November 24, 2024

Haya ndiyo maeneo ambayo watu wanataka kwenda 2019

Orodha hiyo ni sehemu ya watu, mada, matukio, maeneo, na habari za kimataifa ambazo zilitafutwa zaidi katika mtandao wa Google kwa mwaka 2019.

Kwa mujibu wa Google, maeneo 10 ambayo watu wanapendelea kwenda duniani ni pamoja na kisiwa cha Maldives ambacho kimeshika nafasi ya kwanza kutafutwa na watu katika mtandao huo. Picha| Jennvmy/Unsplash.


  • Kisiwa cha Maldives, Kusini Magharibi mwa nchi za Sri Lanka na India kimeshikwa nafasi ya kwanza kutafutwa zaidi na watu. 
  • Watu wengi wanaotafuta maeneo ya kutembelea, wanapendelea zaidi kwenda Marekani.

Dar es Salaam. Kama tayari au unapanga kutafuta mahali utakapokwenda kutumia mapumziko yako ya mwisho wa mwaka, wewe na umpendaye, basi mtandao wa Google umekurahishia kazi. 

Mtandao huo umetoa orodha yake ya mwaka 2019 ya maeneo 10 duniani ambayo watu wengi walikuwa wanatafuta katika kitafutio chake cha “Google Search” kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo mapumziko. 

Orodha hiyo ni sehemu ya  watu, mada, matukio, maeneo, na habari za kimataifa ambazo ziligonga vichwa vya watu katika mtandao huo kwa mwaka 2019. 

Pia imeonyesha mada zilizovuma zaidi katika nyanja mbalimbali za muziki, michezo, sanaa, utamaduni, habari, siasa, teknolojia ikijumuisha ni wapi ambapo watu wengi walitamani kwenda. 

Kwa mujibu wa Google, maeneo 10 ambayo watu wanapendelea kwenda duniani ni pamoja na kisiwa cha Maldives ambacho kimeshika nafasi ya kwanza kutafutwa na watu katika mtandao huo. 

Kisiwa hicho kiko kwenye bahari ya Hindi, Kusini Magharibi mwa nchi za Sri Lanka na India, takriban kilomita 1,000 kutoka bara la Asia, kikisifika zaidi kwa fukwe na samaki ambao wamekuwa kivutio kikubwa cha watalii wanaopenda kupata jua na upepo mwanana wa bahari. 

Orodha hiyo imetawaliwa na miji kutoka Marekani ambapo imeiingiza maeneo sita, jambo ambalo linaashiria kuwa huenda watu wengi wanapenda kwenda katika nchi hiyo yenye uchumi mkubwa duniani. 

Maeneo mengine yaliyotafutwa zaidi ni nchi ya Japan, kisiwa cha Bora Bora (French Polynesia), Las Vegas (Marekani), Mexico, majimbo ya Alaska, New Orleans na California, New York nchini Marekani. Na nchi ya  Costa Rica ambayo imefunga 10 bora ya maeneo yaliyotafutwa zaidi mwaka 2019, inasifika zaidi kwa kuwa na ukanda mpana wa fukwe na mbuga za wanyama. 


 Zinazohusiana:


Huenda maeneo hayo yataendelea kutafutwa zaidi mwaka 2020, kwa sababu ni maeneo muhimu kuvutia wasafiri na utalii kutoka maeneo mbalimbali duniani. 

Lakini kama uko Tanzania na huna uwezo wa kwenda nje ya nchi bado una fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii nchini ambayo yanafaa kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka. 

Maeneo hayo ni pamoja na hifadhi ya Taifa ya Serengeti yenye kambi mbalimbali na ‘Bustani ya Mungu’ maarufu kama hifadhi ya Taifa ya Kitulo ambayo ni ya 14 kuanzishwa hapa nchi mwaka 2005.

Ukiwa Kitulo utapata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo kupanda Mlima LivingStone ambao uko karibu na ziwa Nyasa, kupanda farasi, michezo ya gofu.  

Sambamba na hilo watalii wanaotembelea hifadhi hiyo watapata upepo mwanana kutoka mwambao wa ziwa Zambwe na milio tofauti ya ndege wanaopamba hifadhi hiyo.