Wiki yaisha kwa neema soko la hisa Dar
Thamani ya mauzo katika soko hilo yamepaa mara 11 ndani ya wiki moja hadi Sh22.64 bilioni wiki iliyoishia Januari 17 kutoka Sh2 bilioni wiki iliyopita.
- Thamani ya mauzo yapaa mara 11 ndani ya wiki moja hadi Sh22.6 bilioni wiki iliyoishia Januari 17 kutoka Sh2 bilioni wiki iliyopita.
- Wachambuzi walieleza awali kuwa sikukuu za mwisho wa mwaka ni moja ya mambo yaliyoathiri wiki mbili za awali za mwaka
Dar es Salaam. Biashara katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imeanza kurudi taratibu katika hali yake baada ya thamani ya mauzo kupaa mara 11 hadi Sh22.64 bilioni katika wiki iliyoishia Januari 17 kutoka Sh2.04 bilioni wiki moja iliyopita.
Hali hiyo inakuja baada ya thamani za mauzo ya wiki mbili zilizopita kuwa chini kidogo kwa kile wataalamu wa masuala ya hisa na dhamana kueleza kuwa yaliathirika na sikukuu za mwisho wa mwaka.
Taarifa ya kampuni ya udalali wa hisa na dhamana Zan Securities imeeleza kuwa kampuni ya bia Tanzania (TBL) ndiyo ilikuwa kichocheo kikubwa cha mafanikio ya soko hilo baada ya kuchangia asilimia 70.65 ya thamani ya mauzo yote kati wiki hiyo iliyoishia Januari 17.
TBL imefuatiwa na CRDB ambayo ilichangia asilimia 29.18 ya mauzo yote ya wiki hiyo.
Biashara katika soko la hisa hufanywa katika siku za kazi pekee yaani Jumatatu hadi Ijumaa.
Zinazohusiana:
- M-pesa, intaneti vyachangia Vodacom Tanzania kupata faida ya Sh90 bilioni
- Wawekezaji wa Acacia soko la hisa Dar tabasamu tupu
- Maumivu kwa wawekezaji wa kampuni ya bia soko la hisa Dar
Mtendaji Mkuu wa Zan Securities, Raphael Masumbuko amesema katika taarifa hiyo kuwa kaunta ya CRDB ilipaa kwa asilimia 5.26 na kufunga kwa Sh100 kwa hisa wakati kaunta ya NICO ilishuka kwa asilimia 2.86 hadi Sh170.
“Mafanikio katika soko la mitaji limesadifu utabiri wetu wa wiki iliyopita ambapo mauzo yaliongezeka na soko la ndani lilifanya vizuri. Haturajii mafanikio hayo kuendelea wiki ijayo lakini tunaamini soko linazidi kuimarika siku zijazo,” amesema Masumbuko katika utabiri wa soko wiki ijayo.
Mtaji wa jumla (total market capitalisation) katika soko hilo, kwa mujibu wa Zan Securities, ulishuka kiduchu kwa asilimia 0.6 hadi Sh17.25 trilioni wakati mtaji wa soko la ndani ukipaa kidogo kwa asilimia 0.14 hadi Sh9.02 trilioni.