumia namba za utambulisho kuokoa simu iliyopotea

Husaidia katika kubaini simu iliyopotea na mahali ilipo ikiwa namba hizo zitatumika kikamilifu.

Umuhimu wa kufahamu tarakimu za IMEI  ni mkubwa kwani unampa mhusika uwezo wa kutambua kifaa chake kwa njia ya kielektroniki. Picha | Mtandao.


  • Zinatambulisha kifaa husika kwa mtumiaji pindi anapokuwa mbali na kifaa hicho.
  • IMEI ni kiunganishi kati ya mitandao ya simu na mteja.

Dar es Salaam. Uwezo wa kutambua tarakimu za IMEI kwenye simu yako ni moja ya vitu muhimu kama mmiliki wa kifaa  untakiwa kufahamu ili kukusaidia  katika utambuzi  pale anapotaka kujua kifaa hicho kilipo.

IMEI kwa kirefu chake ni “International Mobile Equipment Identity”. Ni namba ambazo zinakuwa kama utambulisho wa kifaa na katika simu, mara nyingi zinakuwa tarakimu15. Namba hizi huwa hazifanani na zinakuwa katika kifaa kimoja tu.

Umuhimu wa kufahamu tarakimu za IMEI  ni mkubwa kwani unampa mhusika uwezo wa kutambua kifaa chake kwa njia ya kielektroniki hata asipokuwa na kifaa hicho kwa muda muafaka.

Ili  mmiliki wa kifaa hicho aweze kupata tarakimu hizo kwenye simu; Anapaswa kwenda kwenye Mpangilio wa simu (Settings) kisha Kuhusu simu (About phone) ndipo ataona tarakimu za IMEI au kwa kupiga (*#06#) na kupata tarakimu anazoweza kunukuu na kutunza kwa manufaa yake ya  baadae.

Tarakimu hizo pia  husaidia  kuzuia  matukio ya wizi  kwani kwa kutumia namba hizo, mara baada ya kuibiwa simu mhusika anaweza kuripoti polisi na kupata msaada wote wa namna ya kupata tarakimu hizo au kunasa mahali simu ilipo kwa wakati fulani.

Endapo itatokea simu imepotea na mhusika kukosa tarakimu hizo, hatua za awali ni kwenda kwenye kituo chochote cha polisi kwaajili ya kupata maombi yanayoenda kwenye kampuni husika kwaajili ya kupata namba hizo na kunasa mahala simu ilipo.


Zinazohusiana:


Mtaalamu wa masuala ya teknolojia kutoka mtandao wa simu wa Halotel, ameiambia www.nukta.co.tz kuwa kupata huduma ya kunasa simu pale itakapoibiwa ni haki ya kila mtanzania kinachohitajika ni kufuata taratibu zote za mchakato huo.

Amesisitiza kuwa  umuhimu wa namba hizo ni mkubwa kwani ni  kiunganishi kati ya mitandao ya simu na mteja.

“Moja ya jukumu ulilonalo kama mmiliki wa kifaa kama simu ni kujua IMEI namba. Zinasaidia sana hasa kwenye wizi. Tumeshasaidia wateja wengi kupitia namba hizo.” Amesema mtaalamu huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.