Serikali kuanzisha mfumo wa Tehama kudhibiti michezo ya kubahatisha
Serikali imesema iko mbioni kukamilisha uanzishwaji wa mfumo wa pamoja wa Tehama wa kudhibiti biashara ya michezo ya kubahatisha na kupunguza ushawishi wa vijana kushiriki katika michezo hiyo kupita kiasi.
Serikali imefanya marekebisho katika Sheria ya Michezo ya Kubahatisha ya mwaka 2003 inayomtaka kila anayeendesha michezo ya kubahatisha kuingizwa kwenye mfumo wa Tehama. Picha|Mtandao.
- Mfumo huo utaunganisha michezo ya kubahatisha nchini ili kusimamia mapato.
- Pia utasaidia kupunguza ushawishi wa vijana kushiriki katika michezo hiyo kupita kiasi.
- Serikali yasema inaendelea kutoa elimu kwa vijana juu ya athari za michezo hiyo.
Dar es Salaam. Serikali imesema iko mbioni kukamilisha uanzishwaji wa mfumo wa pamoja wa Tehama wa kudhibiti biashara ya michezo ya kubahatisha na kupunguza ushawishi wa vijana kushiriki katika michezo hiyo kupita kiasi.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji aliyekuwa akizungumza leo (Novemba 13, 2019) Bungeni jijini Dodoma amesema Serikali imejipanga kuunganisha michezo yote ya kubahatisha nchini Tanzania katika mfumo mmoja wa Tehama unaoendelea kujengwa.
Amesema uendeshaji wa michezo ya kubahatisha bila utaratibu na usimamizi thabiti unaweza kuwa na athari hasi kwa jamii ikiwemo kupoteza nguvukazi ya Taifa inayohitajika katika uzalishaji.
Athari hasi ni pamoja na vijana kutumia muda mwingi kucheza michezo hiyo na muda mwingine kucheza katika sehemu ambazo hazijasajiliwa na mfumo wa Tehama uliyowekwa na Serikali.
“Ili kukabiliana na athari hasi zinazotokana na michezo ya kubahatisha, Serikali imechukua hatua zifuatazo; kujenga mfumo wa Tehama utakaotumika kusimamia mapato yatokayo na michezo ya kubahatisha pamoja na kuratibu mwenendo wa wachezaji ili kukabiliana na urahibu wa michezo hiyo,” amesema Dk Kijaji wakati akijibu swali la Mbunge wa Ileje (CCM), Janeth Mbene.
Katika swali lake, Mbene amesema michezo ya kubahatisha inaingiza pato kwa Taifa lakini ina athari kubwa za kimaadili na saikolojia kama ilivyo kwenye dawa za kulevya ikiwa haitaangaliwa kwa umakini.
“Je Serikali imechukua tahadhari zipi kuhakikisha michezo hii inahusisha watu wenye ufahamu wa athari za kutegemea michezo hii na kuwaletea athari kubwa kiuchumi, kijamii na kifamilia na Taifa kwa ujumla,” amehoji Mbene.
Soma zaidi:
Dk Kijaji amesema pamoja na kuanzisha mfumo wa Tehama, wanaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia semina katika mikusanyiko ya vijana kuhusu athari hasi zitokanazo na michezo ya kubahatisha.
Hatua nyingine ni pamoja na kudhibiti uagizaji na uendeshaji holela wa vifaa vya michezo ya kubahatisha hasa mashine za michezo hiyo (Slot Mashine).
“Hatua hizo zinalenga kupunguza ushawishi wa kushiriki michezo ya kubahatisha kupita kiasi na hatari hasi zitokanazo na michezo ya kubahatisha kwa jamii,” amesema Dk Kijaji.
Aidha, Serikali imefanya marekebisho katika Sheria ya Michezo ya Kubahatisha ya mwaka 2003 inayomtaka kila anayeendesha michezo ya kubahatisha kuingizwa kwenye mfumo wa tehama.
Pia Serikali imeanzisha kampeni iliyopewa jina la “Makinika Kijana” yenye lengo la kuwaasa vijana kutokutegemea tu michezo hiyo katika kupata kipato bali wajishughulishe na kazi muhimu zinazokuza kipato cha mtu na Taifa kwa ujumla.