October 8, 2024

Kabendera kutoshiriki msiba wa mama yake

Ni bayana sasa kuwa Mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera hataweza kupata fursa ya kushiriki msiba wa mama yake baada Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kueleza kuwa haina mamlaka ya kusikiliza maombi ya kumruhusu kushiriki maziko ama kuaga mwili

  • Ni baada Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kueleza kuwa haina mamlaka ya kusikiliza maombi ya kumruhusu kushiriki maziko ama kuaga mwili wa mzazi huyo.
  • Mama yake Kabendera alifariki alifariki Desemba 31 2019 na mwili wake unatarajiwa kuagwa kesho katika Kanisa Katoliki la Chang’ombe.
  • Kabendera anakabiliwa na mashataka ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana. 

Dar es Salaam. Ni bayana sasa kuwa Mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera hataweza kupata fursa ya kushiriki msiba wa mama yake baada Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kueleza kuwa haina mamlaka ya kusikiliza maombi ya kumruhusu kushiriki maziko ama kuaga mwili wa mzazi huyo.

Mawakili wa Kabendera waliwasilisha maombi madogo mahakamani hapo leo wakiomba mahakama hiyo imruhusu Kabendera kushiriki msiba huo wa mama yake Verdiana Mjwahuzi (80) akiwa chini ya ulinzi. 

Mjwahuzi alifariki Desemba 31 2019 na mwili wake unatarajiwa kuagwa kesho katika Kanisa Katoliki la Chang’ombe kabla ya kusafirishwa Jumamosi kwenda Bukoba kwa maziko.

Katika hoja zao, Wakili kiongozi wa Kabendera Jebra Kambole ameiambia mahakama kuwa ni haki ya msingi ya kimahakama kwa Kabendera kuhudhuria maziko au sala za mwisho.

“Mtu anatakiwa adhaniwe kwamba hajatenda kosa mpaka pale itapothibitika. Kwa kumzuia Erick kushiriki maziko au kutoa heshima ya mwisho tutakuwa tunamuadhibu. Adhabu hiyo itakuwa kubwa na ni ya kinyama,” amesema Kambole mahakamani hapo wakati akijenga hoja kuhusu maombi hayo.

Kambole amesema kuwa tangu Kabendera akamatwe hajawahi kufanya fujo wala kutaka kutoroka hivyo haitakuwa rahisi kutoroka akipewa fursa hiyo kwa kuwa hadi sasa anaumwa na anatembea kwa shida.

Ameeleza kuwa tukio la heshima za mwisho linafanyika Dar es Salaam siyo mbali sana na linafanyika mchana haitakuwa vigumu Erick kupelekwa kanisani Chang’ombe na ulinzi kwa kuwa hapo nyuma alishawahi kupelekwa Hospitali ya Amana kwa ajili ya matibabu.

“Tunaamini kuwa kwa kumruhusu mtuhumiwa kwenda kutoa heshima za mwisho jamhuri haiwezi kuathirika. Hawawezi kuumwa yeye akihudhuria maziko ya mama yake mzazi. In that sense of humanity (katika hali hiyo ya kibinadamu) tunaiomba mahakama iweze kutoa amri ya kutoa heshima za mwisho under escort (chini ya uangalizi) kesho Saa 6 mchana,” amesema Kambole.


Soma zaidi: 


Hata baada ya upande wa mawakili wa Kabendera kutoa hoja hizo, upande wa Serikali ulipingana na maombi hayo ukisema kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kushughulikia kesi za uhujumu uchumi.

“Nichukue nafasi hii kumpa pole Erick kwa kufiwa na Mama yake mzazi. Hili ni jambo la majonzi kwa binadamu yeyote lakini hoja hizo zilizotolewa na Jebra Kambole itoshe kusema tunazipinga,” amesema Wakili wa Serikali Wankyo Simon kabla ya kuanza kutoa sababu za kupinga maombi hayo.

Simon amesema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashauri ya uhujumu uchumi na mwenye nguvu hiyo ni Mahakama Kuu. 

“Pamoja na kusikitika kwa msiba huo, ni wazi mahakama yako tukufu imefungwa mikono kisheria kwa sababu haina mamlaka kwa sababu DPP hajaipa mahakama hii kibali kushughulikia mashauri yaliyopo chini ya sheria ya makosa ya uhujumu uchumi na hati ya kumruhusu mahakama hii ya kusikiliza shauri hili,” amesema Simon.

“Suala la msiba ni la kibinadamu lakini suala kubwa na la msingi ni kuzingatia sheria za nchi. Katika shauri hili mahakama imefungwa na sheria… hoja hizi hata kama ni nzito zinakosa kupenya katika mikono ya sheria. Mahakama hii haina mamlaka na shauri hili tunaomba itupilie mbali maombi hayo,” ameongeza Simon katika kesi hiyo iliyovutia watu wengi.

Mwanahabari, Erick Kabendera (kushoto) akiwa na Wakili wake, Jebra Kambole katika chumba cha mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakati kesi yake ilipotajwa leo Januari 2, 2020.

Akitoa huhumu juu ya maombi hayo madogo, Hakimu Mwandamizi Janeth Mtega amesema kuwa anaungana na mawakili wa Serikali kuwa mahakama yake haina mamlaka kisheria kushughulikia maombi hayo.

“Mahakama hii imefungwa mikono kisheria. Maombi haya hayana nafasi leo kwa kuwa mahakama haina mamlaka,” amesema Mtega.

Baada ya hukumu hiyo ndugu wa Kabendera walianza kububujikwa na machozi na baadaye kuangua vilio baada ya kutoka katika chumba cha mahakama. 

Baadhi ya ndugu waliojikaza na hali hiyo walianza kuwasaidia wenzao na kuwatuliza wakati wakishuka ngazi za mahakama hiyo iliyopo katikati ya Jiji.

Nje ya mahakama, Kambole amewaambia wanahabari kuwa hawajaridhika na uamuzi huo na bado wanaamini kuwa mahakama ilikuwa na uwezo wa kusikiliza maombi madogo madogo kama yao.

“Kimsingi hatujaridhika na uamuzi huu na tunaona siyo halali. Kwa kuwa jambo hili linafanyika kesho hatuwezi kukata rufaa,” amesema Kabendera

“Tunaomba Watanzania waendelee kumuombea Erick.”

Naye Mratibu wa Watetezi wa Haki za Binadamu Onesmo Ole Ngurumwa amesema nje ya mahakama kuwa aliongea na Erick mchana wa leo na kwamba alikuwa tayari kwa maamuzi yeyote.

“Erick amesema atakayoyapata yatabaki milele. Suala hili la kumnyima kumuaga Mama yake ni jeraha atakalobaki nalo maisha yake yote,” amesema Ole Ngurumwa.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha inayokabili Kabendera imeahirishwa hadi Januari 13, 2020 itakapotajwa tena baada ya upelelezi wa mashtaka yanayomkabili kutokamilika.