Kampuni tatu za nje kujenga kiwanda cha mbolea cha Sh4 trilioni Lindi
Serikali imesema ipo kwenye mazungumzo na muungano wa wawekezaji watatu kutoka Denmark, Ujerumani na Pakistan kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuzalisha mbolea mkoani Lindi.
- Kampuni hizo tatu zinatoka nchi za Ujerumani, Denmark na Pakistan.
- Haijawa bayana ni lini ujenzi wa kiwanda hicho utaanza.
- Serikali yasema kitaajiri wafanyakazi 5,000.
Dar es Salaam. Serikali imesema ipo kwenye mazungumzo na muungano wa wawekezaji watatu kutoka Denmark, Ujerumani na Pakistan kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuzalisha mbolea mkoani Lindi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof Palamagamba Kabudi amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam leo kuwa kiwanda hicho kitagharimu Dola za Marekani 1.9 bilioni (zaidi ya Sh4 trilioni).
Prof Kabudi amesema majadiliano na wawekezaji hao yanaendelea japo hakuweka bayana ni lini watakamilisha mazungumzo hayo na ujenzi wa kiwanda hicho utaanza.
“Kampuni hizo ni Ferrostaal ya Ujerumani, Hardol Topsoe ya Denmark na Fauji Fertilisers ya Pakistan ambayo itashughulika na masuala ya utawala wa kiwanda hicho,” amesema Kabudi wakati wa mkutano wake na wanahabari kuhusu mkutano wa mawaziri wa mambo wa nje wa Afrika na nchi za Scandinavia (Africa Nordic Foreign Affairs Ministers meeting).
“Mradi huu wa kiwanda cha kuzalisha mbolea utaajiri watu 5,000,” amesema Prof Kabudi akieleza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kushawishi wawekezaji wa nje wakiwemo wa nchi za Scandinavia kuja kuwekeza Tanzania.
Mkutano wa mawaziri hao utafanyika jijini hapa Novemba 7 na 8 na utahusisha mawaziri kutoka katika mataifa 34 wakiwemo watano kutoka nchi za Denmark, Iceland, Norway, Finland na Sweden. Rais John Magufuli anatarajiwa kuzindua mkutano huo wa 18 tangu uanzishwe mwaka 2000.
Zinazohusiana:
- Dawa ya Ejiao inavyohatarisha kutoweka kwa punda Afrika Mashariki
- Chamwino kujenga kiwanda cha kuzalisha bidhaa za ngozi
Mbali na mkutano huo, Prof Kabudi ambaye amekuwa kinara wa majadiliano katika miradi mbalimbali ya uwekezaji na Serikali, amesema Tanzania inaamini wawekezaji wa mradi wa kusindika gesi asilia (LNG) watafikia muafaka wao wenye hivi karibuni ili kuendelea na mradi huo unaogharimu Dola za Marekani bilioni 30.
Amesema hadi sasa Serikali inaendelea na mazungumzo na kampuni ya Equinor kutoka Norway kwa ajili ya uwekezaji wa masuala ya gesi baada ya kampuni hiyo kukubali kuendelea na uwekezaji katika mradi huo.
Prof Kabudi amesema makubaliano ya Equinor na Shell yalikuwa wachangie ujenzi wa miundombinu ya gesi na kuchakata lakini kila mtu ana kitalu chake na kwamba hata Equinor wakikamilisha miundombinu hiyo watakayoijenga bado wataweka fursa ya kuunganisha kwa kampuni nyingine.
“Tofauti yao ilikuwa ni speed (kasi) ndiyo maana tukasema yule anaona anayeweza kuanza, aanze. Lakini kuanza kwao, tunafanya mazungumzo na wote kwa sababu hatuwezi kuwaacha Shell mwenye kitalu namba 4 na namba 1…hatuwezi kumucha.
“Bado tunaamini wao wenyewe wataendelea kuzungumza lakini tulipoona mazungumzo yao yatachukua muda mrefu ndiyo maana tuliafikia na Equinor kama wao wanaweza kuanza waanze kwa sababu mchakato wake ni wa miaka mingi,” amesema.
Kwa muda mrefu kumekuwa na ucheleweshaji wa kuanza ujenzi wa mradi huo mkubwa wa kuchakata gesi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kucheleweshwa kwa makubaliano baina ya Serikali na wawekezaji hao na baina ya wawekezaji wenyewe.
“Tunaamini mbele ya safari wataashirikiana. Wao wakiafikiana sisi tutachukua mazungumzo yao,” amesema Prof Kabudi.