Fahamu njia za kuweka akiba kwa malengo ya baadaye
Njia hizo ni pamoja na kutunza pesa nyumbani, benki, kwa njia ya simu za mkoni au kununua hisa.
- Njia hizo ni pamoja na kutunza pesa nyumbani, benki, kwa njia ya simu za mkoni au kununua hisa.
- Akiba ya fedha inasaidia kutekeleza mipango ya muda mfupi na mrefu.
Dar es Salaam. Kufanya kazi ni hitaji la kila binadamu ili kupata kipato kitakachotumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kutatua changamoto za maisha zinazotukabili.
Pamoja na umuhimu wa kufanya kazi na kujipatia kipato, bado tunakumbushwa kujiwekea akiba ya sehemu mapato yetu tunayopata. Akiba ya fedha inasaidia kutekeleza mipango ya muda mfupi na mrefu.
Pia inaweza kuwa mkombozi tunapopata dharula kama ajali, msiba au jambo lolote linalohitaji fedha kwa haraka. Licha ya kuwa kuweka akiba ni jambo muhimu bado limekuwa changamoto kwa watu wengi kulitekeleza kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kujisahau na kuridhika na hali ya pesa waliyona na matumizi makubwa kuliko kipato wanachopata.
Hiyo haiondoi uhalali na umuhimu wa kuweka akiba kwa matumizi ya baadaye. Ni njia zipi unaweza kuzitumia kuweka akiba? Chagua moja kati ya hizi kujiwekea akiba kulingana na mazingira uliyopo:
Hifadhi Pesa taslimu
Pesa taslimu hujumuisha pesa zote za sarafu na noti ambazo zinaonekana au unaweza kuzishika. Hii ni njia ya kuweka akiba ambapo huchukuliwa kama njia ya zamani na iliyopitwa na wakati.
Unaweza kutunza pesa zako nyumbani hasa kwenye kibubu kwa kipindi fulani kabla hujazitumia. Hutumiwa zaidi na watu ambao wako mbali na benki au huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi.
Njia hii ni nzuri na haina gharama kuweka akiba lakini siyo salama hasa kama unatunza kiasi kikubwa cha pesa nyumbani. Unaweza kuvamiwa na kuibiwa fedha zao au hata nyumba inaweza kuungua na ukapoteza akiba uliyodunduliza kwa muda mrefu.
Unaweza kutumia njia hii kama una jambo la haraka ambalo linahitaji fedha, mfano mahitaji ya nyumbani ikiwemo nauli ya shule ya watoto.
- bajeti inavyookoa matumizi mabaya ya pesa ngazi ya familia
- Jinsi ya kudhibiti matumizi mabaya ya pesa zako
- Zingatia haya wakati ukifanya manunuzi msimu wa sikukuu
Fungua akaunti ya benki
Unashauriwa kufungua kaunti ya benki mahususi kwa kujiwekea akiba huku ukiwa na malengo ya kiasi cha fedha unachotaka kutunza kwa kipindi fulani.
Akaunti za benki ziko za aina mbalimbali. Ipo ya kawaida ya kutunza fedha (Saving account) ambayo unaweza kuweka na kutoa kiasi chochote wakati wowote.
Pia unaweza kufungua akaunti ambayo utaweka pesa kwa muda fulani ili ukitoa upate riba (fixed account) au akaunti ya cheki ambayo unapata kitabu cha cheki kufanya miamala mbalimbali ikiwemo kuhamisha pesa kutoka akaunti moja hadi nyingine.
Njia hii ya kuweka pesa benki ni salama na ya uhakika inakuondolea ushawishi wa kutumia pesa ukilinganisha na ya kutunza pesa nyumbani.
Hata hivyo, ili malengo yako yatimie unahitaji kijitia nidhamu ya kuweka pesa kila unapopata au kwa muda uliojiwekea.
Tunza kwa njia ya simu za mkoni
Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, simu za mkononi ni zaidi ya kifaa cha mawasiliano. Kwa wale ambao wanaona ni tabu kuweka pesa benki, njia hii inawafaa zaidi.
Tumia huduma za kuweka na kutoa pesa za mtandao wako wa simu (mobile money) kuweka akiba ili ikufae wakati wa dharula.
Njia hii ni sawa na ile ya kutunza pesa nyumbani lakini zinakaa kwenye simu yako na unaweza kuzitoa wowote na ukazitumia utakavyo. Inahitaji tahadhari na nia ya dhati kuhakikisha kile unachohifadhi hakitoki isipokuwa kama kimetimiza malengo uliyojiwekea.
Nunua hisa
Hii ni njia nyingine ya kuweka akiba pesa zako. Hisa ni akiba unayoiweka na kuituma kuleta fedha nyingine. Kuweka akiba ya pesa zako hukupa utulivu moyoni na pumziko la fikra.
Sheria ya Kampuni ya mwaka 2002 na Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya mwaka 2002 zimeweka utaratibu rahisi kwa mtu yeyote kuwekeza kwenye kununua hisa za kampuni fulani ili kupata faida baadaye.
Faida kadhaa zinaainishwa kwenye biashara hii ambazo ni pamoja na hisa kuwa dhamana. Cheti cha hisa unazomiliki ni dhamana yako katika taasisi za fedha, unaweza kutumia cheti hicho kukopa pesa.
Hata kama huna hati ya nyumba, cheti cha hisa kinakuwezesha kukopa na kufanikisha malengo yako.
Thamani ya hisa zako inaweza kukua hivyo kuongeza thamani ya kiasi ulichowekeza katika kampuni husika. Kumbuka, kila mwaka kampuni hufanya hesabu ya faida iliyopatikana. Endapo kampuni itaridhia kutoa gawio kila mwaka utalipata. Gawio hili utaendelela kulipata maisha yako yote kadri kampuni inavyotengeneza faida.
Changamoto ya aina hii ya kuweka akiba ni kushuka au kutopanda kwa bei ya hisa au kufirisika kwa kampuni uliyowekeza, jambo litakalokufanya upoteze kiasi cha pesa ulichowekeza.
Bado hii ni njia sahihi kwa watu wenye malengo ya muda mrefu.
Katika makala ijayo tutaangazia namna unavyoweza kuwekeza pesa zako katika shughuli mbalimbali ili kujiongezea kipato.