Njia nne za kukabiliana na sumu wakati wa dharula
Ni viyeyusha sumu vya asili ikiwemo kitunguu swaumu, mkaa na ndizi mbivu ambavyo hutumika kupunguza makali ya sumu au maumivu kabla ya kwenda hospitali.
- Hutumika zaidi kupunguza makali ya sumu au maumivu kabla ya kwenda hospitali.
- Ni viyeyusha sumu vya asili ikiwemo kitunguu swaumu, mkaa na ndizi mbivu.
- Hata baada ya kutumia, unashauriwa kwenda hospitali kupata matibabu.
Katika mizunguko na shughuli za kila siku tunazofanya kazini au nyumbani, tunakutana na viambata sumu mbalimbali na hata wadudu wadogo wadogo (micro organisms) wanaoweza kutudhuru na kusababisha magonjwa katika miili yetu.
Pia tunaweza kugusa sumu kupitia kuchomwa na mimea, kuumwa na wadudu na hata pia wanyama. Katika hali ya kawaida unaweza kupata ajali kama hizi na ukakosa msaada wa haraka wa huduma za kisasa.
Pale ambapo huduma hizi hazipo karibu na wewe, basi usihofu kwa sababu maisha yatakuwa salama baada ya kufahamu viyeyusha sumu (universal antidotes) vinavyoweza kuokoa maisha yako popote ulipo.
Inashauriwa kuwa navyo katika matembezi na shughuli mbalimbali ikiwemo mbugani na msitumi. Viyeyusa sumu hivi vya asili vinatumika kupambana na sumu na maambukizi ya magonjwa.
Mkaa (Activated charcoal)
Unaweza kushangaa! ndiyo mkaa ni dawa. Kuna zaidi ya vitu 80 vya hatari ambavyo mkaa una uwezo mkubwa wa kuneutralize (kuvisawazisha). Una uwezo wa kuzuia sumu 29 kati ya 30 zinazoongoza kuua duniani ikiwemo inayoingia kupitia kinywa na ngozi.
Pia unawafaa watu waliokunywa dawa za kawaida kupita kiasi na kupata matatizo katika miili yao.
Ina uwezo mkubwa dhidi ya maambukizi tofauti tofauti. Kutafuna vipande kumi saizi ya kidonge na kuvinywa na maji huweza kuzuia sumu iliyoingia mwili isikudhuru zaidi na kukupa nafasi ya kufika katika kituo cha afya kwa matibabu zaidi.
Hata hivyo, haitumiki kutibu sumu inayotokana na tindikali na pombe.
Mkaa ni dawa ambayo hutumika kuondoa sumu mwilini. Picha|Mtandao.
Kitunguu Swaumu (Garlic)
Kuna zaidi ya magonjwa 45 ambayo kitunguu swaumu kibichi kina uwezo wa kutibu ipasavyo. Kina nguvu dhidi ya bakteria, virusi na maambukizi ya fangasi.
Kina viwango vikubwa vya kiambata cha “germanium” kuliko mmea au chakula chochote kile ambacho kinatibu magonjwa mengi na kuondoa sumu mwilini.
Ili kilete matokeo mazuri mwilini, kitunguu swaumu kinatakiwa kiwe kibichi ambapo unaweza kutafuna au kukikata katika vipande vidogo vidogo na kuchanganya kwenye maji.
Hata hivyo, wakati wa kutumia unaweza kupata harufu mbaya mdomoni ambayo hutokana na kemikali ya AMS (allyl methyl sulfide). Harufu mbaya hii, hata hivyo, yaweza kupunguzwa kwa kunywa maziwa, kunywa maji mengi au kutafuna karafuu.
Kwa baadhi ya watumiaji, vinaweza kuwaletea mzio au mcharuko mwili (allergies au inflammatory reactions), kichefuchefu, kutapika na kuharisha. Ikikutokea kuharisha siku mbili tatu furahi kwani ni njia mojawapo ya mwili kujisafisha.
Soma zaidi:
- Watafiti watofautiana matumizi vifaa vya kukaushia mikono
- Teknolojia ya kisasa kuongeza ufanisi matibabu ya figo Muhimbili
- MOI kuanza upasuaji wa ubongo kwa teknolojia ya kisasa
Vitamini C
Kiambata hiki ni cha ajabu sana. Husaidia seli hai nyeupe za damu kwa kuziongezea nguvu ya kupigana dhidi ya magonjwa na sumu aina tofauti ambazo zinaingia mwilini.
Ni muhimu kwa afya na kuimarisha mifupa, meno, fizi na mishipa ya damu. Inasaidia pia mwili kufyonza madini ya chuma, kuponya vidonda na kazi za ubongo.
Vitamini C ni kirutubisho kinachopenya kwenye maji na hupatikana kwenye vyakula. Katika mwili kinafanya kazi kama kiosha sumu na husaidia kulinda seli zisiharibike.
Vitamini C hupatikana katika vyakula mbalimbali tulavyo kila siku zikiwemo mbogamboga za majani hasa zenye rangi ya kijani (mchicha, sukuma wiki, mchicha, matembele, spinachi, mnafu, kabeji majani ya kunde au maboga, ya maharage,kisamvu, pilipili hoho); matunda na mimea yenye miziz kama viazi.
Ulaji wa matunda na mbogamboga na matumizi ya ndizi mzuzu pia ni njia mojawapo ya kujikinga na magonjwa na sumu mwilini. Picha|Lorena Medina/Unsplash.
Ndizi Mzuzu (Plantain)
Ni kiungo cha asili ambacho hupatikana sehemu nyingi duniani. Ukiachilia mbali inavyotumika kama chakula, ni moja kati ya nyenzo za haraka kujisaidia ukipata matatizo ya kiafya.
Husaidia kuondoa aina tofauti za sumu zitokanazo na kuumwa na wadudu. Tafuta au saga majani yake kisha paka tui lake mahala pale ulipoumwa au kuathirika kisha tafuta msaada zaidi.
Hizi ni njia rahisi ambazo katika hali ya dharula zinaweza kukusaidia kuokoa maisha ili kuweza kufikia huduma ya afya iliyo karibu nawe.
Lakini siyo mbadala wa matibabu ya hospitali. Iwapo umepata tatizo, nyenzo hizi huweza kukupa nafuu mpaka pale utakapopata huduma.
Sumu hutofautiana nguvu, kiasi kilichoingia mwilini na kusambaa na vitu vingine vingi. Utakapotumia nyenzo hizi za dharula inakupa nafasi ya kupunguza makali na kama ni kiwanga cha chini kuondosha kabisa madhara ya sumu hiyo.
Dk Joshua Lameck Sultan ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba katika Chuo cha Tiba na Sayansi Shirikishi Moshi (KCMC) pamoja na hospitali ya KCMC. Pia ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) ambapo hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.