Windows 7 kuzikwa rasmi Januari 14
Wataalamu wanashauri kuhamia katika mifumo endeshi ya Windows 8 na 10 ambayo imeongezewa usalama zaidi ikilinganishwa na Windows 7 ambao umepitwa na wakati.
Windows seven haikuwa na miraba ya programu wala programu ya Cartona. Picha|Digi.
- Ukomo wa mfumo endeshi huo ni leo (Januari 14, 2020).
- Kuendelea kuitumia kunamweka mtumiaji wa kompyuta kwenye shida ya kusumbuliwa na virusi vya kielektroniki.
- Wataalamu wanashauri kuhamia kwenye mfumo endeshi wa Windows 8 na 10.
Dar es Salaam. Kampuni teknolojia ya Microsoft kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari imesema leo Januari 14, 2020 ndiyo ukomo matumizi ya mfumo endeshi wa kompyuta wa Windows 7 na kuwataka wateja wake kugeukia mifumo mengine.
Mfumo huo ulioundwa Julai 2009 unaondoka katika uso wa teknolojia na kuipisha mifumo mingine endeshi ya Windows 8,na Windows 10 ambayo inatumiwa zaidi na watumiaji wa kompyuta.
Kupitia taarifa yake, kampuni hiyo yenye makao makuu nchini Marekani imeainisha kuwa inakusudia kuondoa mikono yake kuendesha mfumo huo leo.
Hata hivyo, kusitishwa kwa Windows 7 hakutazima kompyuta zinazotumia mfumo huo lakini kama mtu ataendelea kutumia ataiweke kompyuta yake katika hatari ya kushambuliwa na virusi vya mtandaoni kwa sababu ya usalama wake utapungua.
“Hautaweza kupokea maboresho yakiwemo ya kiusalama kutoka Microsoft. Tunashauri kila anayetumia mfumo huu ahamie kwenye mfumo endeshi wa Windows 10 kabla ya January 2020 kuepuka kuhitaji msaada wa huduma ambayo haipo,” imesema Idara ya huduma na msaada ya Microsoft.
Zinazohusiana
- Microsoft sasa jino kwa jino na Google katika utoaji wa taarifa
- Microsoft kuwezesha upigaji simu kwa kompyuta
- Microsoft mbioni kuingiza sokoni “Simu ya Android”
Tutakumbuka nini kutoka kwa Windows 7?
Kitu kikubwa ni muonekano rahisi kwani kwa mfumo endeshi wa Windows 7, mambo yalikuwa rahisi kwa mtumiaji kwani baada ya kubonyeza kitufe cha “Start”, mtumiaji angeona programu zote kwa wakati mmoja na kuchagua programu anayoipenda.
Kwa mifumo endeshi inayobaki, yaani Windows 8 na 10, baada ya kubonyeza kitufe cha “Start”, mtumiaji atakaribishwa na ‘Live Tiles’ ambazo ni kama programu lakini zinakua katika mfumo wa mraba ambazo zinakaa mkono wa kulia kwenye “start Menu” (menyu inayoonekana baada ya kubonyeza kitufe cha start).
Hata hivyo, ikumbukwe kuwa maboresho hufanyika mara kwa mara ili kumlinda mtumiaji na shida za kiusalama pamoja na virusi vya kielektroniki, ni vyema kwa mtumiaji wa Windows 7 akaanza kuhamia kwenye mifumo endeshi iliyoshauriwa.
Mbali na usalama, mifumo endeshi hiyo ina sehemu ya kutafuta programu kwa uharaka, jambo ambalo Windows 7 haina.
Kwa Windows 8 na 10, unaweza kuongea na “Cartona” ambayo ni programu unayoweza kufanya nayo majibizano kama ilivyo kwenye simu za iPhone ambapo programu hiyo inajulikana kama “Siri”.
Mdau wa Teknolojia na Mbunifu wa programu za kompyuta, Joshua Mabina amesema kuhamia Windows 10 na 8 ni kama mtu anapohama kutoka kwenye nyumba isiyo na geti na kuhamia kwenye nyumba iliyokuwa na geti.
Mabina amesema ni wazi kuwa Windows 7 haina ulinzi tena na hivyo itakuwa rahisi kuvamiwa na virusi viharibifu kwa ambaye atabaki akitumia programu hiyo bila ulinzi thabiti.
“Kuhamia kwenye programu ambazo zinaelekezwa na wataalamu kunamaanisha kuna ulinzi ulioimarishwa zaidi,” amesema Mabina.