November 24, 2024

Kusafiri na watoto kunavyochangia uelewa wa masomo shuleni

Matokeo chanya ya kusafiri yanaweza kuongeza wigo wa mwanafunzi katika elimu na taaluma yake na kumuongezea uwezo wa kujifunza vitu vipya.

  • Utafiti uliofanywa huko Marekani unaelewa kuwa, kuna matokeo chanya kwa maendeleo binafsi ya mwanafunzi anayesafiri. 
  • Matokeo chanya ya kusafiri yanaweza kuongeza wigo wa mwanafunzi katika elimu na taaluma yake. 
  • Walimu wapendekeza wanafunzi wasafiri wakati wa likizo na waongozwe na wazazi. 

Ni msimu wa mwisho wa mwaka, wazazi na walezi kila mahali wanakuna vichwa ni jinsi gani watafanikisha elimu ya watoto wao mwaka 2021. 

Tunaweza kusema ni kipindi kigumu kidogo kwa sababu pesa huwatoka wazazi ili kukidhi mahitaji ya ada na gharama za vifaa vya masomo kwa wanafunzi wanaoanza masomo Januari mwaka ujao. 

Wakati wazazi wakiwaza hayo, huenda wamesahau kuwa suala la watoto wao kufanikiwa katika masomo ni mchanganyiko wa mambo mengi. Mojawapo ni kuwapa watoto nafasi ya kujifunza mambo mengine zaidi ya yale wanayoyapata darasani. 

Utafiti mpya uliofanywa na chama cha Wanafunzi na Vijana Wanaosafiri (SYTA) cha Marekani kati ya Agosti 2013 na Novemba 2015 unapendekeza kuwa, ikiwa unataka watoto wako wapate mafanikio wakiwa shuleni, unatakiwa kuwapa mapumziko ya kutosha ikiwemo kusafari sana. 

Utafiti huo uliopewa jina la “Student and Youth Travel Digest” uliowahoji takriban walimu 1,500 wa Marekani, ulibaini kuwa asilimia 74 ya wakufunzi wanaamini kuwa kusafiri, “kuna matokeo chanya kwa maendeleo binafsi ya mwanafunzi.”

Walimu wengi (asilimia 56) katika utafiti huo, nao wanaamini kuwa matokeo chanya ya kusafiri yanaweza kuongeza wigo wa mwanafunzi katika elimu na taaluma yake. 


Zinazohusiana


Walimu wanakubaliana kuwa wanafunzi ambao wanasafiri hasa kipindi cha likizo kwenda kujionea tamaduni tofauti na walizozizoea wameonyesha kuongeza uvumilivu na heshima, utayari wa kujifunza na kujaribu vitu vipya. 

Hivi karibuni, www.nukta.co.tz iliongea na Mmiliki wa shule ya Stars Academy ya jijini Arusha ambaye pia ni mwandishi wa vitabu (The Color of Life), Ritha Tarimo ambaye alisema mafanikio ya mwanafunzi hayapimwi pekee na ufaulu wa darasani bali uwezo wake wa kujifunza vitu vipya nje ya mazingira aliyoyazoea.

“Tunafikiri watoto wakipata ufaulu wa asilimia 100 au alama A ni uerevu na ndiyo maana tunaogopa kuwaacha wachunguze vitu vingine kwa sababu tunapima uelewa kama rula. 

“Wazazi wajue kuwa watoto wanahitaji kufahamu mambo mengine kwani siyo tu elimu ya darasani inayomfanya mtu kuwa mwerevu,” alisema Tarimo wakati akiongea na Nukta.

Siyo tu walimu wanaamini kuwa kusafiri kunawasaidia wanafunzi darasani, pia inaweza kuwasaidia wakiwa mtaani au nyumbani. 

Walimu wanakubaliana kuwa wanafunzi ambao wanasafiri hasa kipindi cha likizo kwenda kujionea tamaduni tofauti na walizozizoea wameonyesha kuongeza uvumilivu na heshima, utayari wa kujifunza na kujaribu vitu vipya. Picha| Zach Vessels/Unsplash.

Utafiti huo unaeleza zaidi kuwa, watoto wanaosafiri wana uwezekano mkubwa wa kuwa huru, kujiamini, kujijari, kujieleza, kuendana na kuishi vizuri katika mazingira yanayowazunguka kuliko wenzao wanaokaa nyumbani. 

Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa matokeo chanya ya kusafiri siyo lazima yatokane na kusafiri nchi za nje mbali na anakoishi mtoto. Hata kusafiri ndani ya nchi lakini eneo ambalo ni tofauti na mazingira aliyozoea mtoto, inachagiza uwezo wa kujifunza na kuelewa mambo anayofundishwa.

Utafiti huo, pia umebaini kuwa watoto ambao walipata fursa ya kusafiri mara moja, wameonyesha shauku ya kutaka kusafiri zaidi katika maeneo mengine. 

Walimu hao wa Marekani wameshauri kuwa ni muhimu wanafunzi wawekewe mipaka ya kusafiri ili kutoa nafasi kwa wao kuzingatia masomo darasani. 

Na kipindi kizuri cha kusafiri, kinachopendekezwa ni wakati likizo kwa sababu mwanafunzi anakuwa na shughuli chache za darasani. 

Kama wewe ni mzazi, unataka mtoto wako afanikiwe katika masomo mwaka 2020, basi ni vema katika bajeti yako, mwandalie bajeti ya kumsafirisha katika maeneo ambayo unadhani utapata kitu kimpya. 

Itazame elimu ya mtoto wako kwa jicho pana zaidi. Mafanikio ya elimu siyo darasani tu.