Majaliwa atoa agizo zito ujenzi wa madarasa kidato cha kwanza 2020
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa nchini wahakikishe wanasimamia ipasavyo ujenzi wa vyumba vya madarasa vikamilike kwa wakati ili wanafunzi wote waliochagulia kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2020 waanze masomo kwa pamoja.
- Awataka wakuu wa mikoa nchini wahakikishe wanasimamia ipasavyo ujenzi wa vyumba vya madarasa vikamilike kwa wakati.
- Amesema waliochagulia kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2020 waanze masomo kwa pamoja.
- Aagiza wasimamie vizuri elimu kwa watoto wa kike na kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kuwakatisha masomo.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa nchini wahakikishe wanasimamia ipasavyo ujenzi wa vyumba vya madarasa vikamilike kwa wakati ili wanafunzi wote waliochagulia kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2020 waanze masomo kwa pamoja na kuwawezesha kufanya vizuri katika masomo yao.
Majaliwa aliyekuwa akizungumza Desemba 29, 2019 katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ya Ruangwa, amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote wanaanza kusoma kwa pamoja kwa sababu wakipishana muda wa kuanza masomo baadhi yao wanashindwa kufanya vizuri jambo ambalo si sahihi.
“Wakuu wa Mikoa hakikisheni vyumba vya madarasa vinakamilika ili wanafunzi wote waliofaulu waanze masomo kwa pamoja. Kitendo cha wanafunzi kupishana kuanza masomo kinawafanya waliochelewa kutofanya vizuri katika mitihani yao,” amesema Majaliwa katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, jumla ya watahiniwa 933,369 sawa na asilimia 98.55 ya waliosajiliwa walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019 na kati yao watahiniwa 759,737 wamefaulu.
Kati yao wasichana ni 395,738 ambao wanasubiri kujiunga na elimu ya sekondari mwezi Januari, 2020.
Idadi ya wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza imekuwa ikiongeza kila mwaka na kutoa changamoto kwa Serikali kujenga vyumba vya madarasa ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi.
Mwaka 2018 watahiniwa waliofaulu walikuwa asilimia 77.72, hivyo kuna ongezeko la ufaulu kwa asilimia 3.78 kwa mwaka huu.
Zinazohusiana:
- Mbinu zitakazowasaidia watahiniwa darasa la saba kufanya vizuri.
- Necta yafuta matokeo ya watahiniwa 909 darasa la saba
- Kanda ya ziwa yatikisa matokeo darasa la saba 2019
Aidha, Waziri Mkuu amewasisitiza viongozi hao wahakikishe wanasimamia vizuri elimu kwa watoto wa kike na kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kuwakatisha masomo iwe kwa kuwaoa, kuwaozesha au kuwapa ujauzito.
Amesema Serikali imeweka sheria kali ya kumlinda mtoto wa kike lengo ni kumuwezesha amalize masomo yake ili aweze kujikwamua kiuchumi na aondokane na utegemezi, hivyo ni marufuku kuwakatisha masomo.
“Watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii na Serikali itatoa adhabu kali ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu atakayekatisha elimu ya mtoto wa kike iwe kwa kumuoa au kumpa ujauzito,” amesisitiza Majaliwa.
Waziri Mkuu amebainisha kuwa Serikali inataka kuona idadi kubwa ya watoto wa kike wanatimiza malengo yao kielimu, hivyo ni lazima wakaondolewa vishawishi kwa kuboresha mazingira yao ya kujifunzia ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya mabweni.