November 24, 2024

Wadau wakutana kujadili mikakati ya kuendeleza nishati safi ya kupikia

Ni warsha iliyowashirikisha wadau makundi muhimu ya wanawake, sekta binafsi, Serikali, Asasi za Kiraia (Azaki) pamoja na wanahabari.

  • Ni warsha iliyowashirikisha wadau makundi muhimu ya wanawake, sekta binafsi, Serikali, Asasi za Kiraia (Azaki) pamoja na wanahabari.
  • Wapendekeza suluhu ikiwemo elimu kwa jamii ili kuongeza akasi ya matumizi ya nishati hiyo.

Dar es Salaam. Ilikuwa mwisho wa wiki iliyopita Oktoba 29, 2019, wadau wa nishati endelevu walipokutana jijini Dar es Salaam kujadili suluhu zitakazosaidia upatikanaji wa uhakika wa nishati safi, bora na endelevu ya kupikia.

Warsha hiyo iliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia na Nishati Endelevu Tanzania (Tangsen) iliwashirikisha wadau wa makundi muhimu ya wanawake, sekta binafsi, Serikali, Asasi za Kiraia (Azaki) pamoja na wanahabari. 

Ilikuwa ni jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na njia muhimu zinazoweza kutumiwa na jamii kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi ikiwemo gesi asilia, umeme na gesi ya majumbani (LPG).  

Naibu Kamishna wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Innocent Luoga aliyekuwa akizungumza katika warsha hiyo, amesema warsha hiyo ilikuwa muhimu ili kutafuata suluhu zinazofanya kazi katika kuboresha upatikanaji wa nishati bora ya kupikia.

Amesema katika hotuba yake kuwa majadiliano ni muhimu kwa lengo la kutafuta suluhu zinazofanya kazi (workable solutions) ili kupelekea kuongezeka kwa matumizi safi ya  nishati safi, bora na endelevu ya kupikia kwa kuhusisha makundi muhimu mahsusi  kama Wanawake.

“Jitihada za wadau mbalimbali zinahitajika katika kutafuta suluhu ya kudumu na inayofanya kazi kwenye suala la upatikanaji wa nishati bora ya kupikia,” amesema.

Amesema ni ukweli usiopingika kuwa waathirika wakuu wa upatikanaji wa nishati bora ya kupikia ni wanawake ambao hulazimika kubeba jukumu la kutafuta nishati ya kupikia ambayo upatikanaji wake umekuwa mgumu na kuwalazimu kutumia muda wao mwingi kutafuta nishati ya kupikia.

Pia nishati isiyo safi kama ya kuni ina madhara ya kiafya ikiwemo kusababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji. 

Inakadiriwa kuwa ni chini ya asilimia 5 ya Watanzania wote wanapata nishati bora ya kupikia (access to clean cooking solutions). hii inaonesha kuwa watanzania wengi bado hawatumii nishati bora kwa ajili ya kupikia na hivyo jitihada za makusudi zinahitajika katika kupunguza matatizo ya matumizi  nishati yasiyo sahihi.


Zinazohusiana: 


Afisa habari wa Shirika lisilo la kiserikali la Hivos Afrika Mashariki, Caroline Lohome amesema Tanzania ilivyo ni kama Kenya ambapo wananchi wengi bado wanatumia kuni kwa ajili kupikia  huku akisema watoto na wakina mama ndiyo waathIrika wakubwa wa ukusefu wa nishati bora ya kupikia .

Caroline amesema lazima kuwe na sera nzuri ambayo itasaida kuwa na nishati safi na endelevu na yenye gharma nafuu kwa ajili ya matumizi ya kupikia.

Wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Katibu Mtendaji wa Tangsen, Herzon Kajange amesema lengo la warsha hiyo ni kuongeza uelewa kuhusu aina mbalimbali za nishati, teknolojia pamoja na fursa zinazojitokeza katika sekta ya nishati.

Amesema kitaundwa kikosi kazi kwa ajili ya kufanyia kazi mapekezo yaliyotolewa na washiriki  kwa ajili ya kufanyia maamuzi ili kuhakikisha kuwa wanaume na wanawake wanafaidika na nishati endelevu .

Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, Luoga amesema Serikali itaendelea kuboresha sera na mikakati ili kuchochea matumizi bora ya nishati ya kupikia.