October 8, 2024

Wafanyabiashara wajumuishwa vita ya mabadiliko ya hali ya hewa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amewataka viongozi wa makampuni ya biashara na uwekezaji duniani kuingia katika vita ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa sababu athari zake hazitamuacha mtu yoyote salama.

Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres akihutubia kikao cha ngazi ya juu kuhusu kutunza tabianchi huko Madrid, Hispania Desemba 11, 2019. Picha| UNFCCC.


  • Umoja wa Mataifa wawataka kuingia katika vita hiyo kwa sababu athari zake hazitamuacha mtu yoyote salama.
  • Serikali nazo zatakiwa kuweka sera imara dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amewataka viongozi wa makampuni ya biashara na uwekezaji duniani kuingia katika vita ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa sababu athari zake hazitamuacha mtu yoyote salama. 

Tabianchi ni mwenendo wa hali ya hewa yakiwemo majira, wastani na vizio vya juu na chini kabisa vya joto, utokeaji na mtawanyiko wa mawingu, mvua na theluji. 

Lakini huathiriwa na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa kama vile upepo mkali na kuanguka kwa theluji, na vimbunga vikali vya nchi kavu na baharini.

Guaterres aliyekuwa akizungumza jana (Desemba 11, 2019) katika mkutano wa ngazi ya juu wa mkutano wa 25 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi (COP25) mjini Madrid, Hispania amewataka viongozi katika sekta ya biashara kushika usukani na kubadili historia.

Katika taarifa iliyotolewa na UN, Guaterres amesema muda unayoyoma na kasi ya mabadiliko ya tabianchi inaanza kutupa kisogo tusiposimama imara basi tunaangamiza kizazi hiki na kichacho. 

“Hii ni nafasi nzuri hususan kwa viongozi wa biashara kubaini njia muhimu za kushiriki katika mbio hizi za kuishinda dharura ya mabadiliko ya tabianchi,” amesema Katibu Mkuu huyo katika taarifa hiyo.


Soma zaidi: 


Mapema mwaka huu, mameneja wa mali wanaowakilisha karibu nusu ya mtaji wa uwekezaji duniani,  anasema waliandika kwa viongozi wa nchi tajiri dunini za G20 wakitaka hatua za dharura za mabadiliko ya tabianchi na kuwataka kuweka bei ya maana kwenye hewa ukaa na kuacha kutoa ruzuku kwa mafuta ya kisukuku na makaa ya mawe duniani.

“Wakati tukiwashukuru viongozi hawa tunahitaji wengi zaidi kujiunga haraka na kuongeza kasi. Kiwango cha mabadiliko ya tabianchi kinaweka hatarini mustakabali wetu na maisha tutayoyajua katika sayari hii, kwani mabadiliko ya tabianchi tayari yanaathiri watu, biashara, uchumi na mfumo wa maisha kote ulimwenguni,” amesema. 

Matokeo yake yatakuwa hivi

Guterres amesema katika taarifa hiyo kuwa, kwa makampuni ya biashara kufanya hivyo yatakuwa yanachagiza mbinu mpya za kufanya biashara na kusongesha mabadiliko ya kimfumo kote duniani.

Pia yatakuwa yanatuma ujumbe wa wazi kwa walaji, wawekezaji na serikali kwamba wanadhamiria kuongoza katika mchakato wa uchumi wa dunia kuelekea mustakabali usio na hewa ukaa ifikapo 2050 na wakati huohuo jumuiya ya kifedha inazidi kuonyesha fursa za kuelekea uchumi unaojali mazingira.

Na katika kuunga mkono hatua hizo, Guterres ametoa wito kwa viongozi katika sekta binafsi na asasi za kiraia  kuzitia changamoto serikali kutumia fursa hii kuweka bayana sera zao za maendeleo ambazo zitawezesha makampuni kuwekeza katika mustakabali huru bila hewa ukaa.