October 7, 2024

Elimu bure yasababisha uandikishaji madarasa ya awali kushuka

Huenda elimu ya awali nchini Tanzania ikachukua mkondo wa tofauti siku zijazo baada ya takwimu mpya kuonyesha uandikishaji wanafunzi katika madarasa ya awali umeshuka mfululizo kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita kutokana na baadhi ya wanafunzi kuandiki

  • Uandikishaji huo umekuwa ukishuka kwa miaka miwili mfululizo tangu mwaka 2017.
  • Idadi kubwa ya wanafunzi walijiunga darasa la kwanza bila kupitia elimu ya awali. 
  • Serikali yajipanga kuboresha elimu hiyo kwa kuboresha uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi. 

Dar es Salaam. Huenda elimu ya awali nchini Tanzania ikachukua mkondo wa tofauti siku zijazo baada ya takwimu mpya kuonyesha uandikishaji wanafunzi katika madarasa ya awali umeshuka mfululizo kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita kutokana na baadhi ya wanafunzi kuandikishwa darasa la kwanza moja kwa moja.  

Mtaala wa Elimu ya Awali Tanzania toleo la 2013 unabainisha kuwa elimu ya awali ni ngazi ya kwanza katika mfumo wa elimu ya Tanzania ambayo hutolewa kwa watoto wadogo kabla ya kujiunga na elimu ya msingi.

Elimu hiyo hutolewa kwa watoto kuanzia miaka 5 mpaka 6 kwa lengo la kuwapa maarifa, stadi na mielekeo ambayo itawasaidia kupambana na maisha yao ya kila siku na pia kuwaandaa kwa elimu ya msingi.

Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018 kilichotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) hivi karibu kinaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi wanaondikishwa katika madarasa ya awali imeporomoka kidogo kwa asilimia 6.2 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Mwaka 2018, wanafunzi milioni1.42 waliandikishwa katika elimu ya awali ikilinganishwa na wanafunzi milioni 1.51 walioandikishwa mwaka 2017. 

Lakini upungufu kama huo ulishuhudiwa katika miaka miwili mfululizo iliyopita. Mwaka 2017 wanafunzi milioni 1.51 waliandikishwa katika elimu ya awali ikilinganishwa na wanafunzi milioni 1.56 walioandikishwa mwaka 2016 ikiwa ni sawa na upungufu wa asilimia 2.9.  

Kitabu hicho kinaeleza kuwa upungufu wa uandikishaji katika elimu ya awali ulitokana na utekelezaji wa sera ya elimu msingi bila malipo ambapo idadi kubwa ya wanafunzi walijiunga darasa la kwanza moja kwa moja bila kupitia elimu ya awali. 

Upungufu huo katika uandikishaji unafikirisha hasa mustakabali wa ngazi hiyo ya elimu ambayo ni muhimu kuwaandaa wanafunzi kumudu masomo ya ngazi zinazofuata.

Hali hiyo ni tofauti kabisa na ilivyokuwa kati ya mwaka 2014 na 2016 ambapo uandikishaji ulikuwa ukiongezeka kabla ya kushuka mwaka mwaka 2017.

Mathalani, mwaka 2016, idadi ya wanafunzi walioandikishwa katika elimu ya awali ilikuwa milioni 1.56 ikilinganishwa na wanafunzi milioni 1.06 mwaka 2015 ikiwa ni ongezeko la asilimia 46.1 ndani ya mwaka mmoja.

Wakati uandikishaji katika madarasa ya awali ukishuka, bado Serikali na wadau wa elimu watakuwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha kunakuwa na uwiano mzuri wa mwalimu na wanafunzi katika madarasa hayo.

Kwa hali ilivyo sasa, bado madarasa hayo yana msongamano mkubwa wa wanafunzi, jambo linalowapa changamoto kuwafikia wanafunzi wote na kuwapatia maarifa na ujuzi unaotakiwa.  

Kitabu hicho kinaeleza kuwa uwiano wa mwalimu mwenye sifa kwa wanafunzi katika elimu ya awali kwa shule za Serikali uliimarika kidogo kwa mwalimu mmoja kufundisha wastani wa wanafunzi 146 (1:146) mwaka 2018 ikilinganishwa na mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi 183 (1:183) mwaka 2017.

Licha ya ahueni hiyo kidogo, hali hiyo ni kinyume na kiwango halisi cha uwiano unaopendekezwa ili watoto wasome vizuri wa mwalimu mmoja kufundisha wastani wa wanafunzi 25  (1:25) kwa madarasa hayo ya awali. 


Zinazohusiana:


Licha ya mabadiliko hayo ya uandikishaji, shule za msingi za umma bado zinaongoza kwa kuandikisha wanafunzi wengi kila mwaka katika madarasa hayo ya awali. Mwaka jana, wanafunzi walioandikishwa walikuwa 1.33 milioni sawa na asilimia 93.8 ya wanafunzi wote waliondikishwa.

Kwa upande wa uandikishaji katika ngazi ya mikoa, mkoa wa Mwanza uliandikisha idadi kubwa ya wanafunzi mwaka jana ambao walikuwa asilimia 7.6 ya wanafunzi wote ikifuatiwa na Kagera asilimia 6.6.

Mchambuzi wa masuala ya elimu na Mhadhiri kutoka Shule Kuu ya Elimu ya Chuo Kikuu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE), Dk Luka Mkonongwa ameiambia www.nukta.co.tz kuwa kushuka kwa uandikishaji katika miaka miwili iliyopita kumechangiwa sana na muamko wa wazazi kuwapeleka watoto shule za msingi kwa wingi kulikochangiwa na elimu bila malipo.

Amesema nafuu, iliyotolewa na sera ya elimu msingi bila malipo iliyoanza kutekelezwa tangu mwaka 2016, imesadia kupunguza idadi ya wanafunzi ambao walikuwa wanakaa nyumbani bila kwenda shule au kuchelewa kuandikishwa katika madarasa ya awali. 

“Hali hiyo ya kushuka kwa uandikishaji katika elimu ya awali ni ya kawaida na siyo kwamba wanafunzi ni watoro hapana. Nadhani wazazi wanawapeleka wanafunzi zaidi darasa la kwanza,” amesema Dk Mkonongwa.

Wakati uandikishaji katika madarasa ya awali ukishuka, bado Serikali na wadau wa elimu watakuwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha kunakuwa na uwiano mzuri wa mwalimu na wanafunzi katika madarasa hayo. Picha|Mtandao.

Wadau wa elimu, Serikali waeleza nini cha kufanya

Dk Luka amesema Serikali haina budi kuongeza uwekezaji katika elimu ya awali hasa kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ikiwemo kujenga madarasa na kununua vifaa muhimu ikizingatiwa kuwa shule nyingi zinakabiliwa na changomoto ya madarasa ya awali. 

Pia juhudi zielekezwe katika kuongeza idadi ya walimu ili kuwa na uwiano mzuri darasani na kuwawezesha walimu kuwafikia wanafunzi wote kwa kiwango kinachohitajika.

“Watoto wasisome wengi kwenye darasa, mwalimu anahitaji kumfikia kila mwanafunzi na kuwa naye karibu. Kama wako wengi hawawezi kupata maarifa ya kumudu elimu ya msingi,” amesema mhadhiri huyo.

Hata hivyo, Serikali imesema inaendelea kuongeza jitihada za kutoa ajira kwa walimu wa elimu ya awali pamoja na kuimarisha mafunzo ya ualimu wa elimu ya awali katika vyuo vya ualimu vya Serikali ili kupata wahitimu wengi na kufikia uwiano unaokubalika.

“Mwaka 2013/14, Taasisi ya Elimu Tanzania, imekusanya maoni ya wadau kuhusu maboresho ya mitaala pamoja na kuchambua mihtasari ya masomo ya elimu ya awali na msingi ili kuinua kiwango cha ubora wa utoaji wa elimu,” alisema Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2019/2020.

Mpaka habari hii inachapishwa,  juhudi za kumpata Msemaji wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) hazikufanikiwa ili kueleza mikakati ya Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu ya awali nchini.