Fanya haya kabla hujaingia 2020
Baadhi ya mambo hayo ni kupanga ratiba, bajeti na mipango utakayotekeleza mwaka 2020. Mipango itakusaidia kutumia vizuri muda na kipato utakachokipata mwaka ujao.
- Baadhi ya mambo hayo ni kupanga ratiba, bajeti na mipango utakayotekeleza mwaka 2020.
- Mipango itakusaidia kutumia vizuri muda na kipato utakachokipata mwaka ujao.
Ni msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka yaani Krismas na kuukaribisha mwaka mpya wa 2020. Yapo mengi ya kufanya ili kumaliza vizuri mwaka na kuanza mwaka mwingine kwa nguvu ili kutimiza malengo tuliyojiwekea.
Licha ya kuwa kipindi hiki watu wengi hukitumia kujumuika na wawapendao kwa mapumziko baada ya shughuli nyingi za mwaka mzima, lakini ni kipindi pia cha kutafakari kuhusu mwaka mpya.
Mipango na kufanikiwa kwako katika mwaka ujao kutategemea sana ulivyojiandaa mwisho wa mwaka. Waswahili wanasema safari moja huanzisha safari nyingine.
Ni mambo gani ya muhimu unayotakiwa kufanya kipindi hiki kujiandaa na mwaka unaofuata? Na ujiandae katika mambo gani?
Tengeneza kalenda na ratiba
Tengeneza orodha ya vitu unavyokusudia kufanya mwaka ujao huku ukivipangilia kwa muda utakaotumika kuvifanya. Huenda viko vingi lakini unaweza kuchagua kwanza vile vya umuhimu kama safari, mafunzo, mazoezi na hata shughuli za kikazi na biashara.
Kupanga ratiba ya mwaka mzima ambayo unaweza kuitengenezea kalenda ili ukumbuke vizuri, ni hatua mojawapo itakayokusaidia kuanza mwaka vizuri na kupata mafanikio uliyokusudia.
Tumia programu ya “Google Calendar” kupangilia ratiba ya mambo utakayofanya. Programu hii itakukumbusha hata kama umesahau kufanya jambo ulilopanga kufanya.
Kupata ratiba ya mambo yaliyopo mbele yako, kunakusaidia kutumia vizuri muda wako na kuepuka vitu visivyo na umuhimu kuingilia kati. Kupanga ratiba ni suala moja, lakini kutekeleza kunategemea utashi wako.
Kufanikiwa kwako mwaka ujao kwa yale utakayokuwa unayofanya kunategemea zaidi ulivyopangilia vizuri bajeti yako katika ngazi ya familia na hata katika miradi na biashara zako. Picha| Thought Catalog/Unsplash
Panga bajeti ya mwaka 2020
Usisubiri mpaka umesheherekea mwaka mpya, ndiyo uanze kupanga bajeti yako ya mwaka 2020. Muda mzuri wa kupanga matumizi na mapato yako ni sasa kwa sababu kila kitu ni mipango.
Kufanikiwa kwako mwaka ujao kwa yale utakayokuwa unayofanya kunategemea zaidi ulivyopangilia vizuri bajeti yako katika ngazi ya familia na hata katika miradi na biashara zako.
Kwa mujibu wa Jesse Mecham, mwandishi wa kitabu cha Unahitaji Bajeti (You Need a Budget), panga malengo ya kifedha unayokusudia kuyapata mwaka ujao na jinsi utakavyosimamia fedha zako mwaka 2020.
Anasema fikiria pia unavyoweza kubadili tabia zako ili kufikia malengo hayo ikiwemo kuacha matumizi holela ya fedha yasiyozingatia mipango.
Tumia vizuri likizo yako
Huenda wewe ni mfanyakazi au mfanyabiashara, hadi unapomaliza mwaka hujapata muda wa kwenda mapumziko kutokana na wingi wa kazi. Basi ni vema katika kalenda yako ya mwaka 2020, fidia siku ambazo hukukwenda likizo.
Tena unaweza kwenda likizo miezi ya mwanzoni ya mwaka mpya ili kukusanya nguvu ya kuendelea na safari ya mwaka mzima. Ukifanya kazi unahitaji mapumziko.
Pata muda wa kufurahia kazi ya mikono yako. Tafuta eneo zuri ambalo utapata nafasi ya kupumzisha akili na mwili wako.
Zinazohusiana:
- Jinsi ya kufanya mitandao ya kijamii isikuharibie mahusiano yako
- Utaoa, utaolewa lini: Jinsi unavyoweza kukabiliana na msukumo wa nje wa ndoa
- Mambo ya kufanya wakati wa mapumziko ya mwisho wa mwaka
Panga vizuri picha kwenye simu yako
Mwaka 2019 ulikuwa wa kumbukumbu nyingi za furaha na kuhuzunisha ambazo umezitunza katika picha zako zilizopo kwenye simu. Huenda simu yako imejaa kwa picha nyingi.
Mtaalam wa mipango kutoka kampuni ya Modular Closets, Marty Basher anashauri kuwa pata muda kabla ya kumaliza mwaka kuzipangilia vizuri picha ulizopiga na futa zile ambazo hauzihitaji tena.
Anasema hatua hiyo, itakusaidia kupata nafasi kwenye simu yako kwa ajili ya kutunza picha utakazopiga mwaka ujao.
Weka sawa nyaraka na mahesabu yako
Mwisho wa mwaka, kampuni na wamiliki wa biashara hutumia kufunga mahesabu. Na wewe ni wakati wako wa kuhakikisha nyaraka zote muhimu zikiwemo risiti, bili na mahesabu yamepangwa vizuri.
Zitunze nyaraka hizo sehemu nzuri ili kuepuka upotevu. Pia unaweza kuziskani na kuzitunza mtandaoni.
“Kuwa na nyaraka nyingi za kifedha na nyingine mtandaoni, kunakuwa hakuna haja ya kuzitunza kwenye makaratasi,” ameshauri Mwanzilishi wa taasisi ya Young Adult Money, David Carlson.
Kwa kufanya hivyo, utaanza mwaka mpya vizuri na hutahofia chochote kwa sababu kimepangwa vizuri.
Mwaka mpya uwe wa mipango endelevu inayotekelezeka. Picha| Adeolu Eletu/Unsplash.
Pangilia vizuri nguo zako kwenye kabati
Huenda kabati la kuhifadhia nguo zako limejaa. Ni wakati wa kukagua na kupanga upya. Unashauriwa kulisafisha na kuondoa nguo zote ambazo unafikiri huwezi kuzitumia tena mwakani.
Nguo hizo wape watu wenye uhitaji kipindi hiki cha sikukuu ili nao wafurahie. Kupunguza nguo kwenye kabati kutakupa nafasi ya kuweka zingine endapo utanunua mwaka 2020.
Nakutakia mapumziko mema ya mwisho wa mwaka na fanaka tele unapokaribia kuingia mwaka 2020.
Daniel Samson ni Mhariri wa tovuti ya habari ya Nukta, anapatikana kwa barua pepe: dsamson@nukta.co.tz na Twitter: @Mwalu_Danny.