October 6, 2024

Rafu uchaguzi Serikali za Mitaa zaendelea kutikisa Bunge la Tanzania

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara amesema Wabunge wa Bunge la Tanzania hawana haki ya kulalamikia mapungufu yaliyojitokeza katika uteuzi wa wagombea wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa bali wale

  • Serikali yasema Wabunge hawana haki ya kulalamikia mapungufu yaliyojitokeza katika uteuzi wa wagombea wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
  • Yasema kama kuna mtu hajatendewa haki atumie taratibu na kanuni zilizowekwa.
  • Wapinzani wamuomba Rais John Magufuli kuingilia kati. 

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara amesema Wabunge wa Bunge la Tanzania hawana haki ya kulalamikia mapungufu yaliyojitokeza katika uteuzi wa wagombea wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa bali wale waliojaza fomu na kuondolewa kwa kukosa sifa za kushiriki uchaguzi huo. 

Kauli ya Serikali inakuja, wakati bado kukiwa na mjadala kwenye jamii, juu ya wagombea wengi wa vyama vya upinzani kuondolewa katika orodha ya wagombea watakaokuwa na sifa ya kuchaguliwa katika uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu. 

Waitara ametoa msimamo huo wa Serikali bungeni leo (Novemba 7, 2019) katika kipindi cha maswali na majibu na kusema wale wote wenye malalamiko bado wana nafasi ya kupata haki ikiwa watafuata kanuni na taratibu za uchaguzi huo. 

“Wabunge wamelalamika sana kwenye Bunge hili, naomba niwaharifu kwamba Wabunge hawana haki ya kuweka mapingamizi na kulalamikia uchaguzi kama wamendewa haki ama la!.

“Wenye haki ya kulalamika ni wale watu wote waliojaza fomu na kusema wameondolewa na utaratibu umeanishwa vizuri kwenye kanunuzi yetu na Waheshimiwa Wabunge na vyama vya siasa wamepewa kanuni hiyo,” amesema Waitara. 

Naibu wa Waziri huyo alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim (CUF) ambaye alitakuwa kujua Serikali ina mkakati gani wa kuwarejeshwa wagombea wote wa vyama vya upinzani waliondolewa ili washiriki uchaguzi.

“Kumekuwa na malalamiko kila kona juu ya tabia mbaya ya kuondolewa kwa wagombea wa upinzani hasa katika uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa unaofanyika Novemba 24 kwa vyama vya ACT Wazalendo, CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi na imeonekana kuna mkakati maalum wa Serikali katika kudhoofisha upinzani hapa Tanzania,” amesema Salim wakati akiuliza swali lake. 

Katika maelezo yake, Waitara amesema yanayozungumzwa bungeni na Wabunge ni tofauti na halisi katika chaguzi hizo, kwa sababu baadhi ya madai ya kuondolewa kwa wagombea wa upinzani siyo ya kweli.

“Kwa mfano Tarime Mjini, Mhe. Mbunge alitoa taarifa hapa kwenye clip (ujumbe wa video) akasema wagombea wote wameondolewa siyo kweli, kwa taarifa za leo asubuhi,” amesema. 


 Soma zaidi: 


Hata hivyo, Naibu Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Ukonga amesema ambao hawajaridhika na maamuzi ya kuondolewa katika nafasi za kugombea walipaswa kuwasilisha pingamizi Novemba 5 na 6 kwa Msimamizi wa uchaguzi. 

“Kama hawajaridhika na maamuzi hayo pia, wanayo fursa mpaka Novemba 9 kwenda kupeleka mapingimizi kwenye kamati ya rufaa. Lakini kama hawajaridhika na maamuzi ya kamati ya rufaa ambayo inapatikana ndani ya Wilaya, wanayo fursa ya siku 30 kwenda kwenye mahakama yoyote kwenda kuweka pingamizi kupata haki,” amesisitiza Waitara.

Amesema utaratibu lazima ufuatwe, uchaguzi utakuwa huru na haki kwa wale ambao watazingatia taratibu na sheria za uchaguzi.

Katika maelezo yake, Waitara amesema yanayozungumzwa bungeni na Wabunge ni tofauti na halisi katika chaguzi hizo, kwa sababu baadhi ya madai ya kuondolewa kwa wagombea wa upinzani siyo ya kweli. Picha|Mtandao.

Wapinzani walia kutotendewa haki

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amemuomba Rais John Magufuli kuingilia kati suala la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kile alichokidai ni kuepusha vurugu na matatizo kwenye uchaguzi huo.

“Kitendo cha kuwanyima fomu wagombea wa upinzani siyo tu hakina tija kwenye ukuaji wa demokrasia, pia ni matumizi mabaya ya hela za umma, huwezi ukafanya semina, kuchapisha nyaraka mbalimbali huku ukijua hakuna uchaguzi bali wagombea wanapita bila kupingwa,” amesema Prof Lipumba jana wakati akiongea na wanahabari jijini Dar es Salaam. 

Nacho Chama Cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema) leo kimeitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu kutoa msimamo kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Chama cha ACT kimesema wagombea wake zaidi ya 2,000 wameenguliwa bila kufuata utaratibu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hichi, Dorothy Semu amesema kamati ya uongozi ya Chama hicho itakaa kikao cha dharura kesho (Novemba 8, 2019) ili kutafakari hatua zaidi za kuchukua.