November 24, 2024

Fanya haya kuepuka kusinzia wakati unaendesha gari

Mbali na mwendokasi na ulevi vinavyojulikana kuwa visababishi vikubwa vya ajali za barabarani, kusinzia wakati wa kuendesha gari pia ni moja ya sababu zinazochangia kukatili maisha ya maelfu ya Watanzania wakiwa barabarani.

  • Baadhi ya mbinu hizo ni pamoja na kusikiliza redio, kunywa vinywaji vinavyochangamsha na kuongozana na ndugu au rafiki.
  • Umakini barabarani unasaidia kupunguza uwezekano wa kupata ajali. 

Dar es Salaam, Wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres akisema kuwa mtu mmoja duniani anafariki kila sekunde 24 kutokana na ajali za barabarani, Tanzania pekee imepoteza watu takriban 19,510 ndani ya miaka saba iliyopita. 

Ripoti ya takwimu muhimu za mwaka 2018 (Tanzania in figures 2018) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inaeleza kuwa vifo hivyo vilitokea katika ya mwaka 2013 na 2018.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka 2018 pekee watu 1,912 waliaga dunia huku watu 4,194 wakijeruhiwa kutokana na ajali za barabarani hasa zinazotokana na pikipiki (bodaboda).

Mbali na mwendokasi na ulevi vinavyojulikana kuwa visababishi vikubwa vya ajali za barabarani, kusinzia wakati wa kuendesha gari pia ni moja ya sababu zinazochangia kukatili maisha ya maelfu ya Watanzania wakiwa barabarani.

Kifanyike nini kuzuia vifo hivi?

Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Tanzania (NRSC) kupitia kitabu cha Kanuni za barabara linashauri mtu kuwa katika hali nzuri kila atumiapo barabara.

“Unatakiwa kuwa katika hali nzuri kuweza kuitumia barabara kwa usalama. Iwapo hutakuwa katika hali nzuri, usiendeshe. Tafuta msaada iwapo unatakiwa kwenda mahali fulani,” inasomeka sehemu ya kitabu hicho.

Kuwa katika hali nzuri ni pamoja na kutokuwa na usingizi au uchovu uliopitiliza wakati wa kuendesha chombo cha moto. 

Kama utaendesha gari ukiwa na usingizi au uchovu uliopitiliza, ni rahisi kufumba macho na kujikuta unapoteza mwelekeo wa safari yako na hivyo kupata ajali.


Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka 2018 pekee watu 1,912 waliaga dunia huku watu 4,194 wakijeruhiwa kutokana na ajali za barabarani. Picha| Mtandao.

Hata hivyo, kuna mara kadhaa watu wanajikuta hawana la kufanya kwani kwa namna moja au nyingine, ni lazima utahitaji kurudi nyumbani baada ya kazi za muda mrefu au dharula inayokutaka ufike mahali fulani kwa muda mfupi. Fanya haya kuondoa uchovu na kuepuka usingizi wakati unaendesha chombo cha moto. 

Sikiliza ukipendacho kupitia redio yako

Mbali na kukuepusha kuboreka na kuishia kutumia simu, kusikiliza kpindi cha redio ukipendacho wakati unaendesha gani itakusaidia kuondoa usingizi kwani utakuwa makini wakati ukiendesha.

Kama sio kipindi cha redio, unaweza ukaweka vibao vyako vya muziki unavyovipenda na kuimba huku unaendesha. Siyo busara kuweka nyimbo ambazo hazitokufurahisha kwani zitahamisha mwelekeo wako na huenda ukaanza kusinzia.

Tumia vitafunwa au kahawa ukiwa unaendesha 

Kama una usingizi sana, chagua kitafunwa au kinywaji kama kahawa kitakachokupatia msisimko fulani na kuichangamsha akili na kukuongezea umakini ukiwa barabarani.

“Nikishajiona napiga miayo, naita mtu wa kau kau nanunua zenye pilipili ili ziniwashe vizuri. Hapo usingizi wote unapotea,” anasema Meneja wa kampuni ya kusaga unga ya Lina Mills, Christian Kulwa.



Tafuta mtu wa kuongozana naye

Ni vema wakati wa safari usiwe pekee yako, tafuta mtu ambaye mtakuwa naye kwenye gari ili kuepeka upweke na uchovu. 

Kama hiyo haiwezekani, toa lifti njiani  asiye na usafiri binafsi ambaye anakwenda njia moja na wewe. Unaweza kumfahamu mtu huyo kwa kujenga tabia ya kusalimia watu wanaokuzunguka na kuwauliza wanapoishi.  

Ukishampata, jenga mahusiano chanya yatakayowapatia uhuru wa kuzungumza na kubadilishana mawazo wakati unaendesha. 

Pumzika walau kwa saa moja au nusu saa kabla ya kuanza safari yako

Ni ngumu kwa wale wanaofanya kazi maofisini lakini pia unaweza kufanya hivyo endapo umemaliza kazi zako zote.

Unaweza kujiwekea nusu saa ambapo utapumzika na kisha kuamka kwa msaada wa “Alarm” (teknolojia ya kukusaidia kuamka iliyopo kwenye simu na saa)

Kama unatokea nyumbanani, unaweza kupata nusu saa ya kulala kidogo ukisha oga na hakikisha unategesha alarm yako mara nyingi uwezavyo ili usipitilize. Njia hii itafanya kazi kwa wanaume wengi na wanawake wasiojiremba sana pale watakapo kutoka.

Kwa wanaojiremba, wanaweza kutegesha alarm iwaamshe mapema zaidi ila wapate wasaa wakufanya hivyo.

Hakuna haja yakujikaza kuendelea na safari ambayo mwisho wake unaweza usiwe mzuri. Picha| Traveldudes.

Ukizidiwa, egesha gari lako pembeni, pumzika

Huenda unasafari ndefu sana mbele yako na tayari umeshanza kusikia usingizi. Cha kufanya endapo muziki hautokuwa na msaada cha kufanya ni kuegesha gari pembeni na kisha kulala kwa walau lisali moja.

Hakuna haja yakujikaza kuendelea na safari ambayo mwisho wake unaweza usiwe mzuri.

Kwa kuepuka kusinzia, utazuia ajali za barabarani na utaokoa maisha yako na ya wengine. Umeguswa? Endelea kufuatilia mitandoa ya kijamiii kwa habari zitakazo kugusa zaidi.