November 24, 2024

Serikali yatoa onyo wanaoingiza mifuko mbadala isiyo na viwango

Imebainika kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanaingiza na kuuza mifuko mbadala isiyokidhi vigezo, jambo linalochochea uharibifu wa mazingira.

  • Imebainika kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanaingiza na kuuza mifuko mbadala isiyokidhi vigezo, jambo linalochochea uharibifu wa mazingira. 
  • Imesema watu hao ni sawa na wahujumu uchumi na watachukuliwa hatua stahiki za kisheria. 

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea na utekelezaji wa azimio la kupiga marufu ya matumizi ya mifuko ya plastiki, imebainika kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanaingiza na kuuza mifuko mbadala isiyokidhi vigezo, jambo linalochochea uharibifu wa mazingira.

Serikali ilianza kutekeleza azimio hilo Juni mosi mwaka huu ambapo mifuko ya plastiki iliondolewa sokoni na uzalishaji wake ulisitishwa ili kupisha mifuko mbadala rafiki wa mazingira. 

Taarifa iliyotolewa kwa umma leo (Novemba 4, 2019) na Ofisi ya Makamu wa Rais inayosimamia mazingira, imeeleza kuwa kumeanza kujitokeza uvunjifu wa sheria katika uzalishaji na uingizaji wa mifuko mbadala (Non woven plastic bags).

“Baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakiingiza/zalisha mifuko mbadala aina ya non woven plastic bags ambayo haikidhi vigezo tajwa,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Vigezo vinavyohitajika kuzingatiwa katika uzalishaji wa mifuko mbadala kwa mujibu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mifuko hiyo inatakiwa kuwa na uzito usiopungua gramu 70 za mita za mraba na  iwe na uwezo wa kurejelezwa (Recyclable),


Zinazohusiana:


 Pia inatakiwa iweze kuonyesha uwezo wa kubeba (Carrying capacity) na kuthibitishwa na TBS.

Aidha, kumekuwa na matumizi yasiyokubalika ya mifuko myepesi na laini (Tubings) kubebea bidhaa. Ofisi ya Makamu wa Rais inasema mifuko hiyo inapaswa kutumika kama vifungashio vya bidhaa maalum na viwe lakiri ili kuzuia kuongeza bidhaa nyingine katika kifungashio hicho. 

“Kwa siku za hivi karibuni mifuko hii laini imekuwa kama vibebeo, jambo ambalo ni kosa kisheria. Hatua ya kuongezeka kwa matumizi yasiyo sahihi ya mifuko tajwa inaanza kuleta athari katika mazingira,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo. 

Hata hivyo, Kikosi Kazi cha Taifa cha kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc) pamoja na Kamati za Mikoa na Wilaya wataendesha operesheni  ili kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaokiuka au kupuuza agizo hilo. 

“Kumbuka mazingira ndiyo yanayolea uchumi wa Taifa, hivyo anayeharibu mazingira ni sawa na mhujumu uchumi. Kwa muktadha huo watakaobainika kuvunja sheria watachukuliwa hatua stahiki,” inaeleza taarifa hiyo kwa umma.