Kwanini unashauriwa kukagua chakula unachonunua kabla ya kula
Usomaji wa taarifa hizo kwa umakini husaidia mtumiaji kufahamu malighafi zilizotumika kutengeneza bidhaa hizo na iwapo zina madhara au mzio kwake
- Watu wachache husoma taarifa za bidhaa za vyakula za viwandani baada ya kununua kutoka madukani
- Usomaji wa taarifa hizo kwa umakini husaidia mtumiaji kufahamu malighafi zilizotumika kutengeneza bidhaa hizo na iwapo zina madhara au mzio kwake
Dar es Salaam. Unaweza ukawa wewe ni moja wa watu wanaopendelea kununua chakula kilichotengenezwa viwandani au kuongezwa thamani.
Hata hivyo, swali kubwa la kujiuliza ni je, ni mara ngapi husoma taarifa fupi za kiafya za malighafi zilizotumika kutengeneza bidhaa hizo kila unaponunua matumizi ya taarifa fupi za kiafya zilizopo kwenye bidhaa (Food lables)?
Kwa kawaida taarifa hizo ni muhimu pindi mtu anapotaka kununua chakula kwa kuwa zinamsaidia kujua kiwango cha sukari, mafuta na usalama uliopo kwenye chakula hicho kulingana na afya yake kwa ujumla.
Inaweza ikawa sio desturi ya watu wengi wanaponunua chakula kuangalia taarifa hizo ili kulinganisha virutubisho vilivyopo kwenye chakula husika na zile anazohitaji binadamu kulingana na mwili wake.
Ukweli ni kwamba matumizi ya taarifa hizi ni muhimu. Picha | Mtandao.
Baadhi ya watumiaji wa vyakula vya viwandani wanakiri kuwa hawana utamaduni wa kusoma taarifa hizo akiwemo mkazi wa Tabata Kimanga Jijini Dar es Salaam, Tracy George.
“Kwa upande wangu tabia ya kusoma hayo mambo sina, nikishanunua chakula nilichokipenda nakula sizingatii yote hayo” amesema Tracy.
Ukweli ni kwamba matumizi ya taarifa hizi ni muhimu kwa sababu ya maumbile ya binadamu kutofautiana na kiasi cha virutubisho maalum kuwepo katika chakula kilichonunuliwa au kinachotegemea kuliwa.
Pia, taarifa hizo huwasaidia baadhi ya watu wenye mzio au waliokataliwa na daktari aina fulani vyakula kujua iwapo chakula anachokula kina viambata ambavyo hawatakiwi kuvitumia.
Wataalamu waonya
Wataalamu wa afya wanashauri kuwa watu wasile chakula kilichoongezwa thamani bila kujiridhisha na malighafi zilizotumika.
Daktari wa Hospitali ya Sanitas, Christopher Peterson ametoa ufafanuzi kwamba miili ya binadamu hutofautana katika kiasi cha virutubisho vunavyotakiwa kuingia mwilini
“Kiafya kuna viwango vya kila aina ya virutubisho viingie mwilini, kiafya. Hivyo vyakula hivyo vinakuwa na virutubisho vingi kuliko vile mwili unahitaji, kusoma kabla hujanunua ni muhimu”, amesema Dk Peterson.
Zinazohusiana:
- Jilinde dhidi ya ongezeko la mafuta mwilini kuepuka gharama kubwa za matibabu
- Fanya haya kuboresha ulaji wa chakula
Aidha, Dk Peterson ameeleza kwamba miili yetu inapokea asilimia kidogo ya virutubisho ya vile vinavyowekwa kwenye chakula hivyo usomaji wa maelezo hayo unampa uwezo mlaji kulinganisha virutubisho vilivyopo kwenye bidhaa na vile vinavyohitajika mwilini.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha afya cha Marekani Blue Health Advantage, ukuaji wa mwili wa binadamu hautegemei aina ya chakula bali idadi ya virutubisho vinavyoingia mwilini.