October 6, 2024

Mgawanyo wa jinsia bungeni tangu Tanzania ipate uhuru

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema kuna kazi ya kufanya kuongeza idadi ya wanawake wanaoingia bungeni, ikizingatia kuwa tangu nchi imepata uhuru mpaka sasa, wabunge wanawake ni asilimia 15 tu.

  • Tangu nchi imepata uhuru, idadi ya wabunge walioingia bungeni mpaka sasa ni 3,041.
  • Idadi ya wabunge wanawake mpaka sasa ni asilimia 15 tu.
  • Spika Ndugai asema kuna kazi ya kufanya kuziba pengo la kijinsia bungeni.

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema kuna kazi ya kufanya kuongeza idadi ya wanawake wanaoingia bungeni, ikizingatia kuwa tangu nchi imepata uhuru mpaka sasa, wabunge wanawake ni asilimia 15 tu. 

Spika Ndugai aliyekuwa akizungumza leo (Novemba 5, 2019) wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 17 wa Bunge Jijini Dodoma, amesema tangu nchi imepata uhuru idadi ya wabunge walioingia bungeni mpaka sasa ni 3,041. 

Kati ya hao, wabunge wanawake ni 484 sawa na asilimia 15 au pungufu zaidi ya mara sita ya wabunge wanaume. 

Amesema baada ya uhuru mwaka 1961, Bunge la 1961 hadi 1965 lilikuwa na wabunge 81, kati ya wabunge hao, wabunge wanawake walikuwa sita tu sawa asilimia 7.4. 

Bunge lililofuata la 1965 hadi 1970 wakaongezeka wakawa wabunge 183, wabunge wanawake wakapungua wakawa watano ambapo wakati huo ili kuingia bungeni lazima uwe mbunge wa jimbo (kuchaguliwa).

“Kwa hiyo kuna ongezeko kubwa, nadhani siyo haba asilimia 15 ya wabunge wote kwa sababu kule nyuma kulikuwa na tofauti kubwa, ndiyo maana sasa hivi japo tumesogea sana lakini bado hatujafika mbali,” amesema Spika Ndugai.


Zinazohusiana:


Kwa upande wa vyama, idadi ya wabunge wote tangu uhuru, kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni 1,294. Idadi ya wabunge wanawake wa chama hicho ni 256 sawa na 19.8 ya wabunge wanawake walioingia bungeni.“Wabunge wote wa vyama vya upinzani ni 328. Tangu uhuru idadi yote ya wabunge wanawake wa upinzani 124. Upinzani umeingiza asilimia 40.3 ya wabunge wanawake,” amesema Spika Ndugai.

Hata hivyo, amebainisha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya kuongeza idadi ya wabunge wanawake ili kuongeza usawa wa kijinsia bungeni.

“Kwa hiyo tuna kazi ya kufanya ili kuwezesha wakina mama zaidi kupitia vyama vyetu vyote tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea,” amesema.