November 24, 2024

BoT yatoa tahadhari matumizi ya fedha za kimtandao Tanzania

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewatahadharisha Watanzania kutojihusisha na fedha za kimtandao na kwa kufanya hivyo ni kinyume cha kanuni zilizopo za fedha za kigeni na kunaweza kusababisha hasara kwa anayehusika.

  • Yasema imegundua matukio mbalimbali yanayohusisha uhamishaji wa biashara na matumizi ya fedha za kimtandao nchini.
  • Yabainisha kuwa fedha hizo ni kinyume cha kanuni zilizopo za fedha za kigeni na kunaweza kusababisha hasara kwa anayehusika.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewatahadharisha Watanzania kutojihusisha na fedha za kimtandao na kwa kufanya hivyo ni kinyume cha kanuni zilizopo za fedha za kigeni na kunaweza kusababisha hasara kwa anayehusika. 

BoT katika taarifa yake iliyotolewa leo (Novemba 12, 2019) imesema  imeshuhudia kuwepo kwa wananchi wanaotumia fedha za kimtandao (cryptocurrencies) katika kufanya malipo hapa nchini. 

Imesema inatambua kuwa kuna matukio ya kuhamasisha biashara ya fedha hizo za kimtandao hapa nchini ili zionekane kama ni fedha halali kwa ajili ya kufanya malipo. 

“Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuutahadharisha umma kwamba uuzaji, uhamasishaji wa biashara hiyo na matumizi ya fedha za kimtandao ni kinyume cha kanuni za udhibiti wa fedha za kigeni,” inasomeka na sehemu ya taarifa hiyo.


Zinazohusiana:


BoT, kama taasisi pekee hapa nchini yenye mamlaka ya kuchapisha noti na kutengeneza sarafu na kuamua fedha halali kwa ajili ya matumizi hapa nchini inautarifu umma kwamba Shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali kwa ajili ya kufanya malipo hapa Tanzania. 

“Fedha zingine za kigeni zinauzwa na taasisi zilizosajiliwa hapa nchini kwa mujibu wa taratibu zilizopo za kubadilisha fedha za kigeni. Fedha hizo zinazonunuliwa zinarudishwa kwenye nchi husika kwa mujibu taratibu zilizopo,” inaeleza taarifa hiyo.

“cryptocurrencies” ni sehemu ya “blockchain”; teknolojia ya mfumo unaomruhusu mtu kutuma au kuhifadhi vitu vyake zikiwemo nyaraka na pesa kwa njia ya mtandao bila kumuhusisha mtu mwingine (third party) au kupitia kwa sehemu nyingine ambayo haihusiki.

Katika teknolojia hiyo ya blockchain ni vigumu mtu yeyote aliyepo kwenye mfumo kufanya uchakachuaji katika masuala ya miamala bila wahusika wote kuthibitisha.

Kwa Tanzania, mfumo huo wa malipo bado haujaanza kutumika rasmi.