Fanya haya kupata muda wa kumpumzika na familia msimu wa sikukuu
Dondoo ambazo zitakusaidia kufurahia sikukuu badala ya kuzigeuza kuwa kibarua na mateso ni pamoja na kuajiri wapishi wa muda na kutoka mtoko.
- Ajiri wapishi wa muda mfupi au andaa mtoko wewe na uwapendao.
- Itakusaidia kupata muda mwingi zaidi na familia yako badala ya kila mwanafamilia kuhangaika na majukumu mbalimbali.
- Kuwa makini na panga vizuri bajeti yako.
Msimu wa sikukuu ni kati ya siku ambazo zinahusisha shughuli nyingi ili kukamilisha furaha ya watu katika familia.
Sikukuu hasa za mwisho wa mwaka zikiwemo krismasi na mwaka mpya ni kati ya sikukuu ambazo wazazi wengi hupata mawazo ya ni nini wafanye ili kuwafurahisha watoto pamoja na familia zao.
Ufanye nini basi? Hizi ndizo dondoo chache ambazo zitakusaidia kufurahia sikukuu badala ya kuzigeuza kuwa kibarua na mateso:
- Andaa mtoko
Wakati wengi wakifikiria kununua mbuzi mzima na gunia la mchele ambao huenda ukapikwa na kubaki, haina haja ya kufanya hivyo. Kama familia yako ni ya watu wachache unaweza kuandaa mtoko na kwenda sehemu nzuri kwa ajili ya kufurahia sikukuu hiyo.
Kwa wastani, sehemu nyingi za kuvinjari zikiwemo sehemu za kuogelea huwa na kiingilio cha chini cha wastani wa Sh10,000 hadi Sh15,000 ambapo gharama za chakula anaweza kuzimudu mtu hata wa kipato cha kawaida.
Kwa familia ya watu wa tano wanaweza kutumia takribani Sh200,000 wakitoka mtoko, ambayo inaweza kuwa chini ya ile inayotumika kufanya maandalizi ya nyumbani.
Mbali zaidi, itaipatia familia muda wa kuwa pamoja na kufurahia michezo mbalimbali badala ya wanawake kuhangaika kupika huku wanaume wakihangaika kuchinja vitoweo.
Soma zaidi:
- Wadau wahimiza uwekezaji, uendelezaji nishati jadidifu Tanzania
- Namna umeme vijijini unavyoweza kutumika kuchochea maendeleo
- Jumuika na ndugu na jamaa
Kama una familia kubwa, unaweza kuungana familia zingine za ndugu na marafiki kushirikiana kufanikisha sikukuu. Kwa kufanya hivyo, ni rahisi kuchangia gharama za matumizi.
Pia utapata muda mwingi wa kutumia sikukuu ukiwa umezungukwa na watu uwapendao ambao huenda kutokana na majukumu, haujaonana nao kwa muda mrefu.
- Kubali mialiko
Watu wengi huona aibu kukubali mialiko ya majirani na ndugu wakitaka kufurahia sikikuu wao kama familia. Wasilolijua ni kuwa, mialiko hiyo inawapunguzia gharama huku ikitoa nafasi ya kuonana na watu wapya ambao huenda wakawa na msaada kwako mwaka unapoanza.
Hata hivyo, siyo vyema ukialikwa uende mikono mitupu. Unaweza kuchangia gharama kidogo kwa kubeba vinywaji na hata kuandaa vitafunwa kama ndizi na viazi ambavyo utaenda navyo ugenini.
Kama familia yako ni ya watu wachache unaweza kuandaa mtoko na kwenda sehemu nzuri kwa ajili ya kufurahia sikukuu hiyo. Picha| Blake Barlow/Unsplash.
- Wape watoto wako ruhusa kwenda kusalimia ndugu na jamaa
Katika kipindi cha sikukuu, wazazi wengi huona ni muda wa kutumia na watoto wao huku kwa muda huo, watoto hao hushughulika kuandaa vyakula na vinywaji na kupoteza maana nzima ya kutumia muda na watoto wao.
Wakati watoto wako wakifurahia likizo yao, unaweza kuwaongezea furaha kwa kuwaacha watembelee shangazi, wajomba na jamaa wengine na kisha kutumia sikukuu kutoka na mke au mpenzi wako.
- Ajiri wapishi
Kutokana na ukubwa wa familia yako, unaweza kuwasiliana na wapishi ambao watawajibika kutengeneza chakula cha siku hiyo na kisha wewe na familia yako kupata muda wa pamoja.
Baadhi ya wapishi hawahitaji pesa nyingi sana kukamilisha kila kitu kwani kwa malipo ya Sh50,000 au zaidi unaweza kupata mpishi ambaye atapika chakula na kuandaa vinywaji ama kununua kwa ajili ya familia yako.
Ni muhimu kuhakikisha kuwa sikukuu zinakuwa muda wa mapumziko badala ya kuwa chanzo cha msongo wa mawazo.
Jitahidi kufanya kila lililo ndani ya uwezo wako kuhakikisha sikukuu hizi zinakupatia muda wa kutosha na familia yako.