October 8, 2024

TANePS kuleta tija na ufanisi katika sekta ya ununuzi ya umma

Mfumo huo unao kadiriwa kuokoa wastani wa shilling bilioni 34 katika miaka mitano ya kwanza umetayarishwa kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 na Kanuni za Ununuzi wa Umma chini ya Tangazo la Serikali Na. 446 la Mwaka 2013.

  • Ni mfumo wa kielektroniki wa kufanya manunuzi ya serikali.
  • unatarajiwa kuokoa wastani wa Sh 34 bilioni katika miaka mitano ya kwanza.
  • Serikali yasisitiza taasisi zote za ununuzi nchini ziwe zimeungwa katika mfumo huo ifikapo Desemba 31, 2019.

Dar es Salaam. Serikali imeimarisha mfumo wa manunuzi kwa kuanza kutumia mfumo mpya wa kielektroniki (TANePS) ili kueta tija kwa taifa. TANePS inasimamiwa na Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) ambayo ipo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Mfumo huo unao kadiriwa kuokoa wastani wa Sh 34 bilioni katika miaka mitano ya kwanza umetayarishwa kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 na Kanuni za Ununuzi wa Umma chini ya Tangazo la Serikali Na. 446 la Mwaka 2013.

Unatarajia kunufaisha watumiaji wa mfumo huo kwenye mchakato wa zabuni, ununuzi wa bidhaa, mnada wa mtandaoni, malipo ya ada mbalimbali pamoja na usimamizi wa mikataba mbalimbali. 

Kwa kutumia mfumo huo, itaipunguzia Serikali mzigo mkubwa uliokuwa unatokana na matumizi yasiyo na tija ambayo yalikuwa kwenye mfumo wa kawaida.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James amesema mfumo huo  umeanzishwa ili kuiwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha zinazotumika kupitia ununuzi wa bidhaa, huduma na kazi za ujenzi. 

Hadi sasa, mfumo huo wa ununuzi umeanza kutumika ambapo kwa mara ya wanza ulitumika mwezi Machi 2018 ambapo  baadhi ya taasisi za umma zimeunganishwa baada ya kukamilisha taratibu muhimu ikiwemo mafunzo kwa watumiaji wa mfumo huo.​

Unatarajia kunufaisha watumiaji wa mfumo huo kwenye mchakato wa zabuni, ununuzi wa bidhaa, mnada wa mtandaoni, malipo ya ada mbalimbali pamoja na usimamizi wa mikataba mbalimbali. Picha| Mtandao.

Akielezea baadhi ya faida zake, Katibu Mkuu James amesema mfumo huo utasaidia kurahisisha ushiriki wa wazabuni kwenye michakato ya ununuzi na  kuongeza ushindani na ufanisi pamoja na kupunguza muda unaotumika katika mchakato wa zabuni.

“Mfumo huu utaongeza uwazi na kupunguza vitendo vya rushwa ikiwa ni pamoja na kuongeza kiwango cha uwajibikaji kutokana na urahisi wa uhakiki wa michakato ya zabuni inayoendeshwa, kupunguza gharama za ununuzi kutokana na uokoaji wa muda,  pamoja  na kupunguza  muda wa kuandaa vikao na tathmini yake pamoja na kuimarika kwa utunzaji wa kumbukumbu za ununuzi.” alisisitiza Katibu Mkuu.

Wakati huo huo, Serikali imeagiza PPRA kuhakikisha kuwa ifikapo Desemba 31, 2019  taasisi zote za ununuzi nchini ziwe zimeungwa katika mfumo huo.

“Natoa wito kwa wazabuni, taasisi binafsi na za umma  na wananchi kwa ujumla kuungana na Serikali kwa kutoa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha azma ya Serikali  ya kuwa na mfumo wenye tija kwa taifa” amesema James.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Mhandisi Leonard Kapongo amesema baada ya kupatiwa maelekezo hayo Mamlaka ilianza kutoa  mafunzo kuhusiana na matumizi ya mfumo wa TANePS kwa maafisa wa ununuzi na TEHAMA wa taasisi za Umma. 

“Mpaka sasa Mamlaka imefanikiwa kuunganisha taasisi 418, huku  wataalamu waliopatiwa mafunzo kutoka taasisi nunuzi ikifikia 1,600 ambapo mara baada ya kupatiwa mafunzo taasisi zao huunganishwa kwenye mfumo na kuendelea kutekeleza michakato yote ya ununuzi inayofuata” amesema Mhandisi Kapongo.

Kapongo ametoa rai kwa wakuu wa taasisi kuhakikisha kwamba wanatumia mfumo huo kwani ni takwa la Sheria ya Ununuzi. Pia amesema mfumo huo unafaida kwa wazabuni kwa kuwa hawatahitaji tena kutumia makabrasha au kusafiri kwa ajili ya kuwasilisha zabuni zao. 

“Mambo yote hayo yatafanyika kwa njia ya mtandao, yakihusisha kutangazwa kwa mipango ya ununuzi ya mwaka, matangazo mahsusi ya zabuni na Wazabuni waliosajiliwa kuweza kupakua nyaraka za zabuni na kuziwasilisha kwa taasisi nunuzi kwa njia ya mtandao na majibu ya washindi wa zabuni yatatangazwa kwenye mtandao wa mfumo” amesema Mhandisi Kapongo.


Zinazohusiana


Pia Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Balozi Dkt, Marten Lumbanga ameunga mkono mfumo  kuwa utarahisisha kazi na kuweka uwazi kwa mapato ya Serikali yanayoingia kupitia ununuzi kwa taasisi za umma. 

Watoa huduma mbalimbali, wazabuni na makandarasi wameshauriwa kuchangamkia fursa  hizo kwa kushiriki kwenye michakato ya zabuni kwa kujisajili TANePS kupitia tovuti ya mfumo ambayo ni, www.taneps.go.tz ambapo watapata maelekezo mbalimbali ya namna ya kujisajili.